Waziri Kiongozi, Uwaziri mkuu hawawezi kuwa rais?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
WAZIRI Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha

MCHAKATO wa kusaka mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka huu, umethibitisha kwa mara nyingine kwamba nafasi ya Waziri Kiongozi au Waziri Mkuu si njia ya kutumia kuufikia urais.

Kuanguka kwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Dk. Mohammed Gharib Bilal, ni mwendelezo tu wa jinsi nafasi hii isivyokuwa na baraka kukwea juu zaidi kisiasa nchini.

Kuna mlolongo mrefu wa jinsi viongozi waliopata kuwa mawaziri wakuu au mawaziri viongozi walivyojaribu kwa nyakati tofauti kuwa marais wa ama Zanzibar au Tanzania, lakini walikwama kila walipojaribu.

Mwaka 1995 akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Cleopa David Msuya, alijaribu kuwania urais wa Tanzania kupitia CCM, lakini pamoja na mafanikio aliyopata kwa kuingia hatua ya tatu bora, ambayo walipigiwa kura katika Mkutano Mkuu, hakufanikiwa kupata kura za kutosha kuwa mgombea urais.

Msuya alipambana na akina Benjamin William Mkapa (aliyeshinda) na Jakaya Kikwete aliyetolewa katika raundi ya pili.

Mwaka 2005 aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, naye alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya CCM kuwania urais.

Ingawa jina lake lilipitishwa na Kamati Kuu kwenda Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupigiwa kura, hakuvuka ngazi hiyo. Majina matatu yaliyopitishwa ngazi hiyo kwenda Mkutano Mkuu ni Kikwete, Dk. Salim Ahamed Salim na Profesa Mark Mwandosya. Kiwete aliwabwaga wenzake kwenye Mkutano Mkuu.

Mbali na mawaziri hao wawili waliojaribu kuwania nafasi hiyo kuwa marais, pia waliopata kuwa mawaziri wakuu, kama John Malecela alijaribu mara mbili, mwaka 1995 na 2005, lakini jina lake liliishia Kamati Kuu; Joseph Warioba mwaka 1995 naye alijaribu, lakini naye aliishia NEC kama Sumaye.

Kwa upande wa Zanzibar, aliyekuwa Waziri Kiongozi zama Mzee Ali Hassan Mwinyi, Maalim Seif Shariff, alijaribu kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar zama za chama kimoja, lakini haikuwa riziki.

Lakini, baya zaidi siasa za visa ndani ya CCM zilimsukuma mwanasiasa huyu shupavu nje ya CCM, baada ya kuzushiwa mengi.

Harakati za Maalim Seif siyo tu hazikumfikisha Ikulu akiwa CCM, bali hata akiwa kambi ya upinzani ambako amejaribu mara tatu kuwania nafasi hiyo bila mafanikio. Mwaka huu atatupa karata yake kwa mara nne; tusubiri tuone.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2000, Dk. Bilal alijitosa katika kinyanganyiro cha kurithi mikoba ya Rais wa awamu ya tano wa Zanzibar, Dk. Salimn Amour, wakati huo akiwa Waziri Kiongozi, kama walivyokuwa watangulizi wake. Naye hakufanikiwa, kwani alibwagwa kwenye ngazi ya NEC na Rais anayemaliza muda wake, Amani Karume.

Dk. Bilal alijaribu tena mwaka 2005, lakini jina lake liliishia tu Kamati Kuu ya CCM kwa kile kinachoitwa ‘utamaduni wa CCM wa kumwachia rais aliyeko madarakani vipindi viwili, na bila kupingwa anapowania kipindi cha pili’.

Mwaka huu, Dk. Bilal alijitokeza tena, kwa bahati jina lake likafika NEC, lakini pamoja na Waziri Kiongozi wa sasa, Nahodha, wamebwagwa na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein. Tena anguko kubwa!

Kwenye orodha hii, yaani mawaziri wakuu na mawaziri viongozi waliowahi kukalia viti hivyo vikubwa nchini na kujaribu kukwea zaidi na kushindwa, wanafanya nafsi ya urais kuwa ngumu kwa wakalia viti hivyo.

Hivyo ndivyo ilidhihirika kwa akina Malecela, Msuya, Dk. Salim, Warioba, Sumaye, Maalim Seif, Dk. Bilal, na sasa Nahodha, wote hawa wamekwama kukwea zaidi hadi kwenye urais.

Kwa hiyo, mtu anapotazama nafasi ya Waziri Mkuu au ya Waziri Kiongozi, anapata shida kujua inakuwaje pamoja na nguvu zote za ofisi hiyo, akiwa ni mtendaji na masimamizi mkuu wa shughuli za serikali akimsaidia Rais, wanashindwa kujenga kukubalika kwao na hivyo kuwa chaguo la wengi katika kusaka kuteuliwa kuwania urais? Hili ni swali la kifalsafa zaidi.

Ni dhahiri kazi ya Waziri Mkuu au Waziri Kiongozi ni ya ukiranja mkuu, ni nafasi ambayo aghalabu husababisha waliokalia kiti hicho kukanyaga vidole vya wale walioko chini yao; ni kazi inayotazamwa kama ngazi muhimu kwa shughuli za serikali kufanikiwa au kushindwa.

Katika utekelezaji wa majukumu wa namna hii katika nchi kama yetu ambayo kiongozi mchapakazi huonekana adui na yule asiyewajibika, kwa vyovyote kuonekana mzuri, ni rahisi zaidi kujijengea maadui kuliko marafiki wa kweli ambao wako tayari kupambana kufanikisha harakati kama za kuwania urais.

Pengine matokeo haya ya mawaziri viongozi na mawaziri wakuu kukwama kuupata urais ni mkakati maalum wenye nguvu zilizo nje ya wanadamu kwamba viti hivyo ni kwa ajili ya kutumika si kujijengea himaya kwa maana ya kusaka nafasi ya juu zaidi, kwa sababu yenyewe ni neema tosha ambayo haina sababu ya kumfanya aliyeikalia kuanza kuhangaika.

Ni neema inayowasilisha ujumbe kwa wanaobahatika kukalia kiti hicho kutambua, kwamba kwa kuwa wateule miongoni mwa mamilioni ya Watanzania kukalia kiti hicho wamefika, kwa hiyo wawajibike kwa kutekeleza wajibu wao sawasawa.

Wafanye hivyo kwa sababu wakijielekeza kupanga mikakati ya kupanda kimadaraka baadaye hawatafanikiwa, ni kupoteza muda na badala yake wajielekeze kutumika zaidi ili watakapoondoka madarakani wakitazama nyuma waone alama ya utendaji uliotukuka walioacha nyuma.

Hata hivyo, nadharia hii inaweza isiwe na nguvu sana kwa sababu tu hadi sasa hajapatikana waziri mkuu kuwa rais kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa waziri mkuu kwa muda kabla ya kuuachia madaraka hayo kwa Rashidi Kawawa, ila kitu kinachowakwaza ni kujipanga.

Kwamba kujipanga kisiasa ili kufikia kiti cha urais inajumuisha nini hasa? Je, ni kutumia rasilimali za serikali kujiimarisha, au ni kujiimarisha kwa wananchi, kwa wapiga kura au ni kuwa mwadilifu na mnyenyekevu tu kwa wananchi?

Hili ni swali gumu zaidi kujibu, ila kuna dalili kwamba pengine kutokujulikana sana kwaweza kuwa na hasara na faida. Kama ilivyokuwa kwa Mkapa ambaye alifika kileleni huku akiwa amepuuzwa miongoni mwa vigogo waliokuwa wamejitosa kwenye mpambano; au kwaweza kuwa ni kujipanga na kujitangaza kama alivyoanza Kikwete mapema baada ya kuangushwa mwaka 1995?

Hakuna jibu la moja kwa moja, ila kupanda na kukwea hadi juu kwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa haiba yake na mafanikio ya kisiasa aliyofikia ni aina nyingine ya somo kwa wote wanaokalia kiti cha ama Waziri Mkuu au Waziri Kiongozi kama wakitaka kupaa zaidi.

Hakuna ubishi kwa miaka takribani ambayo Dk. Shein amekuwa madarakani, kwanza kama msaidizi namba moja wa Rais Mkapa, lakini pia kama msaidizi namba moja wa Rais Kikwete, amethibitisha kuwa ni mwadilifu, msikivu na asiyekuwa na makuu.

Ndiyo maana leo hii miaka yake takribani 10 kwenye nafasi ya uongozi, akiwa mtu wa pili, ni vigumu mno kumpaka matope, achilia mbali kumkuta na waa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: