Waziri Masha hasemi ukweli


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 July 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

SAKATA la mradi wa vitambulisho vya taifa, wenye thamani ya Sh. 200 bilioni bado halijafa. Waziri Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, wala hajajibu hoja za wabunge na umma kwa jumla, juu ya kilichosababisha mradi huo kukwama.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Anna Komu, alihoji bungeni, "Mheshimiwa Spika, kuna nini katika vitambulisho? Nani amekwamisha mradi huu? "

Badala ya kujibu hoja ya Komu, Masha ameishia kulalama, kutuhumu na kushutumu wenzake ndani ya serikali.

Alisema kigogo mmoja wa ikulu anamsakama na amemzuia kutimiza wajibu wake, wakati yeye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia mradi.

Hakumtaja kwa jina kigogo aliyemtuhumu. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa alimlenga Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Luhanjo ndiye aliyemwandikia barua katibu mkuu wa wizara ya Mambo ya Ndani, akimtaka kuwasilisha taarifa ya mchakato wa zabuni katika kikao cha Baraza la Mawaziri.

Hii ilikuwa baada ya Masha kuingilia mchakato wa mradi kinyume cha taratibu kwa madai kuwa mmoja wa wazabuni alikuwa na madai kuwa hakutendewa haki, huku Bodi ya Zabuni ikiwa haijatoa taarifa rasmi.

Bila shaka Masha alikuwa akitafuta kujinasua kwenye tuhuma kuwa yeye ni chanzo cha ucheleweshaji mradi wa vitambulisho.

Mapema mwaka huu, Masha alituhumiwa kukutana na mmoja wa wazabuni, kupata maelezo juu ya malalamiko yake na kukutana na wakuu wa kampuni iliyoingia zabuni ya Uswisi, Geneva.

Ilidaiwa na kuchapishwa katika vyombo vya habari kwamba Masha aliingilia mchakato wa zabuni huku bodi ya zabuni ikiwa tayari imefikia hatua ya kuchuja waombaji.

Masha alidaiwa pia kutaka "kubeba kampuni yake ya Sagem Securite" ya Uswisi.

Tuhuma zilikuwa kwamba alikwenda kinyume cha sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi serikalini (PPRA) ya mwaka 2004 na kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 na Kanuni 101 (6).

Hata hatua yake ya kumwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akilalamikia uamuzi wa Kamati ya Zabuni ya wizara yake, ulichukuliwa kuwa kinyume na sheria na kulinganishwa na kutoa siri za serikali na kutumia ofisi ya umma kwa maslahi binafsi.

Katika mchakato wa vitambulisho vya taifa wa mwaka 1998, Masha akiwa wakili kutoka kampuni ya IMMMA Advocates, aliwakilisha moja ya makampuni yaliyoshiriki katika zabuni ya vitambulisho na kuingia katika mgogoro. Mteja wa Masha aliishinda serikali.

Taarifa zinasema tayari Baraza la Mawaziri limeagiza kusimamishwa kwa mchakato wa kutafuta mzabuni. Zinasema serikali imechukua uamuzi huo bila kujulisha makampuni yaliyokuwa yanashiriki katika kuwania zabuni.

Hiki ndicho chanzo au kichocheo cha mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA) kutaka kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusiana na suala hilo.

Lakini badala ya Masha kujadili mchakato wa zabuni wa mwaka 1998 au ule unaoendelea, juzi bungeni alijitumbukiza katika mchakato wa mwaka 1968 na kudai wakati huo alikuwa bado hajazaliwa.

Akiwasilisha bajeti ya makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2009/2010, bungeni Jumatano iliyopita, Masha alisema, "sipaswi kulaumiwa kwa kuwa mchakato wa mradi ulipokuwa unaanza, nilikuwa hata sijazaliwa."

Alisema anashangaa kuona anatuhumiwa kuingilia mchakato wa zabuni kwa hatua tu ya yeye, mwenye dhamana, kuuliza hatua za mchakato kwa katibu mkuu wa wizara yake.

Hatua ya Masha ya kuhusisha "kigogo" wa ikulu imeeleweka kama njia ya kujikinga tuhuma katika sakata kubwa la vitambulisho vya kitaifa, ili wabunge wamwonee huruma wakati wa kupitisha bajeti ya wizara yake.

Kigogo wa ikulu ambaye ametajwa kuwa Luhanjo na waziri Masha, wote ni wateule wa Rais Kikwete. Bali tofauti na Masha, Kikwete anatambua uwezo wa Luhanjo na mchango wake kwa taifa kwa muda mrefu sasa.

Ni Kikwete aliyemteuwa Luhanjo kuwa katibu mkuu kiongozi, ambaye Masha anadaiwa kupingana na uamuzi wake katika mradi huu.

Hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu ikulu inasema nini juu ya tuhuma za Masha, labda hii ni kutokana na kutotaja jina la anayemtuhumu.

Bali hatua ya kutuhumu mtendaji mkuu serikalini bungeni, wakati yeye mwenyewe yumo ndani ya serikali hiyohiyo, inaonyesha mapungufu makubwa katika mawasiliano serikalini.

Aidha, ni hatua inayoonyesha ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja na kukosekana kwa maadili ya uongozi.

Mpaka hapa sharti serikali ianze kutafuta njia ya kujinasua kutokana na aibu na kujinusuru isishitakiwe na kulazimika kulipa mabilioni ya shilingi; fedha za umma, kwa makampuni ambayo tayari yameingia katika mchakato.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: