Wenje, Masha, Nyamagana hapatoshi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Lawrence Masha, mgombea wa CCM jimbo la Nyamagana

EZEKIA Dibongo Wenje (32) amerejeshwa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Nyamagana, mkoani Mwanza. Anagombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wenje amerejea katika kinyang’anyiro hicho baada ya kushinda rufaa yake aliyoiwasilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupinga kuenguliwa kugombea nafasi hiyo kulikofanywa na Wilson Kabwe, msimamizi wa uchaguzi jimbo la Nyamagana.

Kabwe alimuengua Wenje kutoka katika kinyang’anyiro hicho baada ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lawrance Masha kudai kuwa “Wenje si raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, pamoja na mambo mengine, Wenje amesema, ikiwa atachaguliwa kuingia bungeni, kipaumbele chake cha kwanza kitajikita katika mambo matatu.

Kwanza, anasema amepanga kushughulikia suala la upanuzi wa huduma za afya. Anasema wananchi wa Nyamagana wana matatizo makubwa ya afya, na kwamba Masha ameshindwa kulishughulikia kimamilifu suala hilo.

“Angalia hospitali au zahanati zetu. Nyingi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa na madkatari. Nyingine hazina hata vitanda vya wagonjwa. Masha analifahamu hili, lakini katika kipindi chote cha miaka mitano ya ubunge wake, ameshindwa kulitatua tatizo hili,” anasema.

Pili, Wenje anasema atasimamia sekta ya elimu kwa kuhakikisha kila kata inakuwa na shule bora ya msingi na sekondari na ambayo inatoa elimu bora.

Jambo jingine ambalo mgombea ubunge huyo wa CHADEMA anasema amepanga kushughukia katika kipindi chake cha kwanza cha ubunge, ni utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Anasema kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT) ya mwaka 2009, jiji la Mwanza ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi duniani, lakini ukuaji huo haujaendana na upatikanaji wa huduma za jamii.

Kuna matatizo ya ugawaji mbovu wa maeneo, jambo ambalo analosema lisipotatuliwa linaweza kuleta madhata makubwa huko tuendako.

Anasema watendaji wa manispaa wamefikia hatua ya kuuza kiwanja kimoja kwa watu watatu na wote wanakuwa na hati sahihi.

“Hili limetokea kwa wengi na ni lazima nilishughulikie mara nitakapoingia bungeni,” anasema.

Anamtuhumu mpinzani wake kwa kushindwa kukutanisha wananchi wa Nyamagana; kusikiliza shida zao na kibaya zaidi ametumia ubunge wake kuwagawa wananchi katika makundi ya masikini na matajiri kwa kushindwa kusimamia ugawaji wa ardhi, jambo ambalo limewafanya masikini kushindwa kumikiki ardhi.

Akiongea kwa kujiamini, Wenje anasema Masha hajui kuwa akina mama wajawazito wa Nyamagana wanapata taabu gani wanapokwenda kujifungua na kwamba hafahamu wanatunza vipi watoto wanaojifungua.

“Hawezi kujua haya, kwa sababu Masha ana kula kuku Dar es Salaam. Hawezi kuyajua haya kwa sababu, Masha anajiona si sehemu ya matatizo ya wananchi,” anasema.

“Haya ndiyo nitakayoyasimamia katika kipindi cha mwaka mmoja wa kwanza wa ubunge wangu,” anaeleza Wenje.

Alipoulizwa atawezaje kuyashughulikia matatizo yote hayo katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, Wenje amesema, “Huhitaji mabilioni ya shilingi kufanya haya.”

Anasema kinachohitajika ni dhamira na utashi wa kisiasa. Kwa mfano, Wenje anasema, “Haya mambo ya watu kukosa dawa na huduma katika zahanati ni mambo yanayosababishwa na vitendo vya rushwa. Ukishadhibiti hilo, kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa,” anafafanua.

Anasema ripoti za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikiitaja Mwanza kuwa miongoni mwa halmashauri zinazoongoza kwa ufisadi nchini na akasema hilo ni tatizo ambalo linahitaji kutatuliwa.

“Pale zinapohitajika fedha, wananchi watachangia. Mwanza imejaliwa kuwa na watu wengi wenye uwezo na wanachohitaji hawa watu ni kukutanishwa na kuombwa kusaidia,” amesema.

Akizungumzia kilichomsibu, Wenje anamtuhumu Masha kwa kutumia madaraka yake ya uwaziri kwa maslahi yake binafsi.

Anasema, “Masha ametumia madaraka yake kwa maslahi binafsi. Huyu ndiye waziri wa mambo ya ndani ya nchi; ndiye mwenye mamlaka ya kusema nani si raia na nani ni raia.”

Kilichomkuta, anasema ndicho kinawakuta Watanzania wengi, bali kilichomsaidia kupata haki yake ni uelewa wake juu ya mambo ya sheria na ujasiri wa chama chake katika kupigania haki.

Hata hivyo, Wenje anasema, “Nawashukuru wote walionipigania,” bali anamtuhumu Kabwe kwa upendeleo kwa mgombea wa CCM.

Anasema imani yake hiyo ya kuibuka na ushindi inatokana na wananchi wa Nyamagana kuipokea vizuri CHADEMA na upinzani kwa ujumla.

Nyamagana ni eneo la mjini ambalo wananchi wake wanajikita katika kuangalia mambo makubwa, anasema.

“Matatizo ya Nyamagana wanayaona. Wao wanajua kwamba Wenje atawafanyia makubwa na Masha amekwisha kushindwa kazi,” anasema.

Pamoja na kwamba Wenje anasema hana kinyongo, lakini anasema ameandika barua NEC akimuomba mkurugenzi wa uchaguzi, Rajabu Kiravu kumuondoa Kabwe katika usimamizi wa uchaguzi.

“Huyu bwana hawezi kusimamia haki. Tayari ameonyesha kwa vitendo kuwa anatumika kwa maslahi ya CCM,” anaeleza kwa sauti ya kosononeka.

Anamtuhumu Kabwe kunyofoa baadhi ya nyaraka zake alizowasilisha kujibu pigamizi la Masha, ili ionekane kuwa hakuwasilisha ushahidi dhidi ya madai ya Masha.

Anasikitikia pia kitendo cha Kabwe kumnyima fomu Na. 12 ambayo ni mahususi kwa ajili ya kukata rufaa. Ilimbidi kusafiri hadi Dar es Salaam kutafuta haki yake hiyo.

Amesema kauli mbiu yake kubwa katika uchaguzi wa mwaka huu ni “Nchi Kwanza” inayomaanisha kutanguliza maslahi ya nchi, akiwaomba pia wana-CCM kumpa kura.

“Ukiumwa na kwenda hospitalini, haitakusaidia kitu kama utakuwa umevaa fulana za CCM, CUF au CHADEMA,” anasema.

Anasema, katika kushugulikia maendeleo hakuna mambo ya vyama. “Nawaomba wananchi wa Nyamagana, bila ya kujali itikadi zao, waungane kunichagua niwawakilishe bungeni,”anasema.

Wenje mwenye elimu ya chuo kikuu katika ualimu na usimamizi wa biashara, ana mke na ana watoto wawili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: