Wilson Mukama ndio ujio mpya CCM?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Wilson Mukama

TUMEAMBIWA Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejivua gamba. Wapo wanaoamini hilo ni kweli na wapo wasioamini. Nimeamua kutokuwa na hitimisho. Nataka kidogo tutazame kilichofanyika.

Unapotaka kujadili chochote kuhusu CCM, ni muhimu ukaangalia pia vyama vingine vinavyofanana nacho. Na kwa leo, nitapenda zaidi kutumia mfano wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na kile cha Labour cha Uingereza.

Lakini, kuna tofauti kidogo kati ya CPC na Labour na hivyo ni muhimu pia kuangalia tofauti yenyewe kabla ya kulinganisha na CCM moja kwa moja. Tunatafuta uwiano.

CPC, kama ilivyo CCM, ni chama cha kimapinduzi. Kwa lugha nyingine, ni chama cha kikada. Ndiyo maana kila siku kuna watu wanaitwa makada wa CCM. Bila ya kuwa na chama cha kikada, huwezi kuwa na makada.

Wao wameweka utaratibu wa uongozi kila wakati unapofika. Miaka 20 iliyopita, nchi iliongozwa na Jiang Zemin kama Rais na Zu Rongji kama Waziri Mkuu.

Walipoondoka madarakani kina Zemin mwaka 2003, ikaja zamu ya Hu Jintao kama rais na Wen Jiabao, waziri mkuu. Na mwakani, kina Hu wanaondoka na wafuatiliaji wa siasa za China wanajua itakuwa ni zamu ya Xi Jinping kama rais na Li Kenqiang, waziri mkuu.

Cha msingi hapa ni kuwa CPC inatengeneza viongozi wake wa kesho. Ingawa China ina mfumo wa chama kimoja, ingekuwa shaghalabaghala kama watu wangeachiwa tu wawanie madaraka kiholela. CCM, ilikuwa na utaratibu huu wa kutengeneza viongozi wa kesho. Umefutika.

Ukiutazama umoja wake wa vijana, UVCCM, ambao zamani ulikuwa tanuri kuu la kupika viongozi, utaona leo kuna kundi tu la vijana wanaofanya kazi kwa maelekezo ya watu waliowafadhili kupata madaraka. Wanafanya kazi za watu badala ya zile za umoja wao, kwa jumla, za chama chao.

Kwa hiyo, chama cha kikada kisicho mtiririko mzuri wa kubadilishana uongozi, hakiwezi kuwa na maisha marefu. Na hata kama CCM inadai kuwa imevua gamba, kama haijatengeneza watu wa kubeba mustakabali wake, haitabadilika kitu.

Chama kingine cha kikada – Chama cha Kikomunisti cha Urusi, kilijua tu wakati Vladmir Lenin atakapokufa, mrithi wake atakuwa Josef Stalin au Leon Trotsky. Na kweli Stalin alikuja kurithi uongozi.

Swali linakuja: kama Kikwete ataachia madaraka leo, nani atachukua nafasi yake ndani ya CCM? Jibu rahisi litakalotoka ni “wapo wengi.”

Lakini hii si namna nzuri ya kuendesha chama cha kikada. Ilipaswa ijulikane mapema nani atashika usukani akistaafu Kikwete. Mshika usukani ninayekusudia ni yule mwenye uwezo binafsi wa kuongoza siyo wa kubebwa.

Kwa hiyo, hata kama CCM inadai kujivua magamba, hatari kwa chama bado ipo kwa sababu wakati uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 utakapokaribia, kutaibuka vita au mivutano ya ndani kwa ndani miongoni mwa wanaotaka urais.

Na hapa ndipo linapokuja suala la kina nani waliopewa madaraka ya kuongoza CCM. Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) uliofanyika Dodoma wiki iliyopita, ulichagua Sekretarieti mpya inayoongozwa na Wilson Mukama, kama katibu mkuu.

Huyu simfahamu sana. Wanaomjua wanasema ni kada mzuri wa CCM na wanaamini ni kiongozi mwafaka kwa chama sasa. Wanaosema hivyo ni watu wazima na nataka kuwaamini.

Hata hivyo, pamoja na kwamba nataka kuwaamini watu wazima hawa kiumri na uadilifu kiutumishi, ninapata shida sana na uteuzi wa Mukama kwenye nafasi hiyo.

Chama chochote kianchotaka kujivua gamba, pamoja na mambo mengine, huwa kinabadilisha kizazi cha uongozi. Huwezi kujivua magamba na ukabaki na kizazi cha kale madarakani!

Neil Kinnock wa Labour, aliacha madaraka kwa akina Tony Blair na Gordon Brown zaidi ya miaka 15 iliyopita ili chama hicho kijivue gamba na kuleta Labour mpya. Akina Blair wote walikuwa na miaka chini ya 40.

Na baada ya Brown kushindwa uwaziri mkuu mwaka jana. Labour kimejivua gamba na kumpa madaraka Ed Milliband mwenye umri wa miaka 41 tu. Huko ndiko kujivua gamba kihalisia.

Kujivua gamba kwa CCM kunashangaza. Rais Kikwete ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM, ana umri wa miaka 60, mdogo kwa Mukama, aliyekwishapita hapo.

John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu na msaidizi mkuu wa Mukama, ana miaka 60. Pius Msekwa, ambaye ni Makamu Mwenyekiti na msaidizi mkuu wa Kikwete, ana umri wa miaka 76. Ni gamba gani ambalo CCM imejivua?

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, asilimia 44 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 18. Ina maana idadi kubwa ya Watanzania sasa ni vijana. Viongozi karibu wote wa CCM ngazi ya taifa, ukiondoa Nape Nnauye na January Makamba, wako nje ya kundi hili kubwa la wananchi.

Mwaka 1943, kada maarufu wa CPC, Chou En Lai, yule ambaye aina ya suti alizokuwa akivaa ndio baadaye zilikuja kuigwa na kina Julius Nyerere, Kingunge Ngombale-Mwiru na John Malecela, aliandika kitabu kilichoitwa How To Be A Good Leader – Vipi uwe kiongozi makini – ambacho utakisoma vizuri ukipekua mtandao wa google.

Ndani ya kitabu hiki, aliandika umuhimu wa kiongozi kuwa na uwezo wa kuhamasisha watu, kupendwa na wananchi, kuwa na mvuto kwa wananchi na kuwa na nguvu na ari ya ujana.

Sioni sifa hizo katika kundi hili la viongozi wa chama kinachojinasibu kimejivua magamba. Huwezi kuwa na chama kipya ambacho viongozi wake wana umri mkubwa.

Katika dunia ya sasa, vyama vinavyotaka kujivua magamba na kubaki madarakani, huwa na turufu moja ya hizi mbili kubwa za kutumia: wagombea vijana au wanawake. Ukipata kijana mwenye uwezo au mwanamama mwenye uwezo, wananchi huwa tayari kupokea mabadiliko.

Angalia George W. Bush na Barack Obama (Marekani). Tupia jicho kwa Jacques Chirac na Nicholas Sarkozy (Ufaransa), Gordon Brown na David Cameroon (Uingereza) na tena George Bush na Bill Clinton (Marekani). Turufu ya ujana ilikuwa kigezo kikubwa.

Kwa upande mwingine, vyama vingi vimeshinda uchaguzi kwa sababu ya kuweka wagombea wanawake. Julia Gillard alimshinda Kevin Rudd, kwa sababu ya kinamama wengi kujitokeza kumuunga mkono mwenzao.

Wapo kina Christina de Fernandez Kirchner (Argentina) Tarja Halonen (Finland), Hellen Johnson Sirleaf (Liberia), Jadranka Kosor (Croatia) na Angela Merkel (Ujerumani). Wote hawa walishinda katika uchaguzi kwao na jinsia yao (pamoja na kwamba pia wana uwezo) ilichangia.

Kama Obama asingewania urais wa Marekani, huenda leo Marekani wangekuwa na rais mwanamke kwa jina la Hillary Clinton. Hiyo ndio faida ya siasa za kisasa zenye ukweli na mantiki.

CCM, kwa mfano, haijawahi kuwa na Katibu Mkuu mwanamke licha ya kuwa na wanawake wengi wenye uwezo wa kushika nafasi hiyo. Kwa kuteua mwanamke tu, CCM ingekuwa imejivua gamba moja kubwa na watu wangepokea kwa shangwe uamuzi huo. Kingejionesha kuwa kimelenga kubadilika.

Katika zama hizi, si muhimu sana kuwa na mtu mwenye msimamo au mwenye kukijua vema chama ili kushinda. La muhimu zaidi ni kuwepo viongozi au wagombea wa ushindi.

Lakini, sijui chama chochote kilichowahi kushinda katika uchaguzi huru na wa haki katika miaka ya karibuni kikiwa na viongozi wa juu wenye wastani wa umri wa miaka 60. Sijui.

Mimi nawaza hivi. Lakini haya yatajidhihirisha au kupotoka kadiri muda unavyokwenda.

0
No votes yet