Wizi wa mabilioni BoT: Kikwete alidanganya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 September 2008

Printer-friendly version
RAIS  Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete hakuwa na haja ya kuunda Timu ya Kuchunguza Wizi wa fedha za EPA kwa kuwa anajua kilichotendeka, MwanaHALISI limegundua.

Mafaili ya Benki Kuu yamejaa mawasiliano juu ya udanganyifu mkubwa, hasa uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture ambayo pia yatakuwa mikononi mwa Timu yake.

Ni mawasiliano hayo ambayo yanafichua jinsi wakwapuaji walivyotumia Benki ya CRDB Limited kujinyakulia mabilioni ya shilingi, wakati mabenki mengine jijini Dar es Salaam yalikataa “ushirika” huo.

Mfano wa ukwapuaji ambao Rais Kikwete anapaswa kuwa anajua au atakuwa alielezwa na Timu yake, ni ule wa mabilioni ya shilingi yaliyochotwa na kamapuni ya Kagoda Agruculture.

Taarifa za ndani ya Timu ya Rais zinasema wajumbe wake, chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, nao wana nyaraka hizo nyeti na watakuwa wamezitumia kufanya kazi waliyotumwa na rais.

Kagoda ambayo inadaiwa kumilikiwa na mmoja wa viongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rostam Aziz, ilichotewa mabilioni ya shilingi hata kabla haijasajiliwa kama kampuni.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, uhusiano kati ya Kagoda na BoT ulianza mapema 2005 lakini mtiririko wa mawasiliano na shinikizo la kulipwa vinaanza kuonekana kuanzia 10 Septemba 2005.

Kwa mfano, aliyeitwa Meneja Mkuu wa Kagoda, John Kyomuhendo anaonekana akimwandikia Gavana wa BoT tarehe 7 Oktoba. Barua nyingine ya Kagoda, ikikumbushia nia ya kuhamisha fedha kutoka BoT iliandikwa tarehe 12 Septemba.

Naye gavana anajibu mawasiliano hayo kwa barua Kumb. Na. 6054/1355 ya 13 Oktoba 2005 inayofuatwa na barua ya Kagoda ya 20 Septemba ikielekeza uhamishaji wa fedha kwenda benki.

Maelekezo ni kwamba fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti Na. 01J021795700 iliyoko benki ya CRDB tawi la Holland jijini Dar es Salaam.

Barua kutoka Kagoda inayoelekeza jinsi ya kuhamisha zaidi ya Sh. 25 bilioni ilipokelewa na benki siku hiyohiyo ya 20 Oktoba 2005, kuwekwa katika faili na kupewa namba (folio) 7.

Wakati mawasiliano yote yakifanyika, ikiwa ni pamoja na kuchota mabilioni ya shilingi, Kagoda ilikuwa haijasajiliwa. Biashara ilikuwa “mali kauli,” kama ofisa mmoja wa BoT alivyolieleza gazeti hili.

Kagoda ilisajiliwa na Msajili wa Makampuni (sasa wakala wa usajili wa makampuni – BRELA) tarehe 29 Septemba 2005 na kupewa hati Na. 54040, huku wakiwa tayari wamekwapua mabilioni ya shilingi kwa kauli tu.

Pamoja na uhalifu huu wa wazi wa Kagoda, kwa kushirikiana na BoT, ambao ulifahamika kwa wajumbe wa Timu ya Rais na bila shaka kwa rais mwenyewe, Kikwete ameendelea kuwalinda mafisadi hao kwa madai ya kuwapa muda kurejesha fedha walizoiba.

“Kinachosikitisha ni kwamba rais alikuja bungeni; akajimung’unya na kutoa hadi 31 Oktoba mwaka huu walioiba wawe wamerejesha fedha hizo. Aliyegushi anapewa muda? Mhalifu wa aina ya Kagoda? Mwinzi mchafu analindwa?” ameuliza mbunge mmoja wa CCM Kanda ya Kaskazini.

Utapeli wa Kagoda unapamba moto baada ya kusajiliwa. Tarehe 24 Oktoba 2005 Kagoda inamwandikia gavana wa BoT kukumbushia uhamishaji wa fedha za makampuni mengine manane (8).

Katika muda wa chini ya saa 24 tangu kupokea barua ya ukumbusho, BoT inawaandikia Kagoda kwa kusema kuwa inathibitisha kuwapa Sh. 25,759,769,275.40. Barua hiyo ya 25 Oktoba, inasainiwa na Esther Komu wa Idara ya Menejimenti ya Madeni, Kurugenzi ya Sera ya Uchumi.

Makampuni hayo ni MIRRLEES BLACKSTONE Ltd, DAIMLER BENZ AG, LINDETEVES J. EXPORT BV, HOECHST, NS BOMA, SOCIETE GENERAL, PARTIZANSKI PUT na kampuni nyingine ambayo makubaliano yanaonyesha kusainiwa na Afriano Gardella S.P.A.

Kwa pamoja, makampuni hayo manane yalikwapua zaidi ya Sh. 20 bilioni.

Kwa mujibu wa barua ya Kagoda, ambayo nakala yake inapatikana katika faili la BoT  lililopewa folio Na. 24, benki inaelekezwa kupeleka fedha hizo katika akaunti Na. 01J1021795701 iliyoko tawi la Azikiwe la benki ya CRDB.

Kutumiwa kwa CRDB kupitisha fedha za EPA kumekuwa kukijadiliwa chinichini na benki hiyo haijawahi kukabiliwa na tuhuma za wazi za ama kushiriki au watu binafsi kuwa na mkono katika ukwapuaji wa fedha za umma.

Ni CRDB iliyoteuliwa na Kagoda kupeleka fedha zake katika matawi mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa barua Kumb. Na. 6054/1335/16 iliyokuwa inajibu barua ya benki ya siku hiyohiyo Kumb. Na. 6054/1335/15.

Matawi ya CRDB yaliyopewa jukumu la kupokea fedha hizo moja kwa moja kutoka BoT ni Vijana, Kijitonyama, Azikiwe, Holland na Tower yote ya Dar es Salaam.

Sh. 3, 430,099,403.52 zilipangwa kuhamishiwa Vijana, Akaunti Na. 01J1021795705 wakati Sh. 2,715,297,863.12 zilipangwa kuhamishiwa Akaunti Na. 01J1021795703 tawi la Kijitonyama.

Fedha nyingine Sh. 5,000,000,000 zilipangwa kupelekwa kwenye Akaunti Na. 01J1021795701 iliyoko Azikiwe.

Katika tawi la Holland zilipangwa kupelekwa Sh. 5,254,045,455.83 kwenye Akaunti Na. 01J1021795700 wakati Sh. 4,680,163,276 zilipangwa kupelekwa tawi la Tower kwenye akaunti Na. 01J1021795702.

Katika barua yake ya tarehe 1 Novemba 2005 yenye Kumb. Na. 6054/1335/29 kwenda kwa gavana wa BoT, ikijibu barua Kumb. Na 6054/1335/27 ya siku hiyohiyo, kupitia kwa mtu mmoja aliyeonyeshwa kwa jina  la I. Mwakosya, Kagoda inatoa maelekezo jinsi ya kutawanya fedha kutoka BoT.

Jumla ya Sh. 5,196,673,600.58 zilitakiwa kuhamishiwa matawi sita ya CRDB ya Vijana, Kijitonyama, Azikiwe, Holland, Tower na Lumumba. Katika tawi la Lumumba zilitakiwa kuingia kwenye Akaunti Na. 01J1021795704.

Wakati CRDB inapata “mteja mpya,” kuna mabenki ambayo yalionyesha kuwa makini zaidi kwa kutilia mashaka mteja huyo mpya. Kwa mfano, benki ya Barclays Tanzania Limited ya Dar es Salaam.

Barclays walikataa kufanya malipo ya Sh. 3,868,805,737.13 kwa kampuni ya Mibale Farm pamoja na kuhakikishiwa na Esther Komu na I. Mwakosya wa BoT kuwa malipo hayo kwa mteja ni halali.

Katika barua yao ya 2 Novemba 2005 ikijibu barua ya BoT Kumb. Na. 6054/1335/18 iliyopelekwa kwa njia ya fax, Mkurugenzi Mtendaji wa Barclays, Karl Stumke anasema kama ifuatavyo:

“Pamoja na uhalali wa fedha kuthibitishwa na ofisi yako, tumeamua kuacha akuendelea na mahusiano ya kibenki na mwenye akaunti hiyo.”

Utapeli wa Kagoda na washirika wake, ikiwa ni pamoja na wakwapuaji wengine, umepigiwa kelele na wananchi wakitaka serikali iwafikishe mahakamani.

Lakini rais Kikwete alipohutubia bunge 21 Agosti mwaka huu alisema anawapa wakwapuaji muda hadi Oktoba 31 wawe wamerejesha fedha walizoiba.

Upendeleo huo umechukuliwa kuwa ubaguzi unaovunja misingi ya katiba; kwani wanaoiba kuku na karanga wanafungwa, lakini walioiba mabilioni ya shilingi wanapewa muda kurejesha walichoiba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: