Wenye vituo vya mafuta ni wafadhili CCM, hawaguswi


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MWISHONI mwa wiki iliyopita, nilipata bahati ya kukaa kijiweni kunywa kahawa jirani na nyumbani kwangu Tungi, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Hapo kijiweni, mjadala ulihusu wafanyabiashara ya mafuta nchini kukaidi amri ya serikali kuuza mafuta kwa bei iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Mjadala ulikuwa mkali. Wazungumzaji wengi waliishangaa serikali kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wa vituo hivyo waliokaidi amri ya mamlaka halali iliyowekwa kwa sheria, kusimamia biashara ya maji na nishati nchini – Ewura.

Kulingana na maoni yaliyotolewa kijiweni, wanaopaswa kulaumiwa kwa mabaya yote, kashfa zote na matatizo yote yanayowakabili Watanzania ni viongozi wa CCM, serikali ya CCM na wafadhili wa CCM. Kufikia hapo, sikuwa na la ziada bali kutafakari niliyoyasikia.

Nikajaribu kuwatofautisha viongozi wa CCM na viongozi wa serikali ya CCM. Nikagundua kwamba hakuna tofauti kati ya viongozi hawa kuanzia kwa mwenyekiti wa CCM taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri.

Wajumbe wa halmashauri kuu na kamati kuu ya CCM ndio mawaziri, wenyeviti wa bodi za mashirika na wakurugenzi wa makampuni mbalimbali.

Nikatafakari hao wafadhili wa CCM ni akina nani. Nikagundua kuwa ni wamiliki wa viwanda na makampuni makubwa nchini na ambao wengi wao wanakabiliwa na kila aina ya tuhuma kuanzia za kifisadi mpaka zile shutuma za wizi wa waziwazi.

Nikabaki nimeduwaa. Pale pale nikawa nimepata jibu kwa nini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaweza kupata jeuri ya kuivimbia serikali bila hata chembe ya aibu. Jibu ni kwamba wamiliki wa vituo vya mafuta ndio viongozi wa CCM, serikali ya CCM na wafadhili wa CCM. Wamwogope nani?

Kwamba bei ya mafuta ya taa iliyoongezeka, ilipanda siku ileile ya kutolewa tamko lakini bei ya petroli na dizeli iliyopungua haikushuka hata baada ya mwezi kwa madai mafuta ya zamani yaliyonunuliwa kwa bei mbaya yalikuwa yangalipo. Mbona bei ya mafuta ya taa yaliyonunuliwa kwa bei nafuu hawakusubiri yaishe kwanza kabla ya kupandisha?

Nikalazimika sasa kuangalia watuhumiwa wa ufisadi mmoja mmoja. Nikamwona mtu aitwaye Fida Hussein. Huyu aliwahi kuwapa zawadi za pick up double cabin (aliwafadhili) Umoja wa Vijana CCM Songea miaka ya 1990. Nilishiriki kuandika habari ile jinsi vijana wa UV-CCM walivyocheza lizombe na mganda kufurahia gari.

Mwezi mmoja baadaye Fida Hussein alikamatwa na meno ya tembo, ngiri, kiboko na pembe za faru vikiwa vimefichwa kwenye matenki ya mafuta ya petroli vikisafirishwa kutoka Tunduru, Ruvuma kwenda Dar es Salaam.

Toba! Kumbe misaada ya wafadhili ni baada ya kuliibia taifa nyara na rasilimali nyinginezo!

Nikazidi kutafakari nikamwona mtu aitwaye Tanir Sumaia. Huyu aliwahi kushirikiana na mtu aitwaye Vithlani, yule kuwadi maarufu wa rushwa ya rada ambayo wanasheria wakubwa kabisa wa Tanzania wanasema hakuna ushahidi wa kumfungulia mtu mashtaka.

Baada ya kugundulika rushwa ya rada Somaia akatangaza kujitoa kwenye umiliki wa kampuni iliyofanya biashara ya rada na kuiingiza serikali mkenge. Baada ya habari ya kujitoa kutangazwa siku chache baadaye Somaia akawapa UV-CCM fedha taslimu Sh. 400 milioni.

Nikatafakari tena nikaona mgogoro wa Barrick na wananchi kule Nyamongo, Tarime ambako mkuu wa wilaya John Henjewele aliwazuia viongozi wa vijiji na wananchi kuongea na mgodi juu ya tatizo lolote kama yeye hayupo! Mkuu wa wilaya ana maslahi gani kwenye mgodi unaoua raia? Haijulikani ila tunajua yeye ni kada na kiongozi wa CCM.

Nikatafakari tena nikamwona Mwenyekiti mstaafu wa CCM Taifa, Ben Mkapa na waziri wake, Dan Yona na watoto wao na wake zao na marafiki zao wakihusika katika kashfa ya ubinafsishaji wa mgodi wa Kiwira ambao ilithibitika walijiuzia kwa bei sawa na bure.

Tena basi nimeambiwa eti kampuni yao moja ilipangishwa kwenye jengo la ikulu na ikaandikwa kwenye anuani ya kampuni hiyo pale BRELA kuwa ni ikulu na hawakuwahi kulipia kodi ya pango kwa muda wote waliopofanyia biashara zao binafsi kwenye jengo lile la umma. Ataulizwa nani? Labda si mwenzetu huyo!

Nikatafakari tena nikauona mgogoro uliozua kashfa ya Richmond na Dowans ambao uliwagubika makada wa CCM, Edward Lowassa, Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi. Lowassa alilazimika kujiuzulu na akapewa hadhi ya waziri mkuu mstaafu na kulipwa marupurupu kibao. Nani atawajibika kama wahalifu wanaheshimiwa?

Nikatafakari tena nikamwona kada mmoja wa CCM huko Kigoma aitwaye Farijala Maranda alivyohusika katika kashfa ya wizi wa fedha za EPA Benki Kuu ya Tanzania. Huyu kwa vile, hakuwa kigogo ndani ya CCM kafungwa lakini wazito walioiba pesa nyingi wao ushahidi haujapatikana!

Nikatafakari tena nikaona mgogoro wa UDA, nikagundua kuwa wamiliki wa kampuni ya Simeoni iliyonunua UDA ni Waziri mstaafu na mbunge wa CCM pamoja na mtoto wa kigogo, kwa maelezo ya gazeti la Mwananchi.

Hawakutaja jina la mtoto wala kigogo mwenyewe lakini nimenong’onezwa kuwa anaitwa Ree. Nimeambiwa waziri huyo yuko NEC ya CCM na babake Ree yuko NEC hiyo hiyo.

Nikazidi kutafakari tena nikamwona Rostam Aziz.  Huyu kathibitika kuwa gamba (fisadi) CCM. Nikakumbuka makala moja iliyowahi kuandikwa na rafiki yangu Salva Rweyemamu akimsifia na hata kutaja dini yake ambayo sikuwahi kuisikia tangu kuzaliwa. Huyu alikuwa mfadhili na kiongozi wa CCM.

Wengine hatuwataji kwa maana tumezuiwa na mahakama, lakini walifaidika na kashfa za Kagoda na mali nyinginezo za mashirika ya hifadhi ya jamii nchini. Hawa hawakuwahi hata kuchunguzwa wala kuhojiwa licha ya wenyewe kutangaza magazetini kuwa wanawafahamu na wana uhusiano na wamiliki wa Kagoda!

Kama viongozi wa CCM, serikali ya CCM na wafadhili wa CCM ndio wamiliki wa vituo vya mafuta nchini, ndiyo maana serikali inashindwa kuwagusa wanapokaidi amri halali ya mamlaka halali iliyowekwa kisheria.

Wamiliki hawa wamewapa watawala na viongozi wa chama tawala hisa kwenye makampuni yao ya mafuta ndiyo maana watawala wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya wenye vituo maana ni sawa na kuchukulia kituo chako cha mafuta hatua za kisheria. Hakuna anayefanya hivyo.

Baada ya tafakuri hii nimeamini maneno ya kijiweni kuwa wahalifu wengi kama si wote, mafisadi wengi kama si wote, wezi wengi kama si wote na wabadhirifu wengi  wa mali ya umma kama si wote ni viongozi wa CCM, serikali ya CCM na wafaddhili wa CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: