Ya Dowans ni kashfa nyingine serikalini


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Edward Lowassa aliitenda upendeleo kampuni feki

HAKUNA ubishi kwamba uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), unaotaka serikali kulipa Dowans fidia ya Sh.185 bilioni, ni hujuma kwa taifa na kashfa nyingine ndani ya kashfa.

Tarehe 15 Novemba 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), iliagiza Shirika la umeme la Taifa (Tanesco) kuilipa kampuni ya Dowans fidia ya mabilioni hayo ya shilingi kwa kile kilichoitwa, “Kukiuka masharti ya mkataba.”

Katika kuonyesha kuna namna, hata baada ya kutangazwa hukumu, si serikali wala Tanesco walionyesha nia na shauku ya dhati ya kutaka kukata rufaa. Wanaoonekana kustuka ni watu wa kawaida wenye uchungu na nchi yao.

Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuwa serikali iko tayari kulipa fedha hizo.

Je, kama hiyo siyo njama, kwanini serikali imepatwa na kigugumizi cha kukata rufaa na kuzungumzia suala hili nyeti?

Kisheria hata kiakili ya kawaida, ujio wa Dowans Holding Tanzania Ltd., kurithi mkataba wa kampuni tata ya Richmond Development Company (RDC), unaacha maswali mengi yasiyo na majibu.

Hiini kwa sababu, kwa mujibu wa sheria, kila kitu kitokanacho na kitu kingine ambacho ni kinyume cha sheria, nacho ni kinyume cha sheria – batili.

Richmond iliyojifunga kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharula, ilithibitika kuwa kampuni isiyosajiliwa, isiyo na sifa wala uwezo kifedha na iliyopata mkataba kwa upendeleo.

Sasa, iwapo Richmond ni kampuni hewa, mahakama ya kimataifa ilikubali vipi madai ya Dowans?

Kinachoonekana hapa ni kimoja: Wanasheria wa serikali hawakueleza mahakama kwa ufasaha kilichotokea. Hawakusema kuwa Dowans imerithi mkataba wa kampuni feki.

Hawakujenga hoja imara kuwa kuhamisha mkataba toka kampuni tata ni kinyume cha sheria ya mikataba na jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Wala serikali haikusema kwamba wamiliki wa Dowans wamedanganya kwa kusema kampuni yao imesajiliwa nchini Costa Rica.

Kwamba hadi Dowans “wananunua” mkataba wa Richmond, hakukuwa na kampuni yenye jina hilo nchini humo. Huwezi kujadili yai bila kumjadili kuku.

Je, nani anaweza kuamini kuwa hizi si njama za kuhujumu taifa? Nani zaidi ya mwanasheria mkuu wa serikali wa wakati ule, Johnson Mwanyika anayepaswa kubebeshwa mzigo huu wa hujuma?

Yuko wapi wa kulaumiwa zaidi kama siyo rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete ambaye alishindwa kumwajibisha mwanasheria mkuu huyo hadi akastaafu na kukomba marupurupu yake na mafao lukuki?

Yuko wapi aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa ambaye amethibitika kuwa alitenda upendeleo kwa kulazimisha watendaji serikalini kuipa kazi kampuni feki?

Hata pale Kamati Teule ya Bunge ilipofumua siri zote zilizopo nyuma ya pazia na kugundua kuwa licha ya Richmond kuwa kampuni ya kitapeli ilingizwa kinyume cha sheria, serikali ilishindwa kuchukulia hatua Dowans na wanaojiita wamiliki wake.

Lakini kuna jingine. Kampuni iliyothibitika kuwa ni ya kitapeli, haikuomba kuhamisha mkataba wake. Wala haikutangaza zabuni ya kuhamisha mkataba.

Kama hayo hayakufanyika, hicho kinachoitwa, “haki ya Dowans” kinatoka wapi? Nani yuko nyuma ya kadhia hii?

Je, wataalamu wa sheria na upelelezi waliojaa serikalini wanalipwa kwa ajili gani iwapo kila siku tunaendelea kugeuzwa na mafisadi kichwa cha mwendawazimu?

Kwanini wahalifu wa Richmond waliachiwa waendelee kulihujumu taifa pamoja na ushahidi na wengine kukiri na kuwajibika kisiasa na si kisheria?

Tukubaliane. Tunahujumiwa na walewale tuliowaamini na kuwapa madaraka. Ingawa mzigo wa Richmond alibebeshwa Lowassa, kuna haja ya kuchimbua zaidi.

Kwa kuwa wakati wa mchakato wa kuleta Richmond, Kikwete aliwahi kuutaarifu umma kuwa anafuatilia mchakato mzima na hupewa taarifa ya kila kitu na waziri mkuu, maana yake ni kwamba kila alichofanya Lowassa kilikuwa na baraka za bosi wake.

Tusifike mahali wananchi wakakubaliana na madai ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyotoa 19 Julai 2009.

Akinukuu ripoti iliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, Lipumba alimtuhumu Kikwete kuwa mmoja wa wahusika wakuu katika kashfa ya Richmond.

Hadi leo hii, ikiwa takribani mwaka mmoja na ushei tangu kauli hiyo, si Rais Kikwete wala wasaidizi wake waliokana madai ya Profesa Lipumba.

Na hii haikuwa mara ya kwanza kwa Kikwete kuhusishwa kwenye kashfa ya Richmond pamoja na ile ya EPA na asikanushe wala kujitetea.

Je, hili lina maana gani? Mtu aweza pia kuuliza, “Hivi rais anajisikiaje anapoishi kimya katikati ya tuhuma nzito?” Hata mtangulizi wake, Benjamin Mkapa hajawahi kukana shutuma anazobebeshwa.

Ili taifa hili liweze kuwa na maendeleo, lazima tufike mahali tuache kulindana na kuogopana. Ama rais awajibike au awajibishe wenzake.

Kashfa hii mpya ya Dowans ifungue macho ya wananchi. Kashfa hii iwe fundisho kwa watawala wetu ili tusiruhusu watu wengine kuchuma kama taifa hili ni shamba la bibi.

Bahati mbaya kuliko yote, hakuna mwenye kujua ni mikataba mingapi iliyosukwa ki –Dowans, ili kukidhi matakwa ya wachache.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: