Waziri Mkuu sasa anapindisha mambo


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

HAPO zamani, zamani za mwaka 2008 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda alionekana mtu mnyoofu sana tena mpole na muungwana.

Na alipoweka msisistizo katika kilimo, kampeni iliyobatizwa jina la Kilimo Kwanza, Pinda akapewa jina la Mtoto wa Mkulima. Ukweli enzi hizo ni kabla ya kukabiliwa na majaribu ya uongozi na utawala.

Majaribu yalipozidi Mtoto wa Mkulima akajitokeza katika sura halisi ya kiongozi wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba hatofautiani na viongozi wengine wa chama hicho kinachokabiliwa na matatizo na  tuhuma za magamba, rushwa, ufisadi na hata umangimeza.

Katika muda mfupi, Waziri Mkuu Pinda amepindisha mambo mengi kuliko hata hao waliomtangulia. Baadhi ya mambo ambayo amepindisha ni kama yafuatayo.

Kwanza Pinda alipindisha mambo alipotembelea Kanda ya Ziwa. Akionekana kuguswa na mateso yaliyokuwa wanapata albino kwa kuuawa au kukatwa viungo, bila kujali sheria wala kufikishwa mahakamani, alimuru watuhumiwa wa mauaji ya maalbino.

Hatua ya waziri, tena ambaye kitaaluma ni mwanasheria kuamuru mauaji ya watuhumiwa haikuweza kueleweka hata kama alionekana kusikitishwa na vitendo viovu wanavyofanyiwa raia wengine eti kwa sababu tu ni maalbino na hivyo kuwa “dili.”

Kauli yake hii ya kutaka watuhumiwa wa mauaji ya albino wauawe ilisababisha Pinda amwage machozi bungeni pale alipohojiwa uhalali wake kisheria na kikatiba na mbunge wa Wawi – Pemba, Hamad Rashid Mohammed, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo cha kila Alhamisi.

Pinda pia alipindisha mambo pale  alipofanya ziara mkoani Mara na kuagiza eti wananchi wa huko wayatumie mabaraza ya jadi kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi, wizi wa mifugo na mapigano ya koo mbalimbali mkoani humo!

Waziri Mkuu, Pinda aliguswa na hali ya mkoa wa Mara unaokumbwa na mapigano ya koo mara kwa mara kama vile Wanchari na Wakira, Wanchari na Walenchoka, Wanyabasi na Wairegi, Wahunyaga na Wasweta; katika miaka ya 1980 na 1990 walipigana Wanyamongo na Wairegi, Wanyamongo na Wanyabasi, Wangoreme na Watimbaru wa Mugumu na Wakira na Wanyabasi.

Mapigano haya husababishwa na migogoro ya ardhi na wizi wa mifugo. Hata hivyo, ulikuwa upindishaji wa sheria kwa Waziri Mkuu, Pinda kuelekeza migogoro hii itatuliwe kijadi kwa kutumia wazee wa jadi maarufu kama abagaka baekimira au abagaka bainchama.

Aina hii ya utatuzi wa migogoro haifai kwa vile wanaoumia si lazima wawe wale waliosababisha ugomvi. Hawa wazee wakitoa adhabu si lazima mlipaji faini awe yule aliyekutwa na kosa; akishindwa basi hulazimisha alipiwe na ndugu yake yeyote kama baba, mama, kaka, dada au mdogo wake.

Pia wazee hawa hutoza faini kubwa mno isiyolingana na kosa lililotendwa na hivyo kuendeleza migogoro. Mfano kutokuhudhuria mkutano mtu anapigwa faini ya ng’ombe mmoja! Wizi wa kuku au mbuzi mtu anapigwa faini ng’ombe watatu au wanne na hata watano.

Uzoefu umeonyesha kwamba faini ya ng’ombe hao watano ikilipwa, ng’ombe mmoja hupewa polisi, ng’ombe mwingine hupewa ofisi ya mkuu wa wilaya na mwingine hupelekwa mkoani kwa Kamanda wa Polisi Mkoa na Mkuu wa Mkoa.

Faini hizi zilianza kulipwa enzi ya awamu ya kwanza ya Julius Nyerere ambaye ndiye alitoa amri hiyo kuwa wezi walipe faini ya ng’ombe na kwamba wezi wa mifugo wakipitisha ng’ombe wa wizi katika kijiji “A” bila kuzuiwa basi wakazi wote wa kijiji “A” kilichoshindwa kuwazuia wanapigwa faini ya ng’ombe kumi kila mmoja na hoja kuwa wewe ulikuwa Dar es Salaam, Mwanza au Arusha haikubaliki.

Tungependa hapa kuihoji serikali ya CCM chini  ya Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Pinda kuwa ng’ombe wote waliotolewa kama faini tangu miaka ya 1960, 1970, 1980, 1990 na hata 2000 walikwenda wapi? Au kama waliuzwa mauzo yake sasa yamefikia shilingi ngapi?

Leo Pinda anapindisha mambo anataka kurudisha enzi za ujima, ambazo kesi huamuliwa na wazee hawa ambao huonea watu na faini kugawiwa wakubwa wilayani Tarime, Musoma, Bunda na Mugumu? Na wakubwa hawa wakionjeshwa rushwa/faini hizo hata ungelalamika unalia, hata ungedhikiri uchi husikilizwi! Nani anataka upuuzi huu tena katika karne ya 21?

Waziri Mkuu Pinda akapindisha mambo tena alipokubali kuhudhuria vikao vilivyoitishwa na yule Katibu Mkuu maarufu wa Wizara ya Nishati na Madini David Jairo na kupokea posho lukuki. Magazeti yaliripoti kuwa jina la Pinda lilionekana miongoni mwa waliopokea posho naye hajakanusha hili.

Pinda alipindisha mambo alipokataa kumsimamisha kazi rafiki yake Jairo eti kwa sababu yeye kama Waziri Mkuu si mamlaka iliyomteua Jairo kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini!

Lakini leo hii baada ya kibano cha mgomo wa madaktari Pinda yule yule aliyegoma kumsimamisha kazi Jairo, ametoa maelekezo kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga wa Wizara Mtasiwa wasimamishwe kazi!

Sasa watawaliwa tunajiuliza, Pinda leo kapata wapi upinde wa kuwatungua mganga wa wizara na katibu mkuu wakati awali alisema bungeni kuwa mamlaka iliyoteua ndiyo inayohusika kusimamisha na si vinginevyo?

Hili la posho yaonekana limemnogea mno Waziri Mkuu Pinda. Siku chache zilizopita Pinda alipindisha maneno tena alipodai eti ofisi ya Rais imebariki posho za wabunge jambo ambalo halikuwa kweli maana kesho yake ikulu ilikanusha habari hizo.

Pamoja na kauli ya Pinda kukanushwa na kurugenzi ya mawasiliano Ikulu si Pinda wala mtu yeyote kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu aliyejitokeza hadharani kueleza habari za Rais kubariki posho za wabunge zilianzia wapi!

Lakini Pinda hajakoma bado. Angalia alivyoshughulikia mgomo wa madaktari. Hakuna hata kimoja kilichokwenda sawa baada ya Pinda kupindisha mambo na kufokea watu wazima waliokwenda shule na kuwatisha kama watoto wadogo.

Matokeo yake madaktari wakagoma zaidi si kutibu tu wagonjwa, bali pia kuhudhuria vikao vyao pale hoteli ya Starlight. Waziri Mkuu Pinda kashindwa kutambua kwamba mtu mzima, tena msomi na mtaalamu wa mambo hatishiwi nyau.

Kutokana na yote haya mie nasema Pinda kazidi kupindisha mambo ang’oke. Ajiuzulu tu taratibu asingizie kuwa anaumwa au kwamba anakabiliwa na matatizo ya kifamilia basi aondoke, tumechoshwa na namna Pinda anavyopindisha mambo.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: