Ya Lembeli yamkuta Pinda


Igenga Mtatiro's picture

Na Igenga Mtatiro - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version

WALE waliosikitishwa na hatua ya kampuni ya African Barrick Gold kukodi ndege tatu kwa ajili ya wabunge wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bunge kwenda North Mara kuikagua kampuni hiyo Agosti mwaka huu, waliharakisha mno kutoa lawama zao.

Barrick walisubiri kufanya tukio jingine kubwa zaidi ya hilo; kuuweka mfukoni muhimili wa dola. Waziri mkuu Mizengo Peter Pinda ndiye aliyenasa katika mtego huo,  msafara mzima uliingia mgodini kula chakula cha mchana na kugharimiwa mafuta.

Ilikuwa hivi. Mwishoni mwa mwezi uliopita Pinda alifanya ziara katika mkoa wa Mara na tarehe 21 Septemba 2011 alikutana na wananchi wa Nyamongo yaliko machimbo ya madini ya dhahabu katika mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Barrick.

Wananchi walifurika kwanza kumsikiliza na kupokea ujumbe aliowapelekea, na pili kumkabidhi malalamiko au shida zao kongwe na ambazo viongozi wote wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakikwepa kutolea ufumbuzi – mgogoro wao dhidi ya kampuni ya Barrick inayochimba madini ya dhahabu katika mgodi wa North Mara.

Kabla ya Pinda kupanda jukwaani kuhutubia wananchi wa kata hizo katika kijiji cha Kerende mchana huo, walimsomea risala iliyoandaliwa na kata hizo.

Katika risala yao, wananchi walitaka Waziri mkuu Pinda atolee tamko kuhusu uhusiano mbaya kati ya mgodi huo na majirani zake wa vijiji saba vinavyouzunguka mgodi huo unaosababisha kuzuka kwa mauaji ya watu kadha wa kadha.

Mfano uliohai ni tukio la kuuawa kwa watu watano na wengine watatu kujeruhiwa 16 Mei 2011 baada ya polisi kudai kundi la watu zaidi ya 1500 walitaka kuingia mgodini kwa lengo la kuiba na kupora madini.

Vilevile, wananchi walitaka Pinda atolee tamko hatima ya wachimbaji wadogo wadogo 362 waliohamishwa na mashimo yao kuchukuliwa na Barrick katika eneo lililofahamika kama Nyarugusu.

Risala ilionesha wachimbaji hao, wakiongozwa na Juma Kirigiti wanaidai kampuni hiyo mapunjo ya Sh. 43 bilioni baada ya awali kufidiwa viwango walivyodai havistahili.

Walidai katika risala hiyo kwamba baada ya kuona kuwa hawatekelezewi madai yao, waliamua kumwona kamishina wa madini Peter Kafumu. Hawakufanikiwa.

Baada ya njia zote hizo kushindikana, wananchi hao hawakuwa na uamuzi mwingine isipokuwa kukimbilia mahakamani ambako walifungua kesi Na 39 ya mwaka 2011 katika mahakama ya rufaa jijini Mwanza. Mashimo yao yalichukuliwa na mwekezaji huyo mwaka 1996.

Majibu mengine waliyosubiri kutoka kwa Waziri mkuu ni hatua za kuwachukulia wote waliohusika na ufisadi wa malipo ya fedha kwa ajili ya fidia kwa wananchi ambao maeneo yao ya ardhi ya kilimo na makazi ambayo yalichukuliwa kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa madini.

Shauku yao iliwatumbukia nyongo. Kwanza Waziri Mkuu Pinda hakujibu ipasavyo risala yao, lakini pili hakutoa fursa ya kuuliza maswali.

Baada ya kutoa hotuba yake huku akikwepa kuingia kwenye mtego wa kujibu hoja zao, msafara wake ulielekea mgodini North Mara hali ambayo wananchi waliona ni usaliti mkubwa.

Msafara huo ambao miongoni mwao ni waandishi wa habari, uliingia kwenye mgodi huo unaolalamikiwa na wananchi kwa ajili ya chakula cha mchana na kujaziwa mafuta magari. Barrick waligharimia msafara huo wa watu takriban 40.

Mtu pekee aliyekwepa mtego huo ni Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Esther Nicolous Matiko.

Hii ni mara ya pili katika miezi michache mgodi huo wa North Mara kuwakirimu viongozi. Agosti mwaka huu, mgodi huo ulikodi ndege tatu kwa ajili ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bunge chini ya mwenyekiti wake James Lembeli.

Ziara hiyo iliyogharimiwa na Barrick ni ili wawakilishi hao wa wananchi wakakague miundombinu ya uhifadhi wa maji yenye sumu.

Mei mwaka 2009 maji yenye sumu yalikuwa yanatiririka na kuingia katika Mto Tigithe na kusababisha madhara makubwa. Mifugo ilikufa na watu walibabuka ngozi miguuni na midomoni.

Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bung echini ya mwenyekiti wake Job Ndugai (sasa Naibu Spika wa Bunge) ilikwenda kushuhudia uchafuzi huo na iliagiza mgodi ujenge haraka mabwawa ya kuhifadhi maji yenye sumu.

Mbali ya kutoa maagizo hayo kamati hiyo iliyoongozana na wataalamu mbalimbali iliagiza wachukue sampuli ya damu na maelezo ya walioathirika. Serikali imegoma hadi leo kutoa taarifa kuhusu kiwango cha madhara waliyopata wananchi.

Barrick imewachukua hadi Agosti mwaka huu kujenga mabwawa hayo na ndipo ikakodi ndege za kuchukua wabunge wa kuikagua.

Ofa hiyo ilizua maswali mengi kwa Watanzania wengi kuhoji, kampuni hiyo inawezaje kukodi ndege kwa ajili ya wabunge wa kwenda kuikagua? Mbunge wa Tarime Nyambari Chacha Nyangwine (CCM) alikwepa mtego huo, akagoma kupanda ndege.

Kama mihimili miwili – dola na Bunge – imefunikwa na ofa ya Barrick, nani atasikiliza na kutatua malalamiko ya wananchi? Wanyamongo watawaheshimu vipi viongozi walioko madarakani kwa mtindo huu?

Kwa upande wake Esther alisema pamoja na kushiriki kikamilifu katika ziara ya Pinda, anamsubiri bungeniDodoma .

Akasema, “Waziri mkuu  Pinda alishindwa kutoa kauli juu ya changamoto zilizopo kwa wananchi wa vijiji vya mgodi wa North Mara, licha ya kusomewa risala na kupewa. Badala yake aliona inafaa kwenda na msafara wake kula mgodini na magari ya msafara huo kunyweshwa mafuta.”

“Hii ni aibu kubwa. Kilichoshangaza zaidi ni kwamba Waziri mkuu hakuona haja hata ya hakufika kuipa pole familia ya mwanafunzi aliyekanyagwa na dampa Na 25 la Barrick,” alisisitiza.

Siku moja kabla ya Waziri mkuu Pinda, kuwasili wilayani Tarime kwa ziara ya kiserikali mwanafunzi wa kidato cha IV katika shule ya sekondari ya Ingwe, Range Robert alikanyagwa na dampa na kufariki dunia wakati akitokea kwenye mahafali yake ya kuhitimu elimu ya sekondari.

Pinda alifunga ziara eneo la Nyamongo akaenda Sirari akiwaacha wenyeji wake hoi.

0
No votes yet