Wizi wa kutisha Chuo Kikuu Huria


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

CHUO Kikuu Huria Tanzania (OUT) kimeingia katika kashfa nzito ya wizi wa mamilioni ya shilingi, MwanaHALISI limeelezwa.

Fedha zinazotajwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha ni zaidi ya Sh. 800 milioni.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kati ya kiasi hicho, Sh. 500 milioni ziliibwa katika idara ya malipo ya mishahara iliyokuwa ikiongozwa na Angelus Mlekaria.

Fedha kiasi kingine zaidi ya Sh. 300 milioni imeelezwa kuwa zimepotea mikononi mwa James Rweikiza, aliyekuwa mhasibu na mkuu wa kitego cha mikopo ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili imezipata jijini Dar es Salaam, zinasema kuwa wizi katika idara ya mishahara ni wa zaidi ya miaka mitano, wakati ule wa mikopo umefanyika miaka ya karibuni.

Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa Mlekaria anadaiwa kuchota fedha kupitia mishahara ya wafanyakazi hewa, baadhi yao wakiwa wamekwishahama au kufariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, watumishi hao tayari wamesimamishwa kazi na kesi zao ziko polisi kwa uchunguzi.

Hata hivyo, yapo malalamiko kuwa kesi hizo zinacheleweshwa kwa makusudi katika mkakati wa kuwezesha suala hilo kumalizwa kienyeji.

Inadaiwa kuwa Mlekaria alisimamishwa kazi zaidi ya mwaka mmoja uliopita lakini kesi yake ilikuwa “inaozea” Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

“Kila kitu kipo wazi kuhusu wizi wa fedha hizi, lakini ajabu hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya Mlekaria na Rweikiza,” anasema mtoa taarifa na kuongeza:

“Profesa Mbwette (Tolly, Makamu Mkuu wa Chuo) anajua kila kitu, lakini yuko kimya kwa sababu tunajua kwamba anazima kesi hizi. Zina karibu mwaka sasa hazijapelekwa mahakamani na amekuwa kimya.”

Lakini, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Mbwette, baada ya awali kukanusha, alithibitisha kutendeka kwa wizi wa fedha za chuo.

“Ukweli ni kwamba kuna wizi kama unavyosema ndugu mwandishi. Na hili jambo tunalichukulia kwa umakini mkubwa maana linataka kutumika kuchafua taasisi yetu.”

“Suala hili nalifuatilia kwa karibu. Na nianze tu kumzungumzia Rweikiza. Ukweli huyo bwana amekamatwa na kesi yake imefika mahakamani. Mahakama ndiyo chombo cha haki. Tusubiri mwenendo wa kesi na hukumu yake.

“Ama kwa hakika nipo makini kwa watu wanaotaka kuchafua taasisi hii maana haina doa la wanafunzi kugoma au nini. Ni watu wachache tu wanataka kutuchafua.

“Ukiacha huyo Rweikiza, kuna hili la Mlekaria. Hapa ulifanyika ukaguzi wa hesabu. Wakaguzi walitoka nje na wakagundua wizi mkubwa. Ni kweli, karibu mwaka…

“Mimi mwenyewe nashangaa kwanini kesi hii haiendi mahakamani. Mara kadhaa nimemtuma mwanasheria wa chuo kufuatilia. Huko amebaini jambo. Sababu kubwa ya kuchelewesha kesi ni mbinu za kuififisha,” alisema.

Profesa Mbwette amesema kufuatilia kwao kwa karibu, kumewezesha kesi hiyo kuiondoa Oysterbay na sasa imehamishiwa Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam.

Alisema kuna watumishi katika idara ya uhasibu wamesimamishwa, na wengine wanachunguzwa.

Kuhusu tuhuma kuwa utawala wa chuo umejitahidi kuzima kesi hizo, alisema, “mtiririko huo niliokueleza wa namna tulivyofuatilia, wenyewe unaniondoa katika tuhuma hizo. Eti mimi niwalinde watuhumiwa? Haiwezekani.”

Amesema wanafuatilia suala hilo kwa sababu kuna watu wamelenga kulitumia kwa nia ya kuchafua hadhi nzuri ya chuo hicho.

Alipotakiwa wiki iliyopita, kueleza upande wake, mtuhumiwa Mlekaria alisema aliitwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam lakini alibania kutoa maelezo zaidi.

“Mimi nimeitwa Polisi Kanda Maalum, hivi sasa nipo hapa polisi kwa jambo hilo hilo. Nikitoka nitakupigia ili tuzungumze,” alijibu mwandishi kwa njia ya simu.

Alipotafutwa baadaye hakupatikana kwani simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila ya kujibiwa. Hata alipotumiwa ujumbe kumkumbusha ama kupiga au kupokea simu hakujibu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alithibitisha polisi kuchunguza kesi hizo kwa sasa, lakini kwa sababu za majukumu nje ya ofisi, alitaka maelezo zaidi yatolewe na Mkuu wa Upelelezi Kanda (ZCO), Ahmed Msangi.

“Nenda ofisini kwa ZCO,” aliagiza Kova na ZCO Msangi alipopatikana juzi, alisema, “kaka hilo suala liko kwa Kamanda Kova.”

“Si mnajua msemaji mkuu wa kanda ni kamanda wa kanda maalumu…Sasa mnaniuliza mimi iweje ndugu yangu?” alihoji ZCO Msangi.

Hatimaye alisema angewasiliana na Kamishna Kova ili apate idhini. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa na Polisi.

MwanaHALISI lilipowasiliana na mmoja wa watumishi waliosimamishwa kwa tuhuma hizo, Gerald Massawe alisema, “ni kweli nimesimamishwa kazi na mwenzangu (hakumtaja).”

“Mimi niliambiwa nikabidhi ofisi na nimefanya hivyo. Sasa niko nje na sijui kinachoendelea,” alisema. Alipobanwa kueleza kilichosababisha asimamishwe kazi, Massawe alisisitiza, “siwezi kusema kwa sasa.”

Taarifa za suala hilo zilizopatikana baadaye wakati ufuatiliaji ulipoanza wiki kadhaa huko nyuma, zilisema mara baada ya Profesa Mbwette kuzungumza na mwandishi wiki iliyopita, aliitisha kikao ghafla cha wafanyakazi wote chuoni.

Ndani ya kikao hicho kilichofanyika 21 Februari 2012, imeelezwa kuwa Profesa Mbwette aling’akia wafanyakazi akilalamikia kiwango duni cha uwajibikaji.

Kawaida ya vikao vya kazi vya chuo hicho ni kuitishwa nyakati za jioni baada ya saa za kazi.

0
No votes yet