Waziri Ngeleja kufukuzwa?


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja na katibu mkuu wa wizara hiyo, David Jairo wamekalia kuti kavu, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu wa karibu na ikulu, Rais Jakaya Kikwete atalazimika kumuondoa Ngeleja katika nafasi yake ya sasa ili kulinda hadhi ya serikali yake mbele ya wananchi na jumuiya ya kimataifa.

“Nakuambia lazima rais (Rais Jakaya Kikwete) atamuondoa Ngeleja ili kurejesha hadhi ya serikali yake. Huyu bwana tokea ameteuliwa amekuwa mtu wa porojo badala ya vitendo…“Ameshindwa kukaa na wasaidi wake, kuleta bungeni mpango wa muda mfupi wa kukabiliana na tatizo hili. Badala yake amekwenda bungeni na miradi kibao” anaeleza mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya CCM kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Anasema, “Ngeleja ameenda bungeni na miradi ya mwaka 2013 na 2015, huku kila mradi ukiwa umetengewa fedha zake. Busara ya kawaida, serikali ingeenda na mpango wa muda mfupi wa kutatua tatizo hili,” ameeleza.

Waziri Ngeleja anakabiliwa na “mashitaka” ya kushindwa kutatua tatizo sugu la uhaba wa umeme nchini kwa kushindwa kuwasilisha bungeni “mpango mkakati wa muda mfupi wa kukabiliana na uhaba wa umeme na kunyamazia ufisadi unaofanywa na watendaji wake.

Naye Jairo anakabiliwa na kibarua kigumu kubaki katika nafasi yake baada ya kutuhumiwa kutumia jina la ikulu kujinufaisha binafsi, kuchota kutoka taasisi zilizoko chini ya wizara yake zaidi ya Sh. 1 bilioni kinyume na kutenda kinyume cha taratibu.

Tayari Rais Kikwete ameripotiwa kuandika barua ya kumfuta kazi Jairo.

Aliyekiweka kibarua cha Ngeleja na Jairo katika wakati mgumu, ni mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo.

Shelukindo alisema Jairo ameandika kuagiza kila taasisi ichangie mchakato wa bajeti. Kila taasisi ilitakiwa kuchangia Sh. 50 milioni ambazo iliagizwa kupelekwa kwenye akaunti ya kitengo cha madini iliyopo benki ya NMB.

Akichangia bajeti ya wizara hiyo juzi, Shelukindo alisema hawezi kuunga mkono bajeti ya Ngeleja kwa kuwa haikuja na mpango wa kuondoa uhaba wa umeme na imejaa ufisadi.

Akihutubia Bunge mjini Dodoma Jumatatu iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema, “Nilitaka kuchukua hatua zaidi, lakini nikashauriwa siwezi kufanya hivyo kwa kuwa liko nje ya uwezo wangu.”

Alisema, “Ningekuwa na uwezo, ningechukua hatua hapahapa. Lakini kwa kuwa makatibu wakuu wanateuliwa na rais, nitamjulisha jambo hili haraka ili aweze kuchukua hatua kwa kuwa mchakato wa kuchangisha fedha ulitawaliwa na giza.”

Mbali na hayo, gazeti hili limepata nyaraka zinazoonyesha Jairo alitaka kubeba kampuni isiyo na sifa ya kuzalisha umeme, Artimus Group Inc.

Katika barua yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo 26 Julai 2010, Jairo anatetea kampuni hiyo kwa kusema serikali ilikosa dola 28 milioni (sawa na Sh 40.32 bilioni) kwa ajili ya kuendesha mradi huo chini ya mfumo wa ORET kutokana na kucheweshwa na EWURA.

Anatuhumu Mamlaka la Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuwa imeshindwa kusaidia kukamilika kwa mradi wa uendelezaji gesi asili ya Mnazi Bay iliyopo katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Katika barua yake yenye kumbukumbu Na. SAB.88/270/01/11/24 iliyonakiriwa kwa Paniel Lyimo, katibu mkuu - ofisi ya waziri mkuu; Christopher Sayi, katibu mkuu-wizara ya maji na umwagiliaji; Prosper Mbena, katibu wa rais (Ikulu), Jairo anasema, “Kwa miaka kadhaa serikali ilipokea mapendekezo kutoka kampuni kampuni ya Artimus Group Inc na baadaye mwaka 2004 ikafunga mkataba wa mgawanyo wa mapato kati yake, Artimus na TPDC.

Hata hivyo, Jairo akieleza kwa njia ya kushitaki, anasema Masebu aliendelea kukaidi maagizo ya mabosi wake na kuelezea waziwazi kuwa, “Ni bora serikali ikose msaada huo kwa kuwa yeye yupo kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.” Katika kuhakikisha “mradi wake unafanikiwa,” Jairo amepeleka mapendekezo mawili serikalini. Kwanza, anasema “Haruna Masebu kama kiongozi mkuu wa EWURA awajibike ipasavyo kwa sababu amekaidi kutekeleza maelekezo ya mamlaka za juu na pili ameikosesha msaada na kuiingiza serikali hasara ya dola za Marekani 28 milioni.”

Pendekezo jingine ambalo Jairo ametaka serikali itekeleze ni kutaka wizara yake iwe na taasisi yake “yenye ya kusimamia udhibiti wa maendeleo ya nishati-Energy Sector Regulatory Authority. Hivyo inapendekezwa sheria iliyoanzisha EWURA irejewe ili kutengenisha usimamizi wake.”

Kisheria, EWURA ipo chini ya wizara ya maji na umwagiliaji, ambayo kwa sasa iko chini ya Profesa Mark Mwandosya.

Barua ya Jairo ilijibiwa kwa nguvu na Injinia Mbogo Futakamba, aliyekuwa kaimu katibu mkuu.

Hata hivyo, MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kuwa tayari serikali imekiri kwamba ilikuwa njiani kuingizwa mkenge iwapo Masebu angeruhusu utoaji wa leseni kwa Artimus Group Inc.

Akiandika kujibu Jairo, kwa barua yenye Kumb. Na CAB. 48/139/01b/25, 6 Agosti 2010, kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, Futakamba anasema baada ya kufuatilia mvutano wa EWURA na wizara ya Nishati na Madini, ameona Masebu angepewa nafasi ya kujitetea huku akipendekeza mamlaka hiyo kuwa na uhuru badala ya kuburuzwa na Jairo.

Ili kuepuka mvutano, Futakamba anasema, haoni sababu ya kumshitaki Masebu na badala yake anashauri kwamba wizara husika zingekaa chini na kutafakari hali hiyo ili kuboresha ushirikiano kikazi.

Anasema mfumo wa udhibiti uliopo umefanya kazi nzuri sana tangu mwaka 2006, na kwamba changamoto zilizopo katika mifumo ya gesi asilia zinaeleweka. Anasema waziri wa maji haoni sababu kwa sasa ya kumfungulia mashitaka Masebu.

0
Your rating: None Average: 4 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: