Ya Bashe, Kikwete, Masha na serikali ya gizani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Hussein Bashe

KITENDAWILI cha uraia wa Hussein Bashe, mgombea ubunge Nzega (CCM) aliyeenguliwa, kimeibua mapya.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurance Masha aliutangazia ulimwengu kuwa Bashe ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akahoji, “Nani mwenye mamlaka ya kusema Bashe si raia? Nikiwa waziri mwenye dhamana nasema, Bashe ni raia halali na hakuna atakayebadilisha uamuzi huu.”

Aliyesema kuna utata katika uraia wa Bashe, ni Rais Jakaya Kikwete, tena ndani ya vikao halali vya chama chake.

Taarifa zinasema, ndani ya ukumbi wa mkutano Kikwete alisimama kidete kutetea hoja yake kwamba Bashe si raia. Alisema amepata “taarifa za vyombo vya usalama,” zinazothibitisha utata wa uraia wa Bashe.

Wengine waliondeleza kauli ya rais, ni viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu Yusuf Makamba na Katibu Mwenezi John Chiligati.

Masha amenukuu vifungu kadhaa vya sheria ya uhamiaji akisema vinahalalisha uraia wa Bashe.

Kwa mfano, ananukuu vifungu Na.5 (1) na Na. 7 (8) vya Sheria Na. 7 ya uraia ya mwaka 1995 na kusema, “Bashe ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tena kwa kuzaliwa.” Anasema tayari amejulisha Bashe kuhusu uamuzi huo.

Je, Masha hakushauriana na Kikwete, Makamba na Chiligati kabla ya kutoa uamuzi waliofikia? Kama walishauriana, kwa nini wanaanika nguo za ndani hadharani?

Kama walishauriana, kipi kinachompa ujasiri Masha hadi kuamua kupigana na mwamba? Nani aliyemhakikishia usalama wake kisiasa na kimaslahi?

Akiongea kwa kujiamini, Masha alisema kwa mujibu wa nyaraka zilizopo na taarifa zilizofikia wizara yake, “…suala la uraia wa Bashe halina utata.”

Katika maelezo yake, Masha anasema Bashe ni raia halali wa Tanzania, tena kwa kuzaliwa. Hili nalo lina utata. Hata Bashe anajua hilo; kwamba si raia wa kuzaliwa.

Masha anajua kuwa wakati Bashe anazaliwa, baba yake mzazi alikuwa hajaomba uraia. Alikuwa raia wa Somalia. Alipoomba uraia wa Tanzania, hakumwingiza Bashe katika maombi aliyowasilisha katika fomu zake za kuomba uraia.

Aidha, Bashe mwenyewe amekana uraia wa Somalia akiwa na miaka 25.

Kama haya ndiyo maelezo ya Bashe, kwamba baba yake alipoomba uraia hakumuingiza yeye katika maombi yake; hiki ambacho Masha anaita, “Bashe raia wa kuzaliwa” kinatoka wapi? Kimelenga nini?

Kama Bashe hakuzaliwa Tanzania, na baba yake hakuzaliwa nchini na hata wakati baba anaomba uraia, Bashe akiwa na miaka kumi; nani basi rai wa kuzaliwa? Je, Masha amelenga nani na kwa faida ipi?

Kama Kikwete anasema Bashe si raia, huku Masha anasema tofauti, nani aaminike na yupi apuuzwe? Inawezekana Masha anajua vema nani anamtumikia, lakini siyo rais Jakaya Mrisho Kikwete na serikali yake.

Ingekuwa Masha anatumikia Kikwete, waziri na rais wasingepanda gari moja, lakini wakaelekea tofauti. Ama wotateremka na kila mmoja aende zake, au mmoja atabaki kwenye gari.

Lakini ukiyatafsiri vema haya utayafupisha kwa kauli hii: Kikwete ana serikali mbili. Zipi? Serikali anayozunguka nayo na nyingine iliyo kivulini.

Katika nchi zote ambako rushwa imekomaa na ufisadi umekuwa dini, dola linakuwa na sura mbili. Serikali mbili, mabunge mawili na mahakama mbili.

Kunakuwa na waasi wasioonekana kama majini ya Sheikh Yahya Hussein. Wanabaki kivulini.

Watatenda bila kuafikiana na wanaishi kwa kuviziana na kuzomeana. Hatimaye aliyeko kivulini anaangusha serikali iliyo wazi na iliyochaguliwa.

Wakati siyo rahisi kujua Masha yumo katika serikali ya dola lipi, katika hali ya kawaida, asingeweza kwenda kinyume na Kikwete, kama asingeweza kuwa na uhakika wa usalama wake kisiasa.

Sasa kuna wenye maoni kuwa hatua ya Masha “kumsafisha” Bashe imedhihirisha kuwa yeye na yule aliyemteua, wamo serikali tofauti. Hoja ni je, hali hiyo inavumilika? Nani atamvumilia mwenzake?

Hii ni kwa sababu, kama taarifa ambazo Kikwete alizikusanya zilikuwa na usahihi, lazima Masha angejua. Vinginevyo, Kikwete awe amekusanya taarifa zake kwa “njia za panya.”

Vilevile kama taarifa za Masha zingekuwa sahihi, hakukuwa na sababu ya kumiliki usahihi huo peke yake bila bosi wake kujua. Hali hii yaweza kuleta maana moja tu: kwamba mmoja wao anapokea taarifa za wapambe na huenda mitaani au zilizoandaliwa kwa nia mbaya.

Kama maelezo ya Masha ndiyo sahihi, nani aliyesababisha Kikwete kupeleka taarifa tofauti ndani ya vikao vya chama chake?
Taarifa ambazo rais alipeleka NEC na CC zimepitia kwa Masha? Je, waliomfikishia rais taarifa hizo walimueleza waziri kabla au baada ya kuzipeleka kwa rais?

Je, rais baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wandani wake alimpelekea waziri wake taarifa alizopata? Naye waziri alizihakiki na kuthibitishia rais kuwa taarifa alizonazo juu ya Bashe hazikuwa na chembe ya mashaka?

Je, inawezekana kila mmoja alificha taarifa zake ili aweze kumuumbua mwenzake katika vikao? Rais ana nafasi hiyo? Je, waziri ana fikra za kujiangamiza?

Ambayo hayakutendeka ndiyo yangeonyesha umakini wa serikali; uthabiti katika kufikia maamuzi na ufasaha wa taarifa.

Hayohayo ambayo hayakutendeka ndiyo yangeondoa kila chembe ya shaka na hata tuhuma za unafiki kutoka kwa wote wanaohusika. Hapa serikali ingeweza kuwa na hadhi mbele ya wananchi.

Kwa hali ilivyo sasa, Kikwete analazimika kutoka hadharani na kuseme haamini waziri wake, na kwamba kuwepo kwake serikalini kumetokana na shinikizo kutoka nje.

Lakini nani ataamini kuwa rais haamini waziri wake? Nani anaweza kuamini kuwa waziri wa mambo ya ndani – mjumbe katika vikao vya ulinzi na usalama – anakwenda kinyume cha aliyemteua?

Uamuzi wa Masha wa kujitosa kutetea Bashe, hata kwa kauli zenye utata, unachukuliwa na wengi kuwa njia ya kuonyesha kuwa ana msuli wa nje kuliko wa ndani ya serikali ya Kikwete.

Kwa upande mwingine, Bashe amenukuliwa akisema haivi na Ridhiwani, mtoto wa Kikwete. Hivyo inachukuliwa kuwa uamuzi wa Kikwete huenda ulilenga kumfurahisha mwanae.

Bali kuna hili pia: Masha si mjumbe wa vikao vya CC na NEC ambamo Kikwete alisimamia Bashe kuenguliwa. Hivyo, Masha hakupaswa kumuandikia barua Bashe.

Ingebidi kukiandikia chama chake na kumpa nakala Bashe. Badala yake, Masha amepeleka barua kwa Bashe na kunakiri barua yake hiyo kwa mtendaji mkuu wa chama, Makamba.

Itachukua muda, si mfupi, kujua chanzo cha purukushani hizi na tabia inayoelekeza mwenendo mzima ambao wengi wanaita sasa kuwa maasi ya ndani kwa ndani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: