Wazo la Karume kuongoza tena halina tija


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Rais Amani Abeid Karume

SAID Soud Said awaeza kuwa mwanasiasa mwenye akili nyingi. Lakini naona sasa anakuwa "mwanasiasa hatari."

Anapendekeza kwenye majadiliano ya wadau mbalimbali wa maendeleo ya Zanzibar kwamba serikali ya umoja wa kitaifa iundwe haraka Zanzibar. Ni sawa.

Bali serikali anayoipendekeza anataka iongozwe na Rais Amani Abeid Karume, huyu rais ambaye kikatiba, ifikapo 31 Oktoba 2010, urais wake unakoma.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka utaratibu wa muda wa utumishi wa rais wa Zanzibar. Kwamba atakaa kwa kipindi cha miaka mitano na iwapo atachaguliwa tena ataongoza kwa miaka mitano mingine na kulazimika kustaafu.

Soud anataka katiba ibadilishwe ili kumwezesha Rais Karume kuendelea kuongoza baada ya Oktoba mwakani; na kwamba yeye ndio awe kiongozi wa serikali hiyo ya umoja.

Nini mantiki ya wazo la Soud? Kwanza anataka rais Karume aendelee kuongoza baada ya ukomo wake kikatiba. Kwa kuwa hiyo haiwezekani, la pili sasa, anataka katiba ibadilishwe ili imwezeshe kuendelea kuongoza baada ya hapo.

Maana yake nini? Ni kwamba Wazanzibari waondokane na utaratibu wa siku zote tangu walipotunga katiba yao hiyo, wa kuchagua rais kila baada ya miaka mitano. Pili, anataka katiba ibadilishwe kwa ajili ya mtu mmoja tu. Huyu anaitwa Amani Abeid Karume.

Tofauti yangu kubwa naye ipo hapa. Soud ananishtua anapokuwa na mawazo leo kwamba inawezekana kutokea mtu mmoja akawa na akili nyingi na maarifa zaidi kuliko Wazanzibari wengine hivyo tubadilishe katiba ili tumfurahishe na tumtunuku urais.

Kwa mtazamo wake anaamini Rais Karume anastahili kupewa nafasi hiyo adimu kwa kuwa ameongoza nchi vizuri na imepata maendeleo makubwa ambayo hajapata kuyaona katika umri wake wa miaka karibu 60 anayopita.

Hili haliwezekani. Kwanza muhimu Soud afahamu urais si zawadi. Si huo wa Zanzibar wala popote duniani. Sijapata kusikia ipo nchi inatumia utaratibu wa kutoa zawadi ya urais kwa raia wake.

Soud atambue kwamba mawazo yake hayakuzingatia umuhimu wa kuendeleza utaratibu wa kubadilishana madaraka kati ya mtu na mtu uliojengwa na katiba yetu.

Katiba haiwezi kubadilishwa kwa minajil ya kumwezesha mtu mmoja fulani aongoze kipindi zaidi ya kile kilichokubaliwa na kubainisha katika Katiba.

Lakini pia sidhani kama ni busara kwa wakati tulionao Wazanzibari kwa hiari yao wakaja na makubaliano ya kumruhusu mtu fulani, wala si Amani Abeid Karume tu, apewe nafasi ya kuongoza baada ya kukamilisha kipindi cha miaka 10 ya kuwa kiongozi wa nchi.

Utaratibu wa kubadilishana madaraka baada ya kiongozi kukamilisha kipindi chake cha kikatiba unapaswa kuendelea tena ulindwe sana. Ndio utaratibu mzuri.

Hivi leo, kutokana na utendaji usiofaa unaoonekana kwa miongoni mwa wabunge nchini – wakiwemo wale wanaosononeka kusikia mtu anaazimia kugombea ubunge uchaguzi ujao – wamejenga mwenendo wa kufanya wanamiliki majimbo kama mali yao, kumekuwa na mawazo kwamba vizuri iwepo sheria inayoweka ukomo wa mtu kuwa mbunge kama ilivyo kwa urais.

Mtu akishaongoza kwa muda mrefu usio na ukomo anajisahau na matokeo yake huweza kufanya ndivyo sivyo. Anatenda kwa kiburi na jeuri. Anadharau anaowaongoza. Anaibia wananchi hao.

Wazanzibari wanahitaji mabadiliko ya aina yoyote lakini ambayo yanakwenda kwa mujibu wa utaratibu wa kikatiba. Kwa sasa, uchaguzi tu ndio utaratibu unaokubalika.

Inatakiwa rais akishatimiza miaka mitano apimwe tena akitaka ridhaa ya kuongoza tena. Atapimwa kwa kuingia katika kinyang’anyiro na watu wengine wa vyama mbali na alicho yeye, ili aombe tena ridhaa.

Rais Karume aliomba ridhaa mwaka 2000 akatangazwa mshindi. Akaongoza kwa miaka mitano. Alipotaka tena kuongoza, ukafanyika uchaguzi Oktoba 2005 naye akaomba tena ridhaa. Akatangazwa mshindi. Hapo ndo mwisho!

Akitaka kuongoza tena baada ya Oktoba 31 itakuwa anatafuta udikteta. Itakuwa anataka kubadilishwa kwa utaratibu uliojengwa na Katiba. Itakuwa anataka kuwa mfalme wa Zanzibar.

Karume itakuwa anataka kuvuruga hata yale machache aliyoyafanya katika kipindi cha miaka 10 aliyoongoza. Urais si kazi ya maskhara. Urais ni majukumu. Kutumikia urais ni jukumu zito kuliko kupanda mlima wa Kilimanjaro. Uongozi wa nchi tofauti na kwenda sokoni.

Kutumikia urais kunahitaji sifa na mtu awe na dhamira ya kuongoza watu si kuwa komedi kwamba mtu anafanya uigizaji. Urais si kazi ya maigizo jamani. Unataka mtu anayesikia na kusikiliza. Tena asikilize hata asiowapenda na wale anaoamini wakati wa uchaguzi hawakumchagua.

Urais ni imani ya kweli, uadilifu na wito. Wadhifa wa urais haupaswi kushikwa na mtu aliyedhamiria kubahatisha. Hapana. Atende kweli na kwa kuzingatia kuwa binadamu wote ni sawa.

Urais ni kazi inayohitaji mtu makini na ambaye ana nia ya kustawisha jamii; kujenga nchi na kuijengea uhusiano mwema na nchi nyingine, akianzia na jirani zake na zile zilizojenga uhusiano mwema siku nyingi.

Lakini rais anatakiwa kutofikiria kujitajirisha Ikulu. Zaidi anatakiwa kuwa mtulivu na muwajibikaji kwa anaowaongoza; wale alioapa kuwatumikia kwa usawa pasina ubaguzi wa aina yoyote.

Katika zama tulizopo, ni kiburi tu kinachoweza kumsukuma mtu akajitia kujiamini na kutaka kuongoza nchi kwa zaidi ya kipindi kilichobainishwa katika katiba.

Huu ni wakati wa uwazi. Wakati wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, katika uzalishaji na upashanaji habari. Tupo katika zama za kuimarisha demokrasia pale ilipoanza na kuijenga pale ilipominywa.

Kufuata katiba ni moja ya misingi ya kulea demokrasia. Zanzibar inahitaji kupumua ili istawi kama zinavyostawi nchi nyingine. Ustawi wa nchi unafanikiwa kwa vigezo siyo kwa uongozi wa tambo na chusha.

Rais Karume ameongoza kwa mazonge. Amekumbana na mitihani mingi. Najua hana utulivu wa moyo wala akili sasa. Anajiuliza anapofikia kukamilisha muda wake Oktoba mwakani, ameiachia nini nchi yake? Amewaachia nini Wazanzibari?

Ndio maana baada ya kutabiri atakavyokuwa katika maisha ya kustaafu, amebadilika na amelenga kuandika historia. Hataki kuja kuishi kwa manung’uniko. Atakufa kihoro. Itamtesa historia ya utumishi wake.

Sasa anataka kurekebisha mambo. Anataka kuiacha nchi mahali pazuri ili atakayekuja kuongoza asipate shida. Karume ameazimia kufanya kisichofanywa na waliomtangulia: Kuongoza uchaguzi huru na wa haki kwelikweli.

Kumuendeleza akalie kiti Ikulu baada ya Oktoba kwa namna yoyote ile ni kujaribu kuendekeza ujinga. Ujinga ni kule mtu kutenda jambo licha ya kujua halitamnufaisha kwa lolote, pengine kubwa ni kumdhuru.

Sitaki kuamini kuwa Karume anaweza kumkubalia mtu kama Said Soud Said na wahafidhina walio katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) eti aongoze zaidi baada ya kubadilishwa katiba.

Ha, aendelee kuongoza ili iwe nini? Ingawa kila mtu ana haki ya kutoa maoni aonavyo, matokeo ya wazo la Soud hayatakuwa na tija yoyote.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: