Waziri Mwinyi ajiandae kujiuzulu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version
Gumzo
WAZIRI wa Ulinzi, Dk. Hussein  Mwinyi

WAZIRI wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi ameahidi kujiuzulu iwapo itagundulika kuwa milipuko ya mabomu, kwenye ghala la silaha katika kambi ya jeshi, Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam ilitokana na uzembe.

Haijulikani waziri amepata wapi ujasiri wa kiwango hicho. Baadhi ya wachunguzi wanasema huenda, kwa muda mrefu sasa, amekuwa akitafuta njia ya kujiuzulu.

Kwani kauli ya waziri haina kinga. Hata kama tume inayochunguza, ambayo ni ya jeshi, itawasilisha matokeo ya uchunguzi kwa mkuu wa majeshi, ambaye atawasilisha ripoti yake kwa amiri jeshi mkuu ambaye ni rais, bado kuna uzembe usioweza kufichika.

Kwa tume ya jeshi au kwa rais kutoona uzembe haitakuwa na maana kwamba hakukuwa na uzembe. Kufanya ionekane hakukuwa na uzembe, kutakuwa na shabaha ya kumdhalilisha rais na kutukana Watanzania ili Mwinyi aendelee kuwa waziri kinyume na ahadi yake.

Tena bora kwenye tume kungekuwa na mwandishi wa habari, kwani hakuna siri tena. Kama ni kujua kuwa kambi ya Mbagala ni ghala la silaha na silaha za aina gani, tayari imefahamika kwa wakazi wa Mbagala, taifa na dunia nzima.

Bali uzembe wa kumg’oa Mwinyi siyo lazima uwe wake pake yake; ni hata uzembe wa maofisa wake wizarani na uzembe wa makamanda. Siyo lazima uwe uzembe kuhusu ghala la Mbagala peke yake, bali hata maghala mengine ambako mabomu na silaha nyingine zaweza kulipuka wakati wowote.

Kwanza, kuna uzembe unaotokana na kuendelea kuweka ghala la silaha karibu na makazi ya wananchi. Hata kama jeshi lilitangulia kuwa pale, kuruhusu wananchi wajenge uwani mwa jeshi; au jeshi lichimbie silaha uwani mwa nyumba za raia, ni uzembe usiosameheka.

Kwamba silaha ziliwekwa hapo kama hatua ya haraka ya kuzihifadhi kwa kazi ya dharura, hauwezi kuwa utetezi wa kuhalalisha uzembe wa muda mrefu. Kwamba hakuna aliyejua kuwa siku moja mabomu hayo yangeweza kulipuka, ni uzembe ulioota ndevu.

Na kwamba waziri hakujua kuwa hayo yangetendeka; na kwamba tume inayochunguza itamkinga na kusema kwamba hahusiki au hakujua; na kwamba rais ataridhika na utetezi huo, ni mambo yasiyotarajiwa.

Matokeo ya uzembe huu ni vifo vya watu 26 hadi sasa, kuteketezwa na kuharibiwa kwa nyumba na makazi ya raia na kufanya baadhi yao kuishi maisha ya ukimbizi jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, baadhi ya kambi za jeshi hazina mpaka wa umbali rasmi na makazi ya raia – nchi nzima. Chukua mfano wa kambi ya Lugalo na kitongoji cha Kawe. Unatoka ndani ya nyumba ya raia unaingia kambini – ni palepale.

Bila kujali kwamba wamekuwepo mawaziri wengi wa ulinzi kabla ya Mwinyi, uko wapi ushahidi kwamba tangu aingie ameona hilo, amechukua hatua na sasa aweza kujipiga kifua kuwa kama ni uzembe atajiuzulu? Uko wapi?

Pili, hakuna ushahidi kuonyesha kuwa waziri anajua idadi ya mabomu yaliyoko chini ya ardhi pale Mbagala. Ripoti za vyombo vya habari zimesema wataalam hawajui kuna kiasi gani cha mabomu; na kauli hizo hazijakanushwa na waziri wala wataalam wenyewe wa mabomu jeshini.

Hili linazua maswali mengi. Ina maana hata waziri wa ulinzi hajui silaha zake na idadi yake? Yawezekana hata walinzi wa silaha hawajui wanalinda silaha kiasi gani na za aina gani?

Tatu, kauli za wahusika kwamba hawajui lini mabomu yote Mbagala yatalipuka au kulipuliwa; na kwamba wanahitaji msaada wa satelaiti kujua kilichomo ndani na kilivyokaa, ni ushahidi tosha kwamba kuna uzembe wa aina ya pekee ambao hauwezi kumwacha Mwinyi kitini.

Upo uwezekano wa kuthibitika kuwa mabomu katika maghala yote nchini hayajageuzwa hata siku moja; hayajapangwa upya wala kuangaliwa umri wake tangu kuisha kwa vita vya ukombozi kusini mwa Afrika au vita vilivyomwangusha Idi Amin wa Uganda.

Inawezekana waziri Mwinyi hakujua kuwa kwa ahadi ya kujiuzulu alikuwa anajitia kitanzi hata kwa yale ambayo watangulizi wake walizembea, walidharau, walipuuzia, walikataa tu kufanya. Atasalimikaje?

Nne, mlipuko wa mabomu waweza kusababishwa na mambo mengi. Wataalam wanataja mitetemeko ya ardhini inayoweza kuleta msuguano ambao unaweza kuyawasha na hivyo kulipuka.

Waziri ataonyesha nini, na baadhi ya askari wanasema hana, hatua aliyochukua kuzuia msuguano na hatimaye mlipuko wa mabomu? Kama kutochukua hatua ni uzembe na wahusika hawakuchukua hatua, waziri anapata wapi ujasiri wa kujiapiza?

Tano, kuna maelezo ya kitaalam kwamba mabomu hupaswa kukingwa ipasavyo kutokana na radi. Hili linahitaji ufafanuzi mpana.

Inakadiriwa kuwa nguvu ya umeme katika mwale (myai) wa radi inaweza kufikia mwanga wa volti 200 milioni. Fasihi juu ya radi inaonyesha kuwa mwale hutokea kati ya mara 50 na 150 kila sekunde duniani au mara 3 bilioni kwa mwaka kwenye uso wa dunia.

Mwale huu huonekana kwa muda unaokadiriwa kuwa moja ya milioni ya sekunde (1/1,000,000) na wataalam wanasema siyo lazima radi isikike; kuna radi zisizosikika lakini zenye athari kwa vilivyoko kwenye uso wa dunia na chini ya ardhi.

Lakini hewa katika mpasuko wa radi imekadiriwa kuwa na joto la farenhaiti 54,000 au sentigredi 300,000. Hili si joto la kawaida. Ni zaidi ya mara sita ya joto kwenye uso wa jua.

Kwa hiyo mpenyo wa joto hili, katika vitu vyote ambavyo ni vyepesi kuathiriwa na joto kali, huweza kufura kwa joto na kuungua au kulipuka.

Kwa mfano, nchini Marekani inakadiriwa kuwa nguvu ya umeme wa radi iliyotokea mara 15,000, imesababisha kutokea kwa moto na kuunguza zaidi ya eka 2 milioni za misitu katika Alaska na Magharibi mwa nchi hiyo katika kipindi cha miaka 10.

Kuna wanaohusisha radi, hata ziswizosikika, na kulipuka kwa mabomu ya Mbagala. Waziri analijua hilo? Yawezekana wataalam wa mabomu na wale wa radi (hali ya hewa) hawajapata wazo la kuunganisha mlipuko na radi.

Tuchukulie kuwa wameanza utafiti. Je, ghala la silaha la Mbagala lilikuwa limekingwa na “vimeza radi?”

Mara nyingi na katika nchi nyingi, maghala ya silaha hukingwa na mitego ya radi (Thunder arresters). Fasihi ya ulinzi huu inaeleza kuwa hujengwa kichanja karibu mita tatu au nne kutoka kwa kile kinachokingwa. Kichanja hicho huwa na mfumo wa umeme na waya za kuzima nguvu ya radi.

Aidha, mfumo huo waweza kujengwa moja kwa moja katika kuta za nyumba au hata andaki ambamo kuna vifaa vinavyokingwa, kama mabomu. Kwa hiyo nguvu za radi ambazo zingechaji fataki au mabomu na hivyo kulipuka, hunaswa kabla ya madhara.

Je, maghala ya silaha za jeshi nchini yana vinasa radi? Kuna taarifa kuwa kinasa radi kimoja kinagharimu Sh. 30 milioni. Madai kwamba askari waliishaomba kiasi hicho mara nne wakiambiwa “hakuna fedha” yana ukweli gani?

Katika mazingira haya, kubainika kwa ukweli kuhusu radi kuchaji mabomu ardhini na kutokuwepo vinasa radi, kunaweza kuwa uzembe wa aina yake; wa kuogofya na ambao waziri hastahili kusubiri utangazwe redioni.

Kampuni ya Saberta ya China ni maarufu duniani kwa kutengeneza mitego ya radi na nchi nyingi huagiza mitego hiyo rasmi kwa shughuli za kulinda maeneo nyeti kama maghala ya silaha na vifaa vingine muhimu. Bila shaka wizara ya ulinzi inajua hilo.

Sita, kwa kipindi chote tangu 29 Aprili, mabomu yalipolipuka yamejitokeza mambo ambayo pia yanachangia uzembe wa awali.

Wizara haijachukua hatua kuwafundisha wakazi wa Mbagala jinsi ya kukabiliana na milipuko ya mabomu. Kwa mfano, wafanye nini wanaposikia mlipuko?

Kuna wanaokaa wameziba masikio ili wasisikie milipuko, kumbe hiyo ni harati zaidi kwa masikio; badala ya kuyaacha wazi na kuhakikisha wanaweka midomo wazi ili kuzuia kiwambo (ear-drum) cha sikio kisipasuke.

Askari wakifyatua mzinga huwa wanalala chini usawa wa kiuno. Wananchi wafanyeje? Nani awape elimu hii? Wakati huu ambapo mabomu yanalipuka, bado bila mpangilio, wananchi wafanye nini? Wizara ya Mwinyi haijafunza; na waziri anayeahidi kujiuzulu ndiye anahusika.

Saba, isipokuwa kwa siku chache tu baada ya siku ya kwanza ya mlipuko, wizara ya ulinzi imejivua jukumu la kutoa maelezo kuhusu mwenendo wa ulipuaji mabomu yaliyosalia na yasiyojulikana idadi.

Kazi hii ameachiwa mwanasiasa William Lukuvi.

Ukweli ni kwamba Lukuvi, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam hana utaalam wa mabomu na mara nyingi amesema yale ambayo siyo na hata kugonganisha wananchi. Amebebeshwa mzigo usio wake. Wizara husika imekimbia jukumu lake; na huu ni uzembe unaopaswa kumgharimu Mwinyi.

Yawezekana waziri Hussein Mwinyi alikuwa anafanya utani kuhusu suala la uzembe au hakuelewa upana wa uzembe katika utekelezaji.

Haihitajiki kuwa na orodha ndefu ya matukio ili kuthibitisha uzembe. Tukio moja tu linatosha kumwondoa Mwinyi ofisini. Je, kwa orodha hapo juu, Mwinyi anachagua lipi limsindikize au anasubiri kauli ya rais?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: