Waziri Masha kaumbuka


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrance Mash

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha, anadaiwa kusema uongo katika pingamizi lake kwa mgombea wa CHADEMA katika jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza.

MwanaHALISI limepata nyaraka zinazoonyesha kuwa wakati Masha anaweka pingamizi, hakuwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha madai yake.

Kile ambacho Masha anadai kuwa kielelezo, kimeonekana kuwa kilipatikana siku moja baada ya kuweka pingamizi iliyosababisha Ezekia Dibogo Wenje wa CHADEMA kuenguliwa.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizo mikononi mwa MwanaHALISI, Masha aliweka pingamizi tarehe 20 Agosti mwaka huu akidai Wenje siyo raia wa Tanzania.
Alidai pia kuwa Wenje alidanganya katika maelezo yake kuhusu wadhifa wake katika kampuni alikoajiriwa.

Pingamizi la Masha linadai kwamba kampuni anayofanyia kazi Wenje ya Nation Media Group (NMG) inasema kuwa mgombea wa CHADEMA ana wadhifa wa Sales Manager (Meneja Mauzo) na siyo Country Manager kama alivyoandika kwenye maelezo yake ya ugombea.

Hata hivyo, MwanaHALISI limebaini kwamba barua ya kuthibitisha maelezo ya Masha kwenye pingamizi kuhusu wadhifa, iliandikwa siku moja baada ya kuwasilisha pingamizi.

Barua ambayo Masha anadai imetoka NMG na anaikariri katika pingamizi lake, iliandikwa tarehe 21 Agosti mwaka huu, lakini madai ya Masha yalitolewa jana yake.

Masha aliandika kwa Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Nyamagana, Bw. M.W. Kabwe, kuwa mgombea wa CHADEMA “…amesema uongo…na uongo huo umethibitishwa na barua ya kampuni hiyo ya 20 Agosti 2010.”

Lakini hakuna barua yoyote iliyotoka NMG ambayo iliandikwa tarehe 20 Agosti. Barua ya NMG ni ya tarehe 21 inayokwenda moja kwa moja kwa waziri wa mambo ya ndani na siyo msimamizi wa uchaguzi.

Wadadisi wanasema, kwa kadri ya matukio, barua ilikuwa imepangwa kupatikana siku ya mwisho ya kuweka pingamizi; lakini ama mwandishi wa barua hakujulishwa suala la tarehe au alifanya hivyo kwa makusudi ili kujiondoa katika mgogoro uliokuwa umeanza kufukuta.

Barua yenyewe inayodaiwa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited; kampuni tanzu ya NMG, Bw. Sam Shollei, haina kumbukumbu.

Shollei anaandika katika barua yake kuwa Wenje ni Sales Manager na siyo Country Manager.

Shollei anajibu barua ya Kaimu Katibu Myeka wa Masha, Bw. Nelson Kaminyoge aliyetaka kujua nafasi ya Wenje katika NMG.

Barua ya Shollei ipo kwenye karatasi za ofisi zinazoonyesha kuwa inatoka NMG lakini Shollei anasaini kama Mkurugenzi Mtendaji.

Mkanganyiko uliopo ni kwamba Shollei ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, wakati Mkurugenzi Mtendaji wa NMG ni Bw. Linus Gitahu, raia wa Kenya anayefanyia kazi makao makuu, Nairobi.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye na ambazo zilikuwa hazijathibitishwa, zilisema Tume ya Uchaguzi imeamua kumrejesha Wenje ulingoni.

Katika maelezo yake kupinga pingamizi, Wenje alikuwa amedai kuwa Shollei hana mamlaka ya kuwa msemaji wa NMG kwa vile yeye ni mkurugenzi wa Mwananchi ambayo ni kampuni tanzi chini ya NMG.

“Shollei aliyeandika barua hiyo si mkurugenzi wa NMG bali ni wa Mwananchi Communications ambazo ni kampuni mbili tofauti. Hana nguvu ya kisheria ya kuzungumzia mambo ya kampuni nyingine ambayo ina msemaji wake,” anasema Wenje katika maelezo yake ya 21 Agosti 2010.

Akizungumza na gazeti hili juzi jioni, Shollei alikiri kwamba ni kweli aliandika barua kwa serikali katika “siku iliyoandikwa kwenye barua” na kwamba ana mamlaka ya kufanya hivyo.

Alipoulizwa na MwanaHALISI iwapo Masha, akiwa mgombea ubunge wa Nyamagana au Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye aliyeshinikiza yeye aandike barua hiyo, Shollei alipata kigugumizi.

“Ngoja nikwambie kitu. Serikali ilitutaka kutoa maelezo kuhusu nafasi ya Wenje kwenye kampuni yetu. Mimi kama mkuu wa kampuni nikatoa maelezo yetu,” ameeleza Shollei.

Kuhusu uraia wa Wenje, Shollei alisema kwa kadri ajuavyo yeye, mgombea huyo wa CHADEMA ni raia wa Tanzania na alipewa kazi akijulikana kuwa ni Mtanzania.

NMG ni kampuni inayomilikiwa na Aga Khan, kiongozi wa dini; na ina vyombo mbalimbali vya habari katika nchi za Afrika, ikiwemo kampuni tanzu ya Mwananchi.

Kwa upande wao, viongozi wa kata ya Mkoma, wilayani Rorya, mkoani Mara anakotoka Wenje, wamethibitisha uraia wa Wenje.

Katika barua waliyomwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyamagana, ya tarehe 23 Agosti mwaka huu, wamesema Wenje ni raia aliyezaliwa tarehe 2 Oktoba 1978.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: