Wezi wa Dowans hawa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Edward Hoseah, Mkurugenzi wa Takukuru

MAFISADI watatu waliojipanga kuchota Sh. 185 bilioni kutoka serikalini, zikiwa fidia kwa kuvunja mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, wamefahamika.

Vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya serikali na nje ya nchi, vinawataja wanaojiita wamiliki wa Dowans kuwa wote ni Watanzania.

Tarehe 15 Novemba mwaka huu,  Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), iliagiza Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kulipa fidia ya Sh.185 bilioni kampuni ya Dowans Holding Tanzania Limited.

Wanaojiandaa kuchukua kitita hicho wametajwa kuwa ni pamoja na mfanyabiashara mmoja nchini ambaye pia ni mbunge. Mwingine ni mwanasiasa mmoja aliyewahi kushika madaraka ya juu serikalini.

Anayetajwa kuwa mmiliki wa tatu wa Dowans, ni wakili mashuhuri nchini ambaye amewahi kutetea serikali katika kesi mbalimbali na mwenye mahusiano na makampuni ya uwakili nchini Uingereza.

MwanaHALISI lina majina yote ya wamiliki watatu, lakini linayahifadhiwa kwa sasa hadi hatua muwafaka za serikali ziwe zimechukuliwa.

Ili wamiliki hao waweze kutapa fedha hizo, sharti kwanza hukumu ya ICC juu ya kesi hii, isajiliwe katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Lakini waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ameliambia MwanaHALISI kuwa ama usajili utachukua muda mrefu au utashindikana kufanywa kutokana na sababu mbili.

Kwanza, miongoni mwa wamiliki kuna wawili ambao hawataki, piga ua, majina yao yahusishwe na Dowans kwa kuwa wako karibu na kile kinachoitwa “jikoni.”

Hawa wangependa kutumia ushawishi ili walipwe fedha hizo bila kufuata utaratibu wa kusajili hukumu mahakama kuu, au ikibidi, basi “fedha hizo zipotee.”

Pili, wangependa kukamilisha mradi wao wa kusajili Dowans katika moja ya nchi za nje ambako iliwahi kudaiwa miaka mitano iliyopita kuwa ndiko ilisajiliwa.

Nchi hiyo imetajwa kuwa ni Costa Rica.

“Hatua yeyote ya kuisajili kesi hii katika mahakama za ndani, itasababisha kufumka kwa msululu wa mambo yaliojificha. Hata wamiliki halisi wa Dowans watajulikana,” ameeleza waziri huyo.

Kufahamika kwa wamiliki wa Dowans, kumekuja siku tatu baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza wahariri wa vyombo vya habari nchini kuwa Dowans ni “genge la watu wachache wanaofahamika.”

Hata hivyo, Pinda hakutaja majina ya wamiliki hao, badala yake alisema wamiliki hao ni wale walioamua kutafuna rasilimali za taifa bila huruma.

Pamoja na kujua hivyo, Pinda hakusema ni hatua gani serikali itawachukulia watu hao, isipokuwa alisema, ikibidi serikali italipa fedha hizo.

Aidha, kufumuka kwa taarifa za wamikiki wa Dowans, kumekuja wiki mbili tangu spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta kunukuliwa akisema, “Dowans ni genge la watu watatu wanaotaka kutumia fedha hizo kutafuta urais mwaka 2015.”

Kauli za Pinda na Sitta zinaonyesha kuwa wahusika wanafahamika vema. Lakini hakuna hata mmoja wao ambaye anataja majina yao.

Kufahamika kwa “matajiri” wa Dowans kwa Pinda na Sitta kuna maana kwamba kunafahamika pia kwa Rais Kikwete ambaye ni mteule wao; vinginevyo wangekuwa wanahujumu serikali yake kwa kujua jambo kama hili na kushindwa kumwambia.

Wachunguzi wa mambo wanasema kauli za viongozi hao wawili zinaweza kuwa zinalenga kumshawishi Rais Kikwete kujenga ujasiri na kuwataja hadharani kabla wao hawajamuumbua.

Hata hivyo, kujulikana kwa vigogo wa Dowans, kumekuja siku tatu baada ya Edward Hoseah kuripotiwa na vyombo vya habari vya nje, akimtuhumu Rais Kikwete kuwakinga watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Mkurugenzi mkuu huyo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), amenukuliwa na mtandao wa WikiLeaks akisema, “Kikwete amekuwa mgumu kushughulikia viongozi wa serikali na wale wa vyombo vya dola wanaotuhumiwa kwa rushwa.”

Mtandao wa Wikileaks ulinukuu mazungumzo kati ya Hoseah na mwanadiplomasia mmoja wa Marekani, Purnell Delly akidai, “Kikwete hataki kuwa wa kwanza kuweka utaratibu wa kuwafikisha mahakamani viongozi wa zamani kwa makosa waliyofanya wakiwa madarakani.”

Madai hayo ya WikiLeaks yalichapishwa katika gazeti la The Guardian la Uingereza, juzi Jumamosi.

Kauli inayodaiwa kuwa ya Hoseah kwa Delly, inaelekea kuthibitishwa na msimamo wa Kikwete alioutoa kwa wahariri wa vyombo vya habari mwanzoni mwa mwaka 2007 pale aliposema, “Si vema kuanza kuwachimbua viongozi wastaafu.”

Rais Kikwete alikuwa akijubu swali lililoulizwa na MwanaHALISI, iwapo serikali yake inaweza kumchukulia hatua, mtangulizi wake, rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa tuhuma za kufanya biashara akiwa ikulu; jambo linalopingana na utawala bora.

Katika mazungumzo yake na Delly, Hoseah andaiwa kusema, “Unapotaka kushughulika na viongozi hawa wakubwa, inajengwa picha kwako kwamba unachotaka kukifanya ni jambo la hatari…Hao unaotaka kuwashughulikia ndiyo waliokupa wadhifa…”

Mjumbe mmoja wa Kamati Teule ya Bunge ya Richmond ameliambia MwanaHALISI juzi Jumatatu, kamati yake inaweza kuthibitisha kwamba “Richmond na hata Dowans ni makampuni feki.”

Amesema Bunge liliwahi kujulishwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Costa Rica, ambaye ndiye Msajili wa Makampuni, Mei 2008 kuwa katika nchi hiyo hakuna kampuni yenye jina Dowans Holding SA Limited.

Msingi mkuu wa kupinga malipo kwa Dowans, ni kuvuja kwa taarifa zinazoeleza kuwa hadi Aprili 2010, hakukuwa na kampuni ya aina hiyo nchini humo; kuibuka kwa Dowans kulikuja mwaka mmoja baada ya serikali kuvunja mkataba.

Taarifa zinasema, tayari baadhi ya wanasiasa wakiwamo viongozi wandamizi serikalini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani, wamejipanga kuhakikisha kampuni hiyo hailipwi mabilioni hayo ya shilingi.

Waziri mwingine ndani ya serikali ya Rais Kikwete ameliambia MwanaHALISI, juzi Jumatatu, “Nakuhakikishia Dowans haitaambulia chochote. Kama chama kupasuka, basi kipasuke.”

Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na jopo la wasuluhishi, Gerald Aksen, Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, Serikali inatakiwa kuilipa Dowans dola za Marekani 24,168,343 na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka.

Malipo mengine ni dola 19,995,626 ambazo zinatakiwa kulipwa tokea 15 Juni 2010 hadi fidia hiyo itakapokuwa imelipwa.

Kiasi kingine ni cha dola 39,935,765 na riba ya asilimia 7.5; na dola za 36,705,013.94 ambazo zinatakiwa kulipwa kuanzia 15 Juni 2010 na dola 750,000 ambazo zinatakiwa kulipwa kwa wasuluhishi.

Dowans wanatakiwa kulipwa kiasi kingine cha dola 1,708, 521 ikiwa ni gharama za uendeshaji wa kesi.

Katika mazungumzo yao, Delly anamnukuu Hoseah akikiri kuwa rushwa ilitumika katika ununuzi wa rada ya kijeshi iliyonunuliwa wakati wa utawala wa Mkapa.

Anasema taasisi yake imegundua kufanyika ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), lakini wahusika wanalindwa na Kikwete.

Wakati Hoseah akizungumza na Delly mwaka 2007, tayari kashfa ya ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT, tayari ilikuwa imefumuka.

Hadi leo watuhumiwa wakuu wa wizi katika EPA, akiwamo mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, ambayo ilichota zaidi ya Sh. 40 bilioni, ama hawajakamatwa au hawajafikishwa mahakamani.

Katika mazungumzo yake na Delly, Hoseah anadaiwa kusema miongoni mwa wahusika wakuu katika kesi ya rada, ni maofisa wa wizara ya ulinzi pamoja na maofisa wa ngazi za juu katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWT).

“Hoseah alisema pasi na kuficha kuwa kesi zozote zinazomhusu rais au waziri mkuu hazijadiliki. Zinawekwa kapuni. Na wale wote walio karibu nao huwa hawagusiki,” inasema taarifa hiyo ya Delly kwa serikali ya Marekani.

“Kama utahudhuria mikutano iliyoandaliwa na hao watu wa karibu na rais au waziri mkuu, utaona wana tabia ya kuonyesha kwamba, bila wao wewe si chochote na kama utawageuka, basi maisha yako yatakuwa hatarini,” Hoseah amedaiwa kusema kwa mujibu wa WikiLeaks.

Akizungumzia madai hayo ya Hoseah, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyamamu alisema kama kweli mkuu huyo wa TAKUKURU aliyasema hayo, basi hakusema ukweli.

Alisema Rais Kikwete amefanya makubwa katika kupambana na rushwa kuliko rais mwingine yeyote aliyepita, na ushahidi wa takwimu na hali halisi unathibitisha hilo.

Alisema idadi ya kesi za watuhumiwa wa rushwa imeongezeka mahakamani, huku TAKUKURU ikiongezewa meno, utaalamu na bajeti yake ikipanda kuliko wakati mwingine wowote.

Hata hivyo, Salva aligoma kuzungumzia kauli ya Kikwete ya kulinda viongozi wastaaafu.

“Sasa sijui mlitegemea mheshimiwa rais afanye nini zaidi ya hapo. TAKUKURU imepewa kila kitu na imepewa meno; au mlitaka rais aende mwenyewe kukamata watu ndiyo juhudi zake zionekane,” alisema Salva akijibu madai ya Hoseah.

Alisema, “Kama hilo ndilo mnalolitaka haliwezekani. Rais ni muumini mkubwa wa utawala wa sheria ambao unaviachia vyombo na taasisi za kisheria kufanya kazi zake.”

Tayari ubalozi wa Marekani nchini umefanya uchambuzi wa mazungumzo kati ya Hoseah na Delly kubainisha kuwa inawezekana mkuu huyo aliamua kufuatilia rushwa katika suala hilo la rada kwa vile tu Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) ilimletea mafaili yenye taarifa zisizo na shaka kuhusu suala hilo.

Taarifa ya Hoseah inachukuliwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa kuwa Rais Kikwete anamfahamu mmiliki wa Dowans, lakini anashindwa kumchukulia hatua kwa kuwa anahusishwa na mmoja wa maswahiba zake.

 

0
Your rating: None Average: 4.5 (4 votes)