Ya Mdee, Londa na Makamba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Halima Mdee

KESI ya aina yake inarindima. Inahusu makada wawili mashuhuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu, Yusuph Makamba na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Salum Londa.

Inasikilizwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Mwenyekiti wa Kamati hii ni Anne Kilango Malecela.

Makamba na Londa wamemshitaki mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Halima Mdee, kwa madai kwamba amewakashifu na kuwadhalilisha. Londa ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Wajumbe wengine wa Kamati ni Christopher ole Sendeka (Simanjiro), Ali Ameir Mohammed (Donge –Unguja), Abdulkarim Shaha (Mafia).

Wengine ni William Kusila (Bahi), Charles Keenja (Ubungo), Fatma Fereji (Baraza la Wawakilishi), Maulida Komu (Viti Maalum-CHADEMA) na Fatuma Maghimbi (Chakechake-Pemba).

Malalamiko ya Londa na Makamba yanatokana na kauli ya Mdee bungeni mwaka jana, akimtuhumu Makamba “kumlinda” Meya Londa, ambaye alisema anatuhumiwa kwa ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na uuzaji wa viwanja maeneo ya Kawe, Kinondoni.

Kwa mujibu wa maoni ya baadhi ya wabunge, kesi hii yaweza kuleta mtikisiko wa aina yake unaoweza kulingana na kimbunga cha Richmond.

Sakata la Richmond lililofikia kilele Februari mwaka jana, ndilo lilimng’oa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Taarifa za ndani ya kikao zinasema utetezi wa Mdee, uliowasilishwa Ijumaa kwa kutumia nyaraka mbalimbali, ulimstua Meya Londa kiasi cha kuomba muda wa kutosha kupitia nyaraka hizo ili aweze kujenga misingi ya malalamiko yake.

Kilichomstua zaidi Londa, diwani wa Kawe, ni kukuta mwanachama wa chama cha upinzani akiwa na nyaraka za vikao vya ndani vya CCM vilivyomjadili yeye.

Mmoja wa walalamikaji, Yusuf Makamba aliyetakiwa kuwa mbele ya Kamati ya Bunge, hajawahi kuhudhuria vikao vya kamati. Hivi sasa anazunguka mikoani kwa “shughuli za chama.”

Mara baada ya Mdee kuwasilisha nyaraka, wajumbe wote walionekana kushangazwa na nyaraka za vikao vya CCM, zimeeleza taarifa za ndani ya kikao.

Baadhi ya nyaraka ambazo Mdee amewasilisha na kufanya wajumbe wabatuke nywele kichwani ni pamoja na Muhtasari wa Kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam cha 20 Mei 2008; Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM ya Mkoa; na Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni ya 15 Machi 2008.

Kamati zote zilikuwa zikishughulikia kile kilichoitwa “mgogoro wa madiwani wa manispaa ya Kinondoni dhidi ya Meya Londa, kwa kumhusisha na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma, uongozi mbaya na kuleta mpasuko miongoni mwa madiwani.”

Taarifa za ndani zinasema Londa ameegemea sana maelezo yanayoonyesha kumnyooshea kidole aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Hawa Ngulume. Hiyo ni katika uuzaji kinyemela wa uwanja wa shule unaotajwa kunufaisha viongozi waandamizi wa manispaa kwa zaidi ya Sh. 130 milioni. Ngulume sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali.

Mara kadhaa, kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia MwanaHALISI, Londa alikuwa akijitetea kwa kusema yeye ni mwanasiasa ambaye hawezi kujibu hoja za kiutendaji kwa kuwa waliohusika zaidi na jukumu la kiutawala, ni maofisa wa Manispaa.

Londa aliruhusiwa kupata muda wa kupitia nyaraka alizowasilisha Mdee na baadaye amhoji.

Mwaka 2006, Manispaa ya Kinondoni ilimpa mwekezaji wa kampuni ya ISHIK, inayomilikiwa na wageni kutoka Arabuni, uwanja wa shule ya msingi ya Kawe kwa ajili ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 na Sheria ya Uwekezaji ya 1997, mwekezaji anatakiwa kuomba kibali cha miliki ya ardhi kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), vinginevyo miliki yake inakuwa batili.

Kumbukumbu za bunge zinaonyesha Mdee alisema Manisapaa ya Kinondoni iligawa uwanja wa shule kwa maamuzi yaliyopitishwa na vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata, hatua isiyokubalika kwa kuwa baadhi ya wajumbe katika kamati hiyo hawatambuliwi kisheria.

Hii ni kulingana na kifungu Na. 6 cha Sheria Na. 6 ya mwaka 1999; kifungu 31 cha Sheria Na. 7 na kifungu cha 15 cha Sheria Na. 8 ya mwaka 1982.

Kwa kuangalia makubaliano ya kugawa uwanja wa shule (MoU) kati ya Manispaa na mwekezaji huyo, inaonyeshwa iliafikiwa 19 Januari 2006, lakini nyaraka za manispaa zimeonyesha makubaliano hayo yalisainiwa 17 Januari mwaka huo.

Makubaliano hayo yalibainisha kuwa wakati mwekezaji atapata uwanja wa kuendesha mradi wake na manispaa itanufaika kwa kujengewa madarasa manne, mashimo sita ya vyoo na maabara.

Kashfa ya uuzaji uwanja wa shule ilisababisha CCM kuingilia kati kwa kuitisha vikao vya Kamati ya Siasa ya Wilaya na Mkoa ili kujadili hatima ya tuhuma za ufisadi zilizomkabili Londa.

Hata hivyo, pamoja na tuhuma nyingi kuthibitika kuwaandama viongozi wa manispaa, hakuna kiongozi yeyote aliyechukuliwa hatua za kinidhamu.

Suala hilo lilipofika ngazi ya juu ya CCM, Londa alisalimika kutokana na kile kilichoelezwa na baadhi ya viongozi kuwa ni kukingiwa kifua na Makamba.

Maamuzi ya kumlinda Londa yalisikitisha wajumbe wengi na baadhi yao kusikika wakisema kwa utaratibu huo, CCM inafanya mzaha mtupu inapojieleza kwa umma kuwa inapiga vita ufisadi wakati kivitendo inalinda mafisadi.

Malalamiko ya Makamba ni kwamba anatuhumiwa “kumlinda” Londa. Lakini uelewa wa viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ni kwamba ni Makamba aliyempa tafu Londa hadi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

MwanaHALISI ina taarifa kwamba Makamba, wakati mzozo ukifukuta kwelikweli, alimtaka Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, kuingilia kati, lakini rais alisema, “…hilo la kwenu; limalizeni wenyewe.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: