Wizara zirejeshe fedha za CIS


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

USEMI kwamba "ondoa banzi kwenye jicho lako…," unatakiwa kuzingatiwa na serikali kwa kurejesha fedha zote zilizochotwa na wizara nane kutoka uliokuwa Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa nje ya Nchi (CIS).

Serikali ina wajibu wa kurejesha Sh. 44 bilioni zilichotwa visivyo.

Awali baadhi ya wafanyabiashara, wanasiasa na watu maarufu walitajwa kuhujumu mpango huo kwa namna mbalimbali.

Miongoni mwa hujuma ni wafanyabiashara maarufu kutumia watu kwa udanganyifu, kuanzisha kampuni zilizotumika kuchota fedha CIS.

Hujuma zilizobainika kutumiwa na wizara ni za kufuata taratibu stahili katika kukopa fedha hizo, kisha kukana kuhusika na madeni huku nyaraka muhimu za kuthibitisha ukopaji zikiwa zimeyeyuka. Hii ni aibu kwa serikali.

Hili halina ubishi kwani Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo amekiri hivi karibuni baada ya baadhi ya vyombo vya habari kutoa taarifa hizo.

Mkullo alikiri hayo baada ya kuwashirikisha ‘vijana wake wa kazi’ ambao walifuatilia madai hayo kwa siku tatu.

Hoja hapa ni kwamba, endapo ‘vijana wa kazi’ hawakupata ushahidi wa serikali (wizara) kujikopesha fedha ilizotakiwa kuzisimamia ili kuhakikisha sekta ya biashara inaimarishwa, nani mwenye uwezo wa kuupata?

Kupotea kwa ushahidi huo kunadhihirisha kuwa nia ya wizara husika haikuwa nzuri bali kuhujumu mpango mzuri uliokusudiwa kuinua kipato cha jamii kupitia sekta hiyo.

Kitendo cha wadeni wengine wa CIS kuendelea ‘kubanwa mbavu’ wakitakiwa kulipa wanachodaiwa huku serikali ‘ikiziba’ masikio na ‘kufumba’ macho dhidi ya wizara zake, ni aibu nyingine.

Ikiwa nyaraka nyeti kama hizo zinatajwa kupotelea ndani ya wizara ya Fedha na Uchumi, ni dhahiri serikali inakabiliwa na mtihani katika kuhifadhi nyaraka nyeti.

Katika hali ya kawaida, matumizi ya wizara hutegemewa kuzingatia bajeti iliyopitishwa na mamlaka husika, kabla ya kuidhinishwa na Bunge.

Sasa ni mazingira gani yaliyosababisha wizara kukopeshwa fedha na CIS?

Kule kutajwa tu kuwa wizara fulani ilichukua fedha hizi, ni ushahidi tosha wa kuwa mdaiwa.

Iliyokuwa wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, wizara ya Kazi, wizara ya Kilimo, wizara ya Maji, wizara ya Afya na ya Mambo ya Ndani ndizo zinazoonekana kwenye orodha ya wadaiwa wa CIS, kwa upande wa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar, wizara ya Maji na wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi nazo zinatajwa kukopa CIS katika mpango uliotekelezwa 1984-1998.

Kinara wa kukopa kwa mujibu wa orodha ya wadaiwa ni wizara ya Kazi, iliyokopa mara kumi, kwa nyakati tofauti.

Ushahidi pekee wenye nguvu ya kuthibitisha ukopaji ni nyaraka zinazoelezea mchakato mzima: Mathalani barua ya maombi, mkataba hadi nyaraka za makabidhiano ambazo nazo zinadaiwa hazipo.

Wakati nyaraka hizo zimetoweka, majina ya wizara husika hayajaondolewa kwenye orodha za wakopaji, ikiwa ni pamoja na mwaka na kiasi walichokopa.

Lazima Hazina ifahamu zilipo nyaraka, la sivyo, ichunguze na kujiridhisha ili fedha zirejeshwe.

Miongoni mwa wizara zote nane zilizoelezwa kukopa CIS, ni Mambo ya Ndani pekee iliyokiri, tena kwa maandishi, kwamba ilikopeshwa fedha hizo.

Taarifa zinasema wizara ilitumia fedha hizo kununua magari ya kikosi cha Zimamoto katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

Lakini, imebainika hakuna ushahidi unaothibitisha wizara ililipa deni.

Hilo nalo linahitaji kufuatiliwa na kutolewa taarifa na endapo kweli wizara hiyo imerejesha fedha, hoja ibaki kama kweli ilistahili kukopa CIS.

Aidha, waziri mwenye dhamana kukiri kuwa nyaraka hizo hazipo wizarani, pasina kueleza kilichojiri hadi miongoni mwa wadeni wa mfuko ambao wizara yake inausimamia, inaleta mashaka.

Serikali itafiti jambo hili na ije na majibu ya kuridhisha kuhusu kiini cha wizara zake kutajwa kama wadaiwa wa CIS huku wenyewe wakikana kukopa. Nyaraka zinazothibitisha lazima zitafutwe na ijulikane waliozitupa na wachukuliwe hatua za kisheria.

Wahenga husema ‘mficha ugonjwa kifo humuumbua,’ kwani taarifa za uhakika zimebaini kuwa baadhi ya balozi za nchi zilizochangia fedha katika mfuko huo zimeanza kufuatilia kwa karibu marejesho ya fedha hizo.

Ufuatiliaji huo umebainika kufanywa kwa kutumia njia zisizokuwa rasmi. Baadhi ya Balozi zimeanza kuonesha nia ya kutoa ushahidi, kuthibitisha kwamba wizara zinazokana madeni zinahusika nayo.

Hiyo inamaanisha kuwa endapo serikali itaendelea kufumbia macho taarifa hizo, itaumbuka baada ya serikali za nchi zilizotoa fedha kutekeleza azma hiyo.

Ingawa hakuna sababu inayoweza kuhalalisha wizara kuchukua fedha CIS, lakini ni heri ifahamike kuwa zilichukua na zirejeshwe kabla ya kuumbuliwa.

0
No votes yet