Wizi wa kura wanukia


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
WAKALA wa chama cha siasa anayesimamia uchaguzi

MAWAKALA wa vyama vya siasa wanaosimamia uchaguzi, wametengewa “kiasi kikubwa” cha fedha ili kusaliti wagombea wao, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za ndani ya vyama hivyo na ambazo zimethibitishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe zinasema fedha hizo zitatolewa mara baada ya zoezi la kupiga kura.

Mbowe amesema tayari chama chake kimegundua mpango huo, na kwamba wamejiandaa kukabiliana na kila hatua katika kipindi hiki cha “lala salama.”

“Tuko katika kipindi cha lala salama. Tumejiandaa kwa kila hali kukabiliana na kitakachotokea. Tumewambia wanachama wetu wawe wavumilivu na tunawaeleza mawakala wetu kokote walipo kuwa ulinzi wa kura ni jambo ambalo halihitaji mzaha,” amesisistiza.

Taarifa zinasema mawakala hao wamepangwa “kununuliwa” ili kufanikisha mpango wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumuingiza mgombea wake, Jakaya Kikwete madarakani.

Imeelezwa kuwa viongozi wa vyama tayari wamejiandaa kufikisha taarifa za njama hizi kwa vyombo vya habari na jumuiya ya kimataifa wakati wowote kuanzia leo.

Mpango wa kuiba kura kupitia mawakala unatarajiwa kufanyika kupitia kile kinachoitwa, “kuokoa majimbo yasiteketee.” Unadaiwa kusukwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba juu ya chama chake kutaka kununua mawakala, hakupatikana kuzungumzia suala hilo. Simu yake ilikuwa haipatikani.

Mkurugenzi wa kitengo cha Parapaganda cha CCM, Tabwe Hiza alikataa kulizungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba yeye si msemaji wa chama hicho.

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Abdulrahman Kinana juu ya tuhuma hizo, haraka alisema, “Sasa hivi niko kwenye ndege.”

Akiongea kwa sauti ya upole, Kinana alisema, “Kama unataka kuzungumza na mimi kuhusu mambo ya kampeni zetu, naomba uje ofisini kwangu kesho (jana) asubuhi. Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote,” alieleza.

Naye mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amesema iwapo mpango wa kununua mawakala utafanikiwa, umelenga kuongeza kura kutoka kwa watu ambao hawatajitokeza kupiga kura.

Amesema kinachowezekana ni kuiba kura kupitia watu ambao hawakupiga kura.

“Ngoja nikuambie ndugu yangu, hakuna ambacho CCM wanakipanga ambacho mimi sikifahamu. Hawa jamaa wamepanga kuiba kura kupitia watu ambao hawatajitokeza kupigakura. Wamepanga kumuona kila wakala mara baada ya zoezi la kura kumalizika,” ameeleza.

“Kwa mfano, kituo kina watu 500. Iwapo watakaokuwa wamejitokeza ni 300, basi mawakala watakaonunuliwa wataachia kupigwa kura feki 200 ambazo kati ya hizo asilimia karibu 90 zitapelekwa kwa mgombea wa CCM na zilizobaki watazipiga kwa wagombea wa upinzani,” amefafanua Dk. Slaa.

Amesema mpango huo waweza kutekelezwa kwa kushirikisha mawakala wa vyama na wasimamizi wa vituo.

“Lakini sisi tumejipanga kulinda kura zetu. Tayari nimewajulisha wagombea wangu wote nchi mzima kutafuta mawakala waaminifu wa kulinda kura zetu,” ameeleza.

Anasema, “Wizi umepangwa kuwa highly computerized – kutumia mfumo wa komputa. Ni wizi wa matumizi ya mawakala kwa kuwarubuni. Tuko makini na idadi ya vituo na idadi kamili ya wapigakura kwenye kila kituo.”

Tayari CHADEMA kimelalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) juu ya idadi halisi ya wapigakura wakisema idadi iliyotangazwa na NEC haiwezi kukubalika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya chama hicho, Profesa Baregu amesema kwa anavyofahamu yeye na kwa mujibu wa takwimu za wasomi mbalimbali nchini, wakiwamo wale wanaotumiwa na serikali kuandaa bajeti, bado kuna shaka juu ya taarifa ya NEC kuhusu idadi ya waliojiandikisha.

NEC kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Lewis Makame imesema imeandikisha wapigakura 19,670,631 badala ya 21,210,187 ambao ndio watachagua rais, wabunge na madiwani katika uchaguzi Jumapili hii.

Tume imesema wapigakura milioni 1.54 wamefutwa kwenye daftari kutokana na kufariki na wengine kwa udanganyifu.

NEC imepanga vituo 52,000, na kwamba ili kupunguza msongamano, kila kituo kitakuwa na watu kati ya 450 na 500. Katika uchaguzi mkuu uliopita, vituo vya kupigia kura vilikuwa 47,150.

Katika uchaguzi mkuu wa 2000, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 10,088,484, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 8,517,598 sawa na asilimia 84.4.

Mwaka 2005 waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16,401,694, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 11,875,927.

Gazeti lilipomuuliza amepokeaje taarifa hizo, Dk. Slaa amesema hazimtishi na kwamba “safari yangu ya kwenda ikulu imeiva.”

“Tumezitumia vizuri siku 70 za kampeni na sina shaka kwamba wananchi wamekikubali chama chetu, wameelewa sera zetu na wanataka tuwaongoze, ameeleza Dk. Slaa katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii.

Dk. Slaa amesema amepata hata majina ya wanaotajwa kuwa katika mpango wa kupika matokeo kupitia njia ya IT.

Miongoni mwa aliowataja ni maofisa wa usalama wa taifa na mwalimu mmoja wa shule ya msingi jijini Dar es Salaam.

Amesema amepata taarifa kutoka vyanzo vyake vya ndani ya serikali kuwa chapisho la kwanza la karatasi za kupigia kura lilifanywa na wafanyakazi kwenye kiwanda cha uchapaji cha usalama.

Chapisho hilo ndilo lilipelekwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kutengeneza “karatasi hewa” na ambazo amedai kuwa zimepangwa kuingizwa katika mfumo wa uchaguzi.

Hata hivyo, mwalimu anayehusishwa kwenye uchakachuaji naambaye ni kiongozi katika Chama cha Walimu nchini (CWT) na jina lake tunalo, amekana madai hayo.

“Hiyo taarifa ni mpya kwangu. Mimi ni mwalimu tu wa shule ya msingi tena nafundisha watoto wa darasa la pili. Huyo aliyekwambia amekudanganya, naomba uniamini mimi.

“Sijawahi kukutana na watu wa serikalini wala usalama wa taifa. Siwajui na sijawahi kufanya nao mkutano hata siku moja,” ameeleza.

Amesema, “Mimi si mwanachama wa CCM. Nitapigaje kampeni ya kutaka chama hicho kipigiwe kura wakati mimi mwenyewe naidai serikali ya chama hicho mafao yangu mengi tu.”

Mwalimu huyo amesema, “Huo ni uzushi na najua mmepata namba yangu hiyo kwa wabaya wangu. Sijapewa kazi hiyo na nakanusha taarifa hizo.”

Lakini gazeti hili limefahamishwa kuwa Mwalimu huyo amepewa jukumu la kupitia kila mfanyakazi anayemfahamu, na hasa walimu wenzake, kuwaeleza kuwa iwapo Kikwete na chama chake wataingia madarakani, wataneemesha wafanyakazi.

“Kwanza, ameelezwa awambie wenzake kuwa Kikwete na chama chake wakiingia madarakani, watanemeesha wafanyakazi.

“Pili, wale watakaoshiriki kusimamia kuhesabu kura, wawe tayari kupokea maelekezo kutoka juu kuhusu uchakachuaji,” taarifa zimeeleza.

Taarifa nyingine zinasema mpango huo unatekelezwa pia kupitia ofisi isiyo rasmi ya CCM iliyopo Upanga, Dar es Salaam.

Uchunguzi wa MwanaHALISI umegundua kuwa NEC itatumia kompyuta zilizofungwa viwezeshi/viunganishi (modems) vya aina ya 3G kwa kupokelea matokeo kutoka mikoani.

NEC inasema imelenga kupokea matokeo kwa ustadi mkubwa ili kuziba mianya ya kujichanganya.

“Hapa ndipo upinzani unapotakiwa kuwekeza zaidi katika kuhakiki takwimu, huku ukilinganisha na matokeo kamili kutoka kwenye shina,” ameeleza mtaalamu mmoja wa mawasiliano ya kompyuta wa chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, nyumba ya hiyo tayari inalindwa na baadhi ya maofisa usalama na imewekewa kamera maalum za kuangalia wanaotoka na wanaoingia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: