Wimbo waibua makovu ya ubaguzi A. Kusini


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Julius Malema, Rais wa kitengo cha vijana cha ANC

MISUGUANO ya ubaguzi wa rangi iliyokuwapo baina ya wazalendo weusi na weupe huko Afrika ya Kusini haijaisha?

Miaka 16 sasa baada ya kile kilichoitwa “kuzikwa” kwa itikadi chafu na ya udhalilishaji mkubwa ya ubaguzi wa rangi, na baada ya karibu muongo mmoja tangu Tume ya Maridhiano (Truth and Reconciliation Commission) iliyoongozwa na Archbishop Desmond Tutu imalize kazi yake, misuguano hiyo bado ipo.

Makovu yapo na wanaharakati wa chama tawala – African National Congress (ANC) wameazimia kwamba makovu hayo yanaimbwa kwa sauti kubwa kama kumbukumbu ya mapambano yao dhidi ya ubaguzi.

Wiki iliyopita chama hicho kilikata rufani mahakamani kupinga upigwaji marufuku wa wimbo maarufu wa ‘Shoot the Boer’ (‘Piga Risasi Kaburu’) au kwa lugha ya ki-Xhosa ‘dubul' ibhunu’ – wimbo unatumiwa na wafuasi wa chama hicho hadi hivi leo.

Makaburu ni raia wa Afrika ya Kusini wenye asili ya Ulaya ambao walikuwa wanaendesha utawala wa kibaguzi dhidi ya watu weusi hadi mwaka 1994 ulipotokomezwa.

Wimbo huo ulipigwa marufuku kuimbwa hadharani na kwenye vyombo vya habari kufuatia hukumu iliyotolewa na Kaimu Jaji wa jiji la Johannesburg, Leon Halgryn, mapema mwezi March mwaka huu. Jaji huyo alisema kuimba na kuchapishwa kwa wimbo huo ni ukiukwaji wa katiba na uvunjaji wa sheria kwa sababu kunaridhia jinai ya uchochezi.

Halgryn alisema katika hukumu yake kwamba matumizi ya maneno ‘piga risasi’ katika wimbo huo ni sawa sawa nu kusema ‘ua.”

Aliongeza: “Kwa maoni yangu, matumizi ya maneno hayo yanalenga kuchochea mauaji ya watu weupe. Sina shaka yoyote kwamba mdaiwa (ANC) alikuwa na maana ya kuwaua watu weupe.”

Gazeti la Sunday Independent limeripoti mwishoni mwa wiki kwamba katika rufaa yake, chama tawala – ANC – kimesema wimbo huo ni sehemu muhimu ya historia ya mapambano ya kujikomboa na kwamba bado huimbwa na wafuasi wa chama hicho.

Rufaa hiyo ilikatwa na Naibu Katibu Mkuu wa ANC, Thandi Modise ambaye alisema: “Kwa heshima na taadhima natoa tangazo la kisheria kwamba wimbo wenyewe unajulikana na kuimbwa na maelefu ya wananchi wa Afrika ya Kusini. Hivyo ni wazi kabisa matokeo ya ukiukwaji kwa amri ya marufuku iliyowekwa itaathiri wengi sana.”

Aliongeza kwa kusema kwamba ANC inaamini bila wasiwasi wowote kwamba mahakama hiyo ingefikia maamuzi tofauti iwapo kwanza ingekuwa imeshauriana na ANC kuhusu historia na madhumuni ya wimbo huo.

Aidha upigwaji marufuku wa wimbo huo ulishutumiwa vikali na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini humo – The Congress of SA Trade Unions (Cosatu). Katika taarifa yake Cosatu ilikubaliana moja kwa moja na ANC kwamba baadhi ya maneno yaliyomo kwenye wimbo huo kama vile ‘Ayesaba Amagwala’ (The Cowards are Scared – yaani ‘Waoga sasa Wanaogopa’) ni sehemu muhimu ya harakati za ukombozi wa nchi.

Hata hivyo Cosatu ilikiri kwamba kwa tafsiri ya neno kwa neno, wimbo huo unaonekana kuibua chuki baina ya watu wa rangi mbali mbali nchini humo na kuchochea ghasia.

Lakini, Cosatu iliongeza, “nyimbo za aina hii zilizokuwa zinaimbwa wakati wa harakati za mapambano zimekuwa zikilelewa na kukua ndani ya jamii kuonyesha kwamba idadi kubwa ya watu weusi walikuwa wananyimwa haki ya kupiga kura na serikali ya weupe wachache kwa kutumia nguvu ya mtutu wa bunduki.

“Maneno ya wimbo yanaonyesha hasira kubwa waliyonayo watu ambao walikuwa wanaonewa, wanashambuliwa na kuawa na dola…. Watu ambao walinyimwa haki zao zote za kiraia hali kadhalika utaratibu, namna na sheria ya kurudisha mapigo.”

Cosatu ilisema kwamba nyimbo zilizokuwa zinaimbwa enzi hizo za ubaguzi zililenga mapambano hayo dhidi ya mfumo ambao ulishutumiwa duniani kote kama ni wa kidhalimu dhidi ya binadamu.

Taarifa ya Cosatu iliendelea kusema kwamba muungano huo unatambua umuhimu wa jitihada zote zinazofanyika katika kuleta maridhiano baina ya watu wa rangi mbali nchini Afrika ya Kusini na kuzika tofauti zilizokuwapo. “Lakini hii isiwe ina maana ya kwamba tusahau kabisa maumivu makubwa tuliyopata wakati ule.”

Kesi ya awali kupinga matumizi ya wimbo huo ilipelekwa mahakamani na mfanyabiashara mmoja wa Johannesburg, Willem Harmse ikilenga kumkataza mshiriki wake wa kibiashara Mahomed Vawda, kutumia maneno ya wimbo huo katika mabango ambayo yangetumika katika maandamano yaliyokuwa yameandaliwa dhidi ya wimbi la ghasia na uvunjaji wa sheria uliozuka nchini humo.

Baada ya hukumu hiyo, vikundi vya wanaharakati wanaotetea haki za binadamu nchini humo walidhamiria kwenda tena mahakamani kuomba amri ya kumkataza rais wa kitengo cha vijana cha ANC (ANC Youth League – ANCYL), Julius Malema kutoimba maneno ‘Piga Risasi Kaburu.’

Malema alikuwa amedhamiria kuimba maneno hayo pamoja na marufuku ya mahakama, kwa sababu kwamba ANC ilikuwa imepanga kukataa rufaa katika mahakama ya juu.

Nacho chama kinachotetea masilahi ya watu weupe nchini Afrika ya Kusini – FF Plus and the Afrikanerbond kimesema Malema tayari alikuwa ameshatenda kosa hilo pale alipoimba wimbo huo katika hafla ya kuzaliwa kwake mjini Polokwane na pia katika Chuo Kikuu cha Johannesburg.

Kiongozi wa chama hicho, Pieter Mulder alisema kwamba anapendekeza kwa mamlaka ya nchi hiyo Malema ashitakiwe kwa kukiuka sheria hiyo.

0
No votes yet