Ya Kikwete kama ya Mugabe?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Rais Kikwete na Rais Mugabe

YALIYOTOKEA Zimbabwe kwa Robert Mugabe na ZANU-PF, ni kama yale yanayotokea Tanzania kwa Jakaya Kikwete na CCM: Juhudi za kubaki madarakani “kwa gharama yoyote ile.”

Tujadili. Jeshi halina sababu wala uwezo wa kujitumbukiza katika siasa bila kuombwa, kushawishiwa au kuamriwa na watawala ambao wametokana na mchakato wa kisiasa.

Ikitokea askari hao wakajiingiza, sekunde hiyohiyo, watawala watapaza sauti – wakiwaambia wananchi waajiri wao; nchi jirani na jumuia ya kimataifa – kwamba demokrasi iko mashakani au imevamiwa au imeporwa.

Bali ikitokea watawala wakakaa kimya, juu ya vitisho vya wapiganaji; bila kukemea wala kuonyesha shaka; basi ujue askari hao, ama wameombwa au wamelazimishwa na wanasiasa walioko madarakani kuingilia mchakato wa siasa kwa manufaa yao.

Mnadhimu Mkuu wa JW, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, aliwaambia waandishi wa habari, Jumamosi iliyopita kuwa jijini Dar es Salaam, “kuna dalili za amani kuvunjika nchini” na kwamba vyombo vya ulinzi vimejipanga kukabiliana na hali hiyo.

Alisema wanavitaka vyama vya siasa na wananchi kukubali matokeo baada ya uchaguzi mkuu. Uchaguzi utafanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Tangu jeshi, lililokaa meza moja na polisi, litamke nia yao ya kuingilia mchakato wa uchaguzi kwa madai ya kulinda amani, serikali imekaa kimya.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo ilitakiwa kuwa imejiuzulu, kupisha askari na wana-usalama, hadi juzi Jumatatu ilikuwa haijasema lolote.

Serikali iliyokaa kimya ni ile inayoendelea kuongozwa na rais anayemaliza muda wake na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwa nini watawala wamekaa kimya? Vyombo vya silaha vinawasaidia au vinawatibulia utawala? Kama haviwasaidii mbona wamekaa kimya? Kama hawakuviita mbona hawaviambii vikae mbali?

Hivi nani ameripoti jeshini kwamba serikali ya kiraia inayoongozwa na Jakaya Kikwete imeshindwa kumudu utawala na kwamba ni askari wenye uwezo wa kuona “dalili za amani kuvunjika” na wenye kuzuia hali hiyo?

Katika demokrasi, serikali ikishindwa – kwa maana ya viongozi wa chama kinachopanga ikulu kushindwa kuongoza – wananchi huwatupa nje, tena kwa kishindo, kwa njia ya sanduku la kura.

Hayo hufanyika wakati washika silaha wakiwa pale – mbali – wakiangalia na kusubiri amri kutoka kwa utawala mpya.

Vipi leo mambo yawe kama ya Robert Mugabe wa Zimbabwe? Nchini Zimbawe, umaarufu wa Mugabe ulipauka. Thamani ya fedha yake ikaporomoka.

Si hayo tu. Chakula kikapotea majumbani na madukani. Migomo ya wafanyakazi ikauma. Askari wapigania uhuru wakazidisha madai ya kupewa ardhi. Rais akashindwa kulipa askari wanaostaafu.

Wakati huohuo chama cha Movement for Democratic Change (MDC) cha Morgan Tsvangirai kikawa kinapata nguvu na umaarufu wa kipekee.

Ni wakati huo pia, serikali iliogopa hata wafanyabiashara wadogo; na machinga waliswagwa na kuondolewa jijini Harare chini ya kilichoitwa “Operesheni Murambatsvina” – safisha jiji.

Ilikuwa katika hali hiyo, Mugabe alimwamuru mkuu wake wa shirika la kishushushu – Central Intelligence Organisation (CIO) ampe ushauri kuhusu uwezekano wake kushinda katika uchaguzi mkuu. Maoni ya mkuu huyo wa CIO kuhusu upepo wa kisiasa, ndiyo yalimfukuzisha kazi. Alimwambia Mugabe kuwa ni vigumu kushinda.

Bali hata baada ya kumfukuza bosi wa mashushushu wake, Mugabe aliamua kukabidhi sehemu muhimu ya madaraka yake kwa maofisa wa shirika la usalama – CIO.

Mugabe alitaka kutumia wana-usalama kubaki madarakani hata kama wananchi wamemchoka na wanataka mabadiliko. Alifanya hivyo.

Knox Chitiyo, Mzimbabwe mtafiti, mkuu wa Taasisi ya Ulinzi na Usalama kuhusu Afrika, mjini London, Uingereza anasema, “Kanuni ya kwanza ya kubaki salama ni kuweka majeshi ya usalama katika hali ya furaha wakati wote na kuwalipa.”

Yote haya yalikuwa na maana moja. Utawala umeshindwa. Nchi haitawaliki na uchaguzi unotarajiwa huenda ukamtupa nje Mugabe.

Wakuu wa usalama, katika idara mbalimbali wakawa wanaripoti moja kwa moja kwa rais. Wana-usalama, askari jeshi, polisi na vijana wa chama – Green Guards – wakaanza vitisho, kukamata, kupiga, kufunga na hata kupoteza baadhi ya wapinzani na mashabiki wao.

Mashushushu waliwekwa katika mtandao maalum uliopenyeza maajenti katika MDC, vyama vingine vya siasa, taasisi na asasi za serikali na binafsi na kueneza woga.

Hata hivyo, pamoja na ubabe huo, Mugabe hakuona ndani katika uchaguzi mkuu wa 2008.

Mashushushu wake, waliokuwa wamepandikizwa katika Tume ya Uchaguzi walifaulu kuchakachua takwimu ili kuonyesha kuwa kati ya yeye na Tsvangirai, hakuna aliyefikia kiwango cha kuwa mshindi.

Ni mashushushu wake, askari wa jeshi, polisi, green guards na mgambo walioendesha vitisho muda wote kuelekea marudio ya uchaguzi na hatimaye tume kumtangaza kuwa mshindi – rais.

Hapo ndipo wachunguzi wanajiuliza kama yaliyotokea Zimbabwe hayatatokea Tanzania, hasa kufuatia jeshi kutangaza “kushughulikia watakaopinga matokeo ya uchaguzi” ambao haujafanyika.

Kwanza, kauli ya jeshi ya aina hii, katika kipindi hiki na wakati wowote ule, inachukuliwa kuwa, na hasa ndivyo ilivyo, vitisho.

Shimbo, msemaji wa “vyombo vya ulinzi,” anasema vimejipanga kuhakikisha kuwa damu haimwagiki wakati na baada ya uchaguzi.

Anataka vyombo vya habari vichuje habari. Anataka asasi za kijamii zinazotoa elimu ya uraia, zitoe “elimu tu.” Haifahamiki zilikuwa zinatoa kitu gani kingine. Anataka wananchi na vyama vya siasa kukubali matokeo.

Kwa kuzingatia kimya cha serikali tangu Jumamosi iliyopita, hatua ya jeshi itakuwa imetokana na taarifa za wapelelezi na “wana-usalama” wa CCM na serikali.

Taarifa hizo juu ya mwenendo wa kampeni, uwezekano wa kushindwa kwa chama kinachopanga ikulu na hata mgombea wake; na mwonekano wa jumla wa kukubalika kwa upinzani, ndivyo vimeleta kiwewe na woga ndani ya CCM.

Hakika uchaguzi mwaka huu unafanyika katika mazingira ambamo hoja kuu zina mguso kwa wananchi na kuna wanasiasa mahiri wa kuzifafanua.

Mikutano imekuwa madarasa – mahali pa kuelezea kiini cha umasikini wa Tanzania; masuala ya utawala bora, hasa mapambano dhidi ya wizi, rushwa na ufisadi. Hoja zilizosheheni mifano halisi, ushahidi na zisizopingika.

Umuhimu wa katiba mpya, elimu na afya vimepewa nafasi kubwa; ajira na mafao ya wafanyakazi na wastaafu, na uhuru wa wananchi kuwa na kauli juu ya mambo yanayowahusu, vimezingatiwa.

Hizi, pamoja na nyingine, ni hoja zinazoshikika; zinazoelezeka na kugusa. Ni hoja zinazotishia wapangaji wa ikulu, kuwatetemesha na kuleta kiwewe kiasi cha kuomba msaada, hata wa mabavu.

Kauli za jeshi haziwezi kuzima haya. Kama ilivyo siku zote katika nchi ambako chama kimoja kimetawala kwa miaka nendarudi – kama hapa, miaka 50 – kutoweka kwa amani huletwa na walioko madarakani ambao hawapendi kuona wanashindwa.

Nchini Zimbabwe, baada ya vyombo vya ulinzi kuingia katika siasa, vilianza kumeguka. Yalizaliwa makundi. Yalitiliana shaka. Yakajenga kutoelewana na uhasama. Yakawa katili zaidi kwa wananchi. Yakachukiwa hadi leo.

Ni Profesa Wole Soyinka wa Nigeria aliyewahi kusema kuwa, kama watawala wa kiraia wanataka kutawala kwa mabavu, ni afadhali wakabidhi utawala kwa jeshi lililojifunza ubabe.

Na ubabe hauwezi kutawala. Labda ndiyo maana hata siku ya kutangaza majeshi kuingilia mchakato wa uchaguzi, timu ya wakuu jeshini haikutimia.

Kulikuwa na Luteni Jenerali Shimbo – hakukuwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange. Kulikuwa na Kamanda wa Kikosi cha Operesheni Maalum cha Jeshi la Polisi, Venance Tossi – hakukuwa na Inspekta Jenerali Saidi Mwema
Kulikuwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo – hakukuwa na Mkurugenzi wa Upelelezi, Robert Manumba.

Tunasubiri operesheni isiyokubalika. Bali kwa upande wa vyombo vya habari, ambavyo viliamriwa kuchuja habari zake, naweza kuvisemea:
Kwamba vyombo vya habari vikinyamaza – likawa giza la habari – ukweli au uongo havitafahamika. Uhuru utapokonywa. Haki itatoweka. Shaka, woga na kimya – vipitao ukimya wa mauti vitatawala. Tutaishi kama wafu. Hili halikubaliki.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: