Werema, Kombani mnasimamia lipi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

NINAPOWATAZAMA walokole wawe wa Kikristo au Kiislam ninathubutu kuwafananisha na viongozi wawili katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Hawa ni Waziri wa Sheria na Katiba, Selina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema. Ulokole huu ni ule wa kihafidhina!

Hawa ni viongozi walioteuliwa na rais kumsaidia katika eneo la sheria. Mwanasheria mkuu wa serikali akiwa na jukumu kuu moja, kumshauri wakati wote rais na serikali katika kuzingatia na kufuata sheria.

Ni kiongozi muhimu kiasi kwamba kabla hata rais aliyeshida uchaguzi hajaanza kutekeleza majukumu yake kama vile kuteua mawaziri na hata waziri mkuu, mtu wa kwanza kuteuliwa ni mwanasheria mkuu wa serikali.

Waziri wa sheria naye ni muhimu. Ndiye  mwenye wajibu wa kusimamia sekta ya sheria na katiba; ana wajibu mkubwa wa kisiasa kuona kwamba katika eneo hilo serikali na taifa kwa ujumla haliyumbi katika kuendesha mambo yake kwa mujibu wa sheria.

Wakati wote anapaswa kumshauri rais juu ya hilo. Ni kiongozi ambaye kimantiki angepaswa kuwa jicho la rais kisiasa kwa kutazama ni mahitaji yapi ya kisheria ya yanahitajika kwa wananchi na ni kwa njia gani bora zaidi yanaweza kufikiwa kwa ustawi mwema wa jamii na taifa kwa ujumla wake.

Kwa bahati mbaya Kombani na Werema badala ya kuwa nguzo katika maeneo yao, wameamua kuwa wahafidhina wa kisiasa. Badala ya kutazama mahitaji ya taifa ya sasa kisheria na kikatiba, wameamua kuzamisha vichwa wao katika ukale na ukongwe wa kukataa mabadiliko.

Hawa ni viongozi ambao walikosa kabisa ama ujasiri wa fikra au walikuwa wepesi mno kifikra kiasi cha kushindwa kutambua kuwa taifa lilikuwa limeingia katika zama mpya za mabadiliko.

Walishindwa kuona upepo wa mabadiliko ya katiba ulikuwa unavuma kwa nguvu na yeyote ambaye angepingana nao, hakika angeishia kupeperushwa.

Viongozi hawa kwa nyakati tofauti bila hata kutafakari kwa kina maana ya mabadiliko ya katiba na haja ya taifa kupata katiba mpya inayoendeana na miaka 50 ya uhuru ifikapo 9 Desemba 2010, waliibuka na kauli na tata wakipinga katiba mpya.

Walipinga si kwa sababu walikuwa na hoja nzito yenye mantiki, ila kwa kuwa tu wanasumbuliwa na uhafidhina, ukale na ukongwe wa fikra ambazo kutu yake iliyokolea inashindwa kuakisi mahitaji ya sasa na huko tuendako kama taifa.

Katika mazingira mapya ya kisiasa ya sasa baada ya Rais Kikwete kutamka wazi kwamba anakubaliana na mawazo ya kuandikwa upya kwa katiba ya jamhuri na akiwa amekwisha kuamua kuwa ataunda tume ya kuratibu mchakato wa kupatikana kwa katiba hiyo, Kombani na Werema wanabaki wapi?

Je, bado wameshikilia ukale na uhafidhina wao au wamebadilika? Na kama wamebadika wana ujumbe gani basi kwa Watanzania juu ya matamshi yao?

Je, wakati wanazungumza hayo, walikuwa wakimwakilisha rais au walikuwa wanazungumzia hisia zao?

Mwanahabari na  mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii, Ndimara Tegambwage, alipata kumfananisha Kombani na mtu aliyeibuliwa tu kusikojulikana na kukabidhiwa wadhifa ambao pengine hakujua thamani na maana yake.

Ndimara alitoa uchambuzi huo mara tu baada ya Kombani kusema hajui hicho wanasiasa wa upinzani wanachozungumza kuhusu katiba mpya.

Alikwenda mbali zaidi akidai eti hajapokea mapendekezo yoyote juu ya katiba mpya, lakini kwa maono yake (duni) aliamini katiba ya sasa inakidhi kila kitu, hahiitaji marekebisho.

Kwa kauli kama hii, hakika Kombani alikuwa ni mtu anayeelea hewani, haijui jamii anayoizungumzia, hakutaka kujishughulisha kujua hicho wanachodai  wananchi kuhusu katiba mpya ni nini na kwa nini madai hayo yaibuke sasa?

Kiongozi kama huyu ndiye anatarajiwa eti awe kamisaa wa kisiasa katika sekta ya sheria na katiba.

Kamisaa asiyejua ukamisaa wake ni wa nini; kamisaa ambaye anawaza ya zamani; asiyeweza kutambua mahitaji mpya ya kijamii na kwa maana hiyo amsaidie rais katika kutekeleza yale yanaohitajika na jamii kwa wakati wake.

Werema ni tatizo kubwa zaidi: Huyu ni Jaji wa Mahakama Kuu. Amekaa katika idara ya mahakama kwa muda mrefu wa kutosha na kwamba anajua jinsi sheria za taifa hili zinavyosigana.

Kwa uwezo wake na elimu yake, Werema anafahamu sheria nyingi tu ambazo zinazungumzia tofauti masuala mbali mbali katika jamii.

Ipo mifano hai, kwa mfano wakati sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inatambua ndoa ya umri wa miaka 15, zipo sheria nyingine kama ya makosa ya kujamiiana na ile ya watoto, ambazo zinaeleza maana ya mtoto kwa umri tofauti.

Lakini kuna mgongano wa wazi katika katiba ya Jamhuri na ile ya Zanzibar; wakati Zanzibar inajiita nchi, Jamhuri inaitambua kama sehemu ya nchi inayoitwa Tanzania.

Kuna uhuru wa kuwapo kwa serikali ya mseto Zanzibar jambo ambalo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hairuhusu.

Katiba ya Muungano hadi sasa, bado inamtambua waziri kiongozi, lakini katiba ya Zanzibar inatambua makamu wawili wa rais. Katiba ya Muungano haitaji mahali popote makamu wawili wa rais, kazi zao na itifaki zao.

Yenyewe inamtambua waziri kiongozi na rais wa Zanzibar, basi.

Lakini kuna jingine pia. Werema aanafahamu kuwa katiba ya sasa inaakisi kwa kiwango kikubwa mno mfumo wa chama kimoja.

Hili linadhihirika katika mpangilio wa madaraka ya kila muhimili, kwa maana ya Mahakama, Bunge na Serikali (Utawala); nguvu na mamlaka makubwa mno yameachwa kwa serikali kwa gharama ya mihimili mingine.

Ilitarajiwa kuwa Werema ambaye alikwisha kutumikia muhimili wa mahakama kwa muda mrefu, angekuwa chachu ya mabadiliko; kwamba angekuwa ni mtu wa kwanza kushauri mabadiliko ili kujenga taifa bora zaidi kisheria na kikatiba. Lakini wapi? Hakufanya hivyo!

Ninachoweza kusema ni kwamba Werema na Kombani walicheza karata zao vibaya kwa namna ile ile ya viongozi wetu kusukumwa na tabia ya kujikomba na kufurahisha wakubwa.

Hawa wawili waliamini rais Kikwete hakuwa tayari kukubali changamoto ya katiba mpya, na walifanya hivyo bila hata kumuuliza.

Sasa amewaaumbua. Je, watakuwa na ujasiri gani wa kusimama hadharani na kusema wanamsaidia rais ili hali wanapingana naye?

Ingelikuwa ni mimi, mara baada ya kauli ya rais Kikwete kwamba anakubali katiba mpya, ningeomba kukaa pembeni kwa kuwa nimeshindwa kumshauri bosi wangu katika jambo kubwa na nyeti la wakati wa sasa na ujao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: