Wenye dini ndio wauzaji mihadarati


Fred Okoth's picture

Na Fred Okoth - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version

DINI zinapaswa kufanya kazi ya kufinyanga mioyo safi ili wanadamu watende mema ya kumpendeza Mungu. Katika hili watumishi wa Mungu wanapaswa kuonesha njia.

Maovu yanayofanyika duniani – uzinzi, wizi, mauaji na uchafuzi wa hekalu la Muungu unaofanywa kwa nguvu hata na watumishi wa Mungu – ni dhahiri ama dini au watumishi wameshindwa wajibu huo.

Kitendo cha watumishi wa Mungu kushiriki moja kwa moja au kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya ili wanadamu wasiumbiwe mioyo safi ni ushahidi kwamba waliopewa jukumu la kuongoza kondoo wa Mungu wamegeuka chui.

Ushahidi wa ushiriki wa watumishi wa Mungu katika biashara hiyo haramu umepatikana wazi ila tofauti na hatua kali zinazochukuliwa kwingineko duniani, hapa watuhumiwa wanapigiwa magoti kana kwamba kitendo wanachofanya kina baraka za Mwenyezi Mungu.

Mawaziri na wabunge wameoneshwa watuhumiwa lakini majina yao ni siri; vyombo vya dola vinawajua wapotoshaji hawa wa kondoo wa Mungu, lakini wanadai wanawafuatilia. Hadi lini?

Rais Jakaya Kikwete amesema kuna shehe alikamatwa na mchungaji mmoja wa kanisa lililoko Biafra kwamba anaisaidia polisi. Halafu akasema vijana wake (maofisa usalama) wanamweleza kuwa mashehe na wachungaji si waaminifu.

Anasema pia kuwa vijana wake wamemwambia wapo waliokiri kosa na kwamba hawatajishughulisha tena. Kwa kauli hiyo ina maana hawa wamekwepa mkono wa sheria, na kinachowafanya wakwepe mkono wa sheria ni kwa vile eti wao ni watumishi wa Mungu. Upindishaji huu wa sheria umetokea pia Uingereza.

Gwiji wa mchezo huu wa dawa za kulevya Curtis Warren anaweza akaachiwa huru eti kwa sababu askari waliomkamata walipata taarifa na uthibitisho wa kumnasa kwa njia isiyo halali kisheria.

Hapo ndipo nasema unafiki wa sheria na watawala wanaotunga sheria hizi, eti sheria hiyo hiyo inatumika kulinda uozo unaoteketeza jamii.

Askari saba wa kituo cha polisi cha New Jersey nao wapo hatarini kuburuzwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupata taarifa za gwiji la dawa za kulevya Warren kwa njia zisizokubalika mbele ya sheria. Maafande hao wanashitakiwa kwa kuweka kifaa maalum cha kunasa taarifa katika gari la kukodi na hapo ndipo waliweza kupata nyendo za gwiji huyo wa biashara chafu ya kuuza dawa za kulevya.

Warren, ambaye pia anajulikana kwa jina la ‘Cocky’ mwenye utajiri ya paundi milioni themanini, anaweza akaruhusiwa kutoka jela aliko kutokana na ulanguzi wa bangi yenye thamani ya paundi milioni moja endapo hawa maafande watapatikana na hatia.

Askari hao inadaiwa walikaidi msimamo wa washirika wa Warren kuzuia uwekaji chombo hicho cha kunasa taarifa katika gari hilo lilipokuwa likisafiri kupitia nchi za  Ufaransa, Ubelgiji na Uholanzi.

Majaji wa mahakama kuu walisema taarifa walizozipata makachero hawa zilipatikana katika njia isiyo halali ingawa Warren mwenye umri wa miaka 48 alinyimwa dhamana. Lakini majaji wanasema kama askari watapatikana na hatia, kumfunga Warren itakuwa  jambo la hatari sana.

Hicho ndicho kinatumiwa pia Tanzania kwamba ni hatari kuwatia ndani watumishi wa Mungu ambao uchunguzi umebainisha pasi na shaka wanaangamiza kondoo wa Mungu.

Labda serikali ya Tanzania inataka kusubiri mpaka Rais wa Marekani, Barack Obama apige marufuku au atangaze hadharani majina ya watumishi wa Mungu waliopotea ndipo ikurupuke na kushughulikia suala hilo.

Kule Nairobi, Kenya serikali ilikaa kimya hadi Obama alipotangaza majina ya viongozi kwamba wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Mmoja wa waliotajwa na Obama ni Mbunge wa Kilome, Harun Mwau.

Wanaharakati wa Kenya walimtaja Mwau pamoja na Ali Hassan Joho (Kisauni), William Kabogo (Juja),  Gidion ‘Sonko’ Mbuvi (Makadara) na mfanyabiashara maarufu wa Mombasa Ali Punjani ambao wapo chini ya upelelezi kwa kashfa ya kusafirisha mihadarati.

Wanaharakati hao walitoa angalizo kwamba kama hawa wafanyabiashara ya dawa za kulevya hawatakamatwa na kutiwa ndani kuna uwezekano wanaweza kuingiza nchi katika vurugu kama zile za mwaka wa 2008 fikapo 2012 katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Wakiongea chini ya mwavuli wa shirika lisilo la serikali liitwalo Chama cha Kijamii cha Kitaifa (National Civil Society Congress) katika hoteli ya kitalii ya Serena- Nairobi, wanaharakati hao waliweka angalizo kwamba kuna uwezekano mkubwa fedha zinazotokana na dawa za kulevya huenda zikatumika katika uchaguzi mkuu wa Kenya mwakani.

Mtumishi wa Mungu Timothy Njoya aliomba serikali ya Kenya iwakamate wote wanotuhumiwa kuhusika na biashara hiyo haramu.

“Magwiji wa biashara za dawa za kulevya lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa sababu fedha za dawa za kulevya zinapitishwa kwa njia za kijanja na zitatumika kufadhili uchaguzi ujao,” mtumishi huyo wa Mungu alisema.

Kusuasua kwa serikali kukamata wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini ambao vyombo vyote vya dola vinawajua ni dalili kwamba fedha chafu imeshaingia na inazuia haki kutendeka. Maana mtu hapaswi kuachwa kwa vile ni maarufu bali iwe kwa vile hana hatia. Leo serikali inasema kuna watumishi wa Mungu wamekiri kosa lakini ‘hakuna’ sheria ya kutumia kuwaadhibu. Maana yake nini?

Kule Columbia, moja ya nchi zinazotetemeshwa na magwiji wa dawa za kulevya mambo ni yale yale.  Aliyekuwa kiongozi wa kundi moja hatari liitwalo Cali drug cartel, Gilberto Rodríguez Orejuela wiki kadhaa zilizopita alitoka jela usiku baada ya mahakama kuamuru kuachiliwa kwake mapema baada ya muda wa kifungo chake.

Orejuela aliondoka jela saa nne usiku chini ya ulinzi mkali wa askari wa kawaida na jeshi ili kuzuia vurugu za aina yoyote kutoka kwa wananchi wenye hasira. 

Rais Alvaro Uribe, aliyeingia madarakani akiahidi kwa nguvu kusambaratisha makundi yanayosafirisha dawa za kulevya, alijaribu kuzuia Gilberto Rodríguez Orejuela asitolewe jela lakini alishindwa. Huko ndiko Tanzania inakoelekea.

0784 778053
0
No votes yet