Waziri wa Fedha anzia Bima


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

MWANAMUME mmoja alifumania mkewe. Akamuua kwa kumpiga risasi, akimwacha mwanamume aliyekuwa na mkewe aende zake.

Alipoulizwa baadaye, kwanini asimpige risasi yule mwanamume, alijibu kwa ukakamavu, “bila kumuua mke wangu, ningelazimika kuua wanaume wengine kila baada ya muda.”

Sababu ya kukumbuka kisa hiki ni taarifa iliyonukuliwa kwenye vyombo vya habari Jumatano tarehe 27 Juni 2012.

Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy (CCM), aliitaka serikali kunyonga watumishi waliofilisi Shirika la Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Akizungumza kwa uchungu, mbunge huyo alipendekeza watumishi wa umma wanaokutwa na hatia ya kufilisi mashirika ya umma, wanyongwe, wafe, wazikwe na makaburi yao ndio yafungwe pingu.

Mbunge huyu amekwenda mbali. Kuua ni kuua tu – awe ameua mtu binafsi au serikali kwa amri ya mahakama. Kutoa uhai wa mtu ni kuvunja haki za binadamu, bila kujali nani ameua.

Wakati haifai kukubaliana na wazo la kuua, ni muhimu kupokea uchungu alionao mbunge, ambao umemsukuma katika kutamka hukumu katili.

Hakuna ubishi juu ya kilichofanywa na watumishi waliokabidhiwa mashirika haya ili kuyasimamia kwa niaba ya Watanzania.

Waasisi wa mashirika haya ya umma walifanya kazi kubwa ya kuyajenga na kuyaimarisha.

Chukua mfano huu. Muasisi wa Bima (NIC), Gibbons Mwaikambo (marehemu), alikabidhiwa shirika hili mwaka 1972 likiwa na mtaji wa Sh. 5.5 milioni tu. Lakini mpaka anaondoka mwaka 1989 aliliacha likiwa na vitegauchumi vya zaidi ya Sh. 31 bilioni.

Waliochukua nafasi yake siyo tu walishindwa kuendeleza mafanikio hayo, bali pia walijigeuza “mchwa” kwa kulitafuna wanavyotaka hadi likateketea.

Kama Mwaikambo akifufuka leo, hakika atazimia ghafla au atakufa tena haraka kutokana na mshituko atakaoupata.

Mwaikambo alilenga shirika linufaishe wateja wake, kwa kulipa madai yao ya bima za maisha, ambazo huchukua muda mrefu kulipwa.

Badala yake, wakwapuaji wameuza vitegauchumi na fedha zimeliwa utafikiri hazina mwenyewe.

Kwa mfano, viongozi wa Bima wasingeweza kulifilisi shirika kama wasingepata ushirikiano imara wa bodi ya wakurugenzi na uongozi wa wizara ya fedha, wasimamizi wakuu wa shirika.

Kinachoshangaza ni kuona wizara hii ikisaidia kulidhoofisha kama vile si kati ya watoto zake.

Hivi kwanini hatua zinazostahili zisichukuliwe kwa mujibu wa sheria? Kigugumizi kinatoka wapi? Hivi tukiamini “wakubwa zaidi” nao wanahusika na uporaji katika shirika, tumekosea?

Bahati nzuri watafuna shirika wote wapo. Wanajulikana kwa majina na sura. Hata wafanyakazi wa Bima wanawajua walipo. Wanawajua wanafanya nini kwa sasa.

Serikali inatakiwa ichukue hatua. Iwakamate na kuwahoji ili waeleze wapi walipata mali walizonazo. Sisi tunafahamu walikochota – Bima.

Wakati shirika wamelikondesha, wao wanazidi kunenepa. Ni watu wanaopaswa kupelekwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo. Ushahidi wa waliyofanya upo.

Kutokana na waovu kuachiwa wafanye ubadhirifu watakavyo, hata waliochukua nafasi zao nao wameendeleza ubadhirifu. Wanaona waliotangulia hawakuguswa.

Pamoja na ukweli kwamba hatua ya kuwashitaki waliotafuna Bima, itasaidia kutisha mafisadi watarajiwa, pia serikali inaweza kuepusha mashirika kufilisiwa na kujijengea heshima na uaminifu kwa wananchi.

Karibu asilimia 50 ya wanaodaiwa kufilisi shirika la Bima, ni wafanyakazi wa idara ya uhasibu.

Uchunguzi mdogo ukifanywa kwa baadhi ya wafanyakazi na wakongwe wa idara hii, utagundua mali walizonazo hazilingani hata kidogo na mishahara yao.

Inafahamika kuwa baadhi ya viongozi walioondolewa Bima, walitumia mbinu za kughushi; wakitengeneza madai hewa, kulipa wateja hewa, na wakatengeneza kesi hewa.

Viongozi waliandaa madai hewa makao makuu na mikoani. Wakaanza kulipana. Kwa watu wenye uelewa wa shughuli za bima, wanajua haya madai ni hewa.

Wafanyakazi waliosimamishwa kazi lakini wakabaki wanalipwa nusu mshahara kwa zaidi ya miaka kumi, walikataliwa kulipwa.

Wale waliofunguliwa kesi feki lakini wakashinda, nao walikataliwa kulipwa.

Uongozi wa Bima unajua sheria inawataka walipe wafanyakazi walioshinda kesi; na waliokuwa wamesimamishwa walipwe nusu mshahara iliyobaki. Hawafanyi hivyo.

Uzoefu wa utawala mbovu ni kwamba wafanyakazi waliokuwa wamesimamishwa kazi au walioshinda kesi, wanaambiwa “nendeni mahakamani.”

Wafanyakazi wakienda mahakamani, uongozi unatafuta mawakili wa kuendesha kesi hizo kwa miaka kadhaa – mrija wa kukinga mapato haramu.

Kuna kugawana ada ya kuendesha kesi. Hii ada usifikiri ni kiduchu. Ni mamilioni ya shilingi; huku mfanyakazi akilia na kusaga meno. Wala kesi haziendi. Bali viongozi wanakula na kunenepeana!

Hivi ndivyo mambo yamekuwa katika mashirika mengi na hata Bima. Nenda Posta; nenda TTCL. Kote ni rahisi kutengeneza pesa kwa njia hiyo.

Serikali ijifunze na itumie vyombo vyake kupata watu waadilifu bila kuangalia sura za wenzao na wasio wenzao.

Serikali iwaondoe watendaji wote waliokuwa kwenye uongozi uliofilisi mashirika ya umma. Nafasi zao zitangazwe, na watu waombe ili watu wenye sifa na dhamira njema, waingie kuongoza.

Serikali inapaswa kuziba mianya ya kesi hewa. Ni vizuri kabla shirika halijapeleka kesi mahakamani, mwanasheria mkuu wa serikali ajiridhishe kuwa kesi husika ina manufaa kwa nchi siyo kwa waovu.

Ni bora ikaweka sheria, kwamba ofisa mkuu yeyote wa shirika akifungua kesi na akashindwa, kwa uzembe tu, awajibike kulipa gharama zote yeye binafsi, hata ikibidi mali zake zifilisiwe.

Sasa, Bima wamepata mkurugenzi mkuu mpya, J.P. Mwandu. Huyu aliwahi kuwa mkurugenzi katika kampuni ya Tudor Insurance Corporation Limited.

Kampuni hii iliibuka kwa kasi mwishoni mwa miaka ya 1990. Ilikusanya fedha nyingi na baadaye mkurugenzi mtendaji wake akakimbia na fedha za wateja.

Wakati kampuni ikifilisika, Mwandu alikuwa mmoja wa wakurugenzi. Sasa ni Mwandu aliyepewa jukumu la kusimamia fedha za umma – Bima. Bahati ya mtende! Nini kitarajiwe chini ya uongozi wake?

Huyu atadhibiti au atalinda wizi? Atakomesha malipo hewa kwa watu hewa? Je, ataondoa kesi hewa ambamo mamilioni ya shilingi yamepotelea? Au atapanda daladala lilelile la kuvuna migongoni mwa wateja?

Kuna taarifa kuwa Sh. 13.8 bilioni zimepatikana Bima kwa kuuza baadhi ya majengo yake. Je, yatatokea madai feki, wateja feki na kesi feki ili zitafunwe na wachache?

Yapo maeneo mengi kwa Waziri mpya wa fedha, Dk. William Mgimwa kuyashughulikia, lakini Bima angeanza sasa, ila kama anadhamira ya kulinda mali za wateja na mali za umma.

Mwandishi ni msomaji wa MwanaHALISI.
0
No votes yet