Waziri Kombani ndani ya sakata la Jery Muro


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly version
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani anachunguzwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, MwanaHALISI limeelezwa.

Lakini Kombani alipoulizwa juzi Jumatatu, kuhusu tuhuma hizi, alikataa kujadili lolote, badala yake alitaka mwandishi aende ofisini kwake Dodoma.

“Hivi gazeti lenu halina mwakilishi Dodoma? Mimi siwezi kuzungumza kupitia simu ya mkononi…Ukitaka njoo ofisini tujadili,” alisema Kombani kwa sauti ya upole.

Waziri Kombani ametajwa kuhusika na kuingilia mchakato wa zabuni na kuipa kazi za serikali kampuni aliyo na uhusiano nayo.

Kampuni ambayo waziri Kombani anatuhutumiwa kuibeba, imefahamika kuwa ni Bicem Investment and General Service Co. Limited (BICEM) iliyopata zabuni katika Halmashauri ya Bagamoyo na Manispaa ya Kinondoni.

Kwa mujibu wa nyaraka za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Kombani ni mmoja wa waanzilishi wa kampuni hiyo yenye makao makuu Kinondoni, Dar es Salaam iliyoanzishwa mwaka 2008.

BICEM ilisajiliwa 8 Oktoba 2008 na kupata hati ya usajili Na. 67835.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa ingawa Kombani haonyeshwi tena kuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni, hisa zake 250 “aliziwekeza” kwa jamaa zake wa karibu.

Zabuni zote mbili zilipatikana akiwa tayari Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), jambo ambalo limeelezwa kuwa ni “mgongano wa maslahi.”

Wanaodaiwa kulinda hisa za Kombani katika kampuni ya BICEM ni Goodluck Mlinga mwenye hisa 175 na Doreen P. Kiwango mwenye hisa 150. Hawa wawili wametajwa kuwa “ndugu” zake.

Wenye hisa wengine ambao wanaonyeshwa kwenye barua ya kuombea zabuni Bagamoyo ni Michael Andrew, Mecktridis F. Mdaku na Mika Libe Wakuchikonja.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, kampuni ya BICEM haikuwa miongoni mwa makampuni matatu yaliyoomba zabuni ya uwakala katika halmashauri ya Bagamoyo.

Zabuni hiyo ilihusu kukusanya ushuru wa kokoto, mchanga, kifusi na mawe. MwanaHALISI limefahamishwa kwamba BICEM iliingizwa katika zabuni siku tatu baada ya zabuni kufunguliwa na ililipa ada ya Sh. 50, 000 tu.

Stakabadhi ya malipo kwa BICEM ni Na. 323438 ya tarehe 2 Novemba 2009. Kwa tarehe hii, zabuni zilikuwa tayari zimefunguliwa, jambo linaloonyesha kampuni hiyo ilibebwa na mamlaka husika.

Kampuni ya BICEM ilipewa zabuni ya kukusanya ushuru wa madini na ushuru katika soko la Mfavesco katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni tarehe 27 Mei 2009.

Kazi hiyo iliyotolewa kwa barua yenye Kumb. KMC/CTB/ AWD/170/2008/09 ilitoka miezi miwili baada ya kuingia kwa Mika Libe Wakuchikonja, anayedaiwa kuwa mtoto wa mtendaji mmoja wa manispaa ya Kinondoni (jina tunalo).

Tuhuma nyingine ambazo vyombo vya dola vinasemekana kuchunguza ni pamoja na waziri kupewa tenda na kununuliwa gari linalodaiwa kufanya kazi binafsi mkoani Morogoro.

Inadaiwa hisani hizo zinalenga kulainisha waziri ili alinde watendaji wa halmashauri ya Bagamoyo ambao wamesimamishwa kazi.

Watendaji Bagamoyo ambao tayari wamesimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na ambao inadaiwa ndio Kombani alikuwa analinda ni pamoja na mweka hazina Michael Karol Wage.

Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji Rhoda Nsemwa, Ofisa Mipango, Aloyce Gabriel, Mkaguzi wa Ndani, Abdul Mwinyi na Ofisa Kilimo, Mifugo Ushirika, Naftal Rhemtullah.

Habari kutoka serikalini zinasema kampuni ya BICEM ndiyo chanzo cha tuhuma za kuomba rushwa zinazokabili Jerry Muro, mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Muro na wenzake wawili, Edmud Kapama na Deogratias Mgasa wanatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh. 10 milioni kutoka kwa aliyekuwa Mweka Hazina wa Bagamoyo, Michael Wage.

Habari kutoka ndani ya vyombo vya dola vinavyofanya uchunguzi zinasema utawala umefadhaishwa na umewekwa katika wakati mgumu juu ya hatua ya kuchukua.

Aidha, kutokea tuhuma dhidi ya waziri na mwandishi wa chombo cha serikali, juu ya masuala yenye utata, kunaiweka pingu serikali, ameeleza mmoja wa watoa taarifa.

Habari za polisi kutoka serikalini zinasema Wage anachunguzwa kuhusu mali alizonazo na madai ya kutenda upendeleo kwa kampuni yenye uhusiano na waziri Kombani.

Ni Wage ambaye anadaiwa kuwa chanzo cha kukamatwa kwa Muro na wenzake kwa madai kuwa “wangemlipua” kwa kutoa taarifa zake iwapo asingewapa mulungula.

Unadaiwa kuwa Muro na wenzake walisafiri hadi Morogoro na kuorodhesha mali kadhaa za Wage, zikiwamo nyumba za kulala wageni.

Mtoa taarifa anasema mwingiliano wa kesi ya Muro na tuhuma zinazomkabili Kombani, vinaiweka serikali katika wakati mgumu.

Mtoa taarifa anasema vyombo vya dola vinachunguza tuhuma za Kombani kunufaika na fedha kutoka halmashauri ya Bagamoyo na madai kuwa mmoja wa watumishi hao alitoa fedha kwa waziri.

Vilevile vyombo vya uchunguzi vya dola vinatajwa kuchunguza mahusiano kati ya Kombani na mmoja wa watumishi waliofukuzwa kazi na Pinda.

“Kwa utamaduni uliokwishajengeka – wa kutokamata viongozi, kuwasimamisha, kuwaondoa kwenye vyeo au kuwahamisha ili kufanya uchunguzi, Kombani aweza kuibuka kidedea,” ameeleza mhadhiri mmoja wa chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa BRELA, wakurugenzi wa kwanza wa BICEM ni Joachim Contantine Nkwabi wa S.L.P 12185, Sinza Mori, Plot Na. 18B2, Dar es Salaam ambaye hivi sasa ni Katibu Mtendaji.

Wengine ni Celina Kombani wa Plot Na. MC 28, Mikocheni, Dar es Salaam, mwenye anuani ya posta 1923, Dodoma na Doreen Kiwango wa Plot Na. KNY 124, Tabata Kinyerezi, na S.L.P. 1573, Dar es Salaam.

Mwingine ni Mecktridis Mdaku wa Plot Na. KND 48, Tabata Kinyerezi. Katika fomu ya usajili BRELA, Mdaku ametumia S.L.P. 1573, Dar es Salaam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: