Waziri Mansour, ZECO walikosea nchi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 10 March 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Waziri Mansour Yusuf Himid

UMEME. Umeme ni maendeleo. Ni uchumi. Umeme ndio maisha. Kama yalivyo maji, umeme nao ni bidhaa adhimu kwa maisha ya mwanadamu.

Lakini wanadamu walioko kisiwani Unguja, hawanao kwa miezi mitatu sasa. Tangu tarehe 10 Disemba mwaka jana, hawajapata manufaa ya umeme.

Maelezo yaliyotolewa awali kuhusu ukosefu huo wa umeme, ni kwamba kulitokea hitilafu ya mitambo kwenye kituo kikuu cha kupokelea umeme cha Fumba, kilichoko kilomita 15 hivi kutoka mji wa Zanzibar.

Fumba ndipo kilipo kituo cha kupokelea umeme wa Gridi ya Taifa uliofikishwa Zanzibar mwaka 1976 kwa njia ya waya zilizotandikwa chini ya bahari kutokea Ras Kilomoni, eneo la pembezoni mwa mwambao wa bahari, kaskazini mwa bandari ya Dar es Salaam.

Umeme huu huzalishwa Kidatu mkoani Morogoro kwa kutumia nguvu za maji ya mto Ruaha. Kutoka hapo, unafikia Ubungo, Dar es Salaam na hatimaye kupelekwa Ras Kilomoni.

Hapo ndipo husafirishwa kwa waya za chini ya bahari mpaka Fumba. Kituo cha Fumba kinapeleka umeme Mtoni ambako mtandao wa kuusambaza kwa wateja umejengwa.

Mfumo wa waya za chini ya bahari ulifungwa mwaka 1976 na wataalamu wa kizungu kutoka kampuni moja ya Norway ambayo ndiyo pia ilifunga mitambo iliyopo Fumba.

Wataalamu hao walisema uhai wa mfumo huo ni miaka 20 lakini ukitunzwa vizuri, kwa maana ya kufanyiwa matengenezo madogo mara kwa mara, unaweza kudumu kwa miaka mitano zaidi.

Bali ukipita hapo na bado ukawa unafanya kazi, basi ifahamike kwamba wakati wowote unaweza kukataa kufanya kazi. Maana yake utasambaratika tu.

Huo ndio mtizamo wa kitaalamu kwani wao wanajua vyema uhai wa waya zilizotumika ambazo zimezikwa chini bahari mahali kwenye chumvi ambayo inaharibu haraka kitu chochote kile.

Mei 2008, ilitokea hitilafu kituoni Fumba na kusababisha umeme kuzimika. Vifaa kadhaa viliharibika kwenye mfumo wa kupokelea umeme.

Uzembe uliofanywa na Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) na uingiliaji usiofaa wa wanasiasa katika suala hilo lililohitaji zaidi ufundi, ukasababisha matengenezo kuchelewa kufanywa.

Serikali iliamrisha menejimenti ya shirika kutogusa chochote hadi wafike wataalamu kutoka Norway. Aibu ilioje kwamba hata mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wenye ushirikiano wa karibu na ZECO, walikatazwa kutia mkono.

Matokeo yake ilichukua muda wa mwezi mmoja ndipo mafundi wakafanikiwa kutengeneza na hatimaye kurudisha huduma ya umeme.

Maharibiko yale, yalikuwa dalili mbaya za mapema kabisa kutuonyesha kuwa wakati wowote mfumo wa mitambo ya kupokelea umeme Fumba, utasambaratika.

Serikali haikuchukua hatua madhubuti kutafuta ufumbuzi. Zipo taarifa kuwa Wizara ya Maji, Nishati na Ardhi, ilipokea ripoti maalum ya ZECO kuhusu hali mbaya ya mitambo ya Fumba na kutoa mapendekezo yake juu ya hatua za ufumbuzi, lakini shirika halikupata mrejesho.

Mwaka mmoja baadaye, tatizo kubwa zaidi likatokea kituoni Fumba. Vifaa vikaharibika na kusimamisha huduma muhimu. Bado ikalazimika wasubiriwe wazungu wa Norway na Afrika Kusini kuja kutengeneza.

Kweli, hadhari haikuchukuliwa, athari zimetokea; kwa kuwa ufa haukuzibwa, inabidi kujenga ukuta. Na serikali haikusikia la mkuu, yajikuta imevunja guu. Yenyewe imekosa mapato mengi ya kodi.

Hoteli nyingi zimesimamisha huduma ya kupokea watalii maana wengi walifuta kutembelea nchi isiyo umeme. Ni athari, athari, athari kila mahali.

Wenye hoteli nao kwa kuwa hawana mapato ya maana wakalazimika kupunguza wafanyakazi. Wengi wakapewa likizo bila malipo.

Ukosefu wa umeme umeleta adha kubwa Zanzibar. Ulizidisha umasikini kwa familia nyingi zinazoutegemea. Ajira za maelfu ya watu zimekatika na kuzidisha gharama za maisha.

Watu kadhaa walifariki dunia kutokana na matumizi ya jejereta. Baadhi ya jenereta zililipuka. Katika nyumba moja eneo la Bububu, moshi wa jenereta ulijaa ndani na kutengeneza hewa chafu ambayo waliokuwemo ndani walipovuta, walifariki.

Ukosefu wa umeme ulisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira. Watu wachache mno ndio wanatumia jenereta majumbani na katika sehemu za kazi.

Mafuta mengi yakisambaa hewani kwenye eneo dogo, huchafua hewa ambayo binadamu na wanyama wanaitegemea ili kuishi.

Majumbani kuna shida kubwa ya maji kwa kuwa mashine za kusukumia maji hazina umeme. Baadhi ya vituo vya maji vina jenereta zake bali nyingi ni mbovu.

Watu wa Unguja wanaujua vizuri umeme. Zanzibar ni moja ya nchi chache katika Afrika zilizopata umeme miaka mingi iliyopita hata kabla ya uhuru.

Ilikuwa na vinu vya umeme vikitumia mafuta ya kulainisha mitambo (IDO). Vyote vimekufa na vingine viliharibiwa kihuni. Hakuna jitihada za kununua nyingine.

Umeme umetumika vizuri kwao katika kujenga jamii. Wameutumia kujenga nchi yao. Kutokana na umeme, idadi kubwa ya watu wamekuwa wakijishughulisha kutafuta riziki zao kwa namna mbalimbali.

Sehemu kubwa ya watu katika nchi inayoelekea kuwa na watu milioni moja, wanaishi kwa kutegemea ajira binafsi katika nyanja tofauti.

Wafanyakazi katika sekta ya umma hawazidi 30,000. Hakika, kulingana na utafiti uliofanywa miaka ya mwisho ya 1990 na kampuni ya Uingereza, wafanyakazi wa serikali walikuwa 28,000.

Waliobaki wanaishi kwa kazi za uzalishaji mali kupitia karakana za kutengeneza magari, vifaa vya umeme, ufundi seremala, mitambo na kuunganisha vyuma.

Shughuli nyingine ni viwanda vidogo vya ushoni, kufyatua matufali, kuoka mikate, kutengeneza keki na ice cream, juisi, majokovu ya kuhifadhia samaki na vinywaji vingine baridi.

Umeme uwe umerudi au haukurudi jana kama ambavyo menejimenti ya ZECO waliahidi, pigo ililopata nchi ni kubwa kihistoria.

Hakukuwa na mtiririko wa kupasha habari wananchi kuhusu maendeleo ya matengenezo. Labda serikali walidhani ni haki yao kunyima wananchi habari. Ilikuwa wajibu wao na imewakatili wananchi. Ni jinai.

Kwanini isielezwe kwamba kulikuwa na mzaha katika suala hili. Kuficha taarifa ni mfumo wa kishetani unaopendwa na madikteta.

Basi si dhambi kusema serikali ibebe lawama za kuchelewa kununua vipuri na kufikisha Fumba kwa wakati uliopendekezwa na wataalamu.

Ajabu ni kwamba wakati nchi imepoteza mabilioni ya shilingi katika mapato na wananchi wameumia sana kimaisha, bado tabia ya serikali ni ileile ya kufanya mzaha.

Ilifanya kweli vinginevyo isingetumia zaidi ya Sh. 700 milioni kugharamia sherehe zilizofanyika Pemba.

Hata kama wamekataa kuwajibika, itabaki tu kwamba waziri Mansour Yussuf Himid na wakuu wa ZECO waliwakosea wananchi.

0
No votes yet