Ya nini ajizi? Mzanzibari sema NDIYO


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

JUMAMOSI hii – tarehe 31 Julai, siku tatu zijazo – ndiyo siku ya uamuzi kuhusu mustakabali wa Zanzibar na Wazanzibari wenyewe.

Hiyo ndiyo siku kwa kila mwananchi kupiga kura ya NDIYO kwenye kisanduku cha kura ya maoni ili kuyapa nguvu maridhiano yaliyoanzishwa na viongozi wetu wakuu katika siasa Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF).

Hiyo ndiyo siku tunayopaswa kuitumia vizuri nafasi yetu ya haki kwa kusema NDIYO.

Ni siku ambayo Wazanzibari walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar, wanatumia haki ya kikatiba kufanya uamuzi kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa kiutawala katika nchi yao.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kutokana na maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, imeandaa swali kwa kila mpiga kura.

Swali lenyewe ni “Je unakubali au unakataa mabadiliko ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa?” Kwenye karatasi hiyo ya kura, kuna visanduku viwili; kimoja kinabeba neno NDIYO na kingine kina neno HAPANA.

Mpiga kura akitia alama yake kwenye kisanduku cha NDIYO ina maana amekubali mabadiliko yanayopendekezwa na serikali, na akitia alama yake kwenye kisanduku kingine ina maana amekataa mapendekezo hayo.

Nini maana ya kukubali mabadiliko? Na nini maana ya kuyakataa?

Pale kura ya NDIYO itakaposhinda, maana yake wapiga kura walio wengi wameridhia matumaini ya serikali kuandaa muswada wa mabadiliko ya katiba ili kuruhusu kuja kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa mara baada ya uchaguzi mkuu.

Serikali hiyo itakuwa na utaratibu mpya wa kiutawala utakaoanza kutumika Zanzibar katika miaka hii ya milenia. Ni matumaini ya wataalamu wa masuala ya kisiasa kwamba serikali hiyo itakuwa ufumbuzi wa mivutano ya kisiasa inayozidi kuisumbua nchi kwa miaka mingi sasa kila unapofanyika uchaguzi tangu mwaka 1995.

Kuja kwa mfumo huo kutakuwa na maana ya kufutwa ule utaratibu uliozoeleka wa kukiruhusu chama kinachoshinda kura ya urais kuunda serikali peke yake. Kwa utaratibu huu mpya kikatiba ni kuwa mgombea aliyeshinda ataunda serikali kwa kushirikisha wajumbe wa vyama vingine – yaweza kuwa kimoja au zaidi – vitavyokuwa vimepata kura kwa asilimia itakayobainishwa katika Katiba.

Na hayo ndiyo hasa mabadiliko ya mfumo wa utawala yanayotakiwa Zanzibar kwa zama hizi ikiaminika kuwa ndilo suluhusisho la mgogoro usiokwisha wa kisiasa ambao umeinyima Zanzibar nafasi muhimu ya kupata maendeleo makubwa kiuchumi na kijamii.

Lakini iwapo HAPANA itashinda, maana yake serikali haitalazimika kupeleka katika Baraza la Wawakilishi mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya kuruhusu mfumo mpya. Kwa maana ya kikatiba, Zanzibar itaendelea na utaratibu uliopo wa chama kinachoshinda urais kuunda serikali peke yake.

Mfumo huu, kulingana na wataalamu wa masuala ya sayansi jamii na utawala, umekuwa ukitumiwa vibaya kuzidisha mgogoro. Wanasema mahali penye migogoro ya kisiasa inayotokana na uchaguzi, serikali kama hii ya Umoja wa Kitaifa huwa njia nzuri ya kufikia ufumbuzi.

Mapema mwaka huu, Baraza la Wawakilishi liliidhinisha hatua za kufanywa na serikali ili kufikia kuwepo mfumo wa kuundwa kwa serikali ya aina hii. Serikali imetekeleza hatua kadhaa, na sasa ni wakati wa wananchi kufanya uamuzi. Wanataka kubadilisha mfumo au wanataka kubaki na mfumo uliopo.

Imekuwa matumaini ya kila mwananchi kwamba kwa kuwa serikali yenyewe, inayoongozwa na CCM, ndiyo iliyopeleka muswada wa sheria barazani, inawajibika kuipigia kampeni ili iweze kutengeneza utaratibu wa kuwepo serikali hiyo baada ya uchaguzi.

Chochote kinachokubalika na serikali kufanyika, huwa kimepata idhini ya CCM, chama kinachoongoza dola. Kwa hivyo basi, imani ya wengi ni kwamba CCM inaridhia hilo.

Hata hivyo, kumekuwa na mgawanyiko ndani ya serikali kama ambao upo ndani ya CCM yenyewe. Wapo mawaziri katika serikali na watendaji katika CCM wasiounga mkono mwelekeo huo. Hao ndio wanapiga kampeni ushindwe.

Baadhi ya viongozi wa CCM wanajulikana walivyoshiriki kuhamasisha wananchi kwenye majimbo wakatae dhamira ya chama chao kwa kupinga maridhiano.

Rais Karume analijua hilo. Amekuwa akiwasema na kuwashangaa. Anahoji wanataka nini zaidi ya kuzungumzia njia za kuimarisha umoja na mshikamano katika nchi, pamoja na kuridhia mwelekeo wa maendeleo yanayoshirikisha kila mtu?

Anauliza, “hivi hawaoni (hao viongozi wenzake) namna wananchi walivyoamua kupendana na kushirikiana katika shughuli za kijamii bila ya kuzingatia itikadi za vyama vyao tangu tulipoanza kufikia maridhiano?”

Ukweli, wananchi wengi wameamua kubadilisha mfumo wa utawala. Uchunguzi uliofanyika kwa siku kadhaa unathibitisha kuwa watu wamechoka kugombana kwa sababu ya siasa; sasa wanataka kuishi kwa amani na kushirikiana na serikali ili kuijenga nchi yao.

Rais Karume anataka maridhiano maana ndivyo kinavyoamini chama anachokiongoza kwa Zanzibar. Anafuata msimamo wa bosi wake, Jakaya Kikwete anayeeleza wazi kuwa chaguo la CCM ni kuridhia kura ya maoni ili kumaliza tatizo la “mpasuko wa Zanzibar.”

Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM kitaifa. Lakini pia ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliwaahidi Wazanzibari, Watanzania na jumuiya ya kimataifa, tangu 30 Desemba 2005, kuwa atahakikisha anatafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la Zanzibar.

Na msimamo huu tayari unaelezwa na mgombea wa CCM katika kiti cha urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. Alisikika kabla ya kuteuliwa na chama chake na anaendeleza ajenda hii baada ya kuidhinishwa.

Sasa rais wa jamhuri anaridhia. Wa Zanzibar nao wanaridhia. Mgombea urais Zanzibar kupitia chama hicho pia anaridhia. Nani anapinga, halafu yeye abakie mwenye hekima na busara zaidi kiuongozi?

Ninaamini kwa msimamo huohuo, ndio maana viongozi wa CCM wanaohimiza wananchi wa Unguja na Pemba wapige kura ya NDIYO hapo Jumamosi, wameongezeka.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, ameshatamka hadharani kuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika CCM na Baraza la Wawakilishi, ambalo ni mhimili mmojawapo wa ile mitatu ya dola, anachagua maridhiano na wananchi wapige kura ya NDIYO.

Mihimili miwili – serikali na baraza – inaongozwa na wanasiasa, bali wa tatu, Mahakama, unaongozwa na mtaalamu wa sheria kwa jina la Jaji Mkuu. Huyu kikatiba hapaswi kushabikia siasa za vyama.

Tayari vyama vilivyo nje ya serikali, vimetangaza kuunga mkono kura ya maoni na vimekuwa vikihimiza wanachama wao pamoja na wananchi wengine wapige kura ya NDIYO.

Chama kikuu, CUF, kinajulikana kilivyo mstari wa mbele katika ajenda hii. Maalim Seif, Katibu Mkuu wake, amekuwa akihutubia mikutano ya hadhara kushajiisha wananchi kupiga kura ya NDIYO.

Niulize, hivi kama viongozi wakuu wa CCM wanaridhia; kama viongozi wakuu wa mihimili ya kisiasa wanaridhia; na viongozi wa vyama shindani wanaridhia, tumpe jina gani anayepinga maridhiano?

Sote tukisema NDIYO tutakuwa tumeidhinisha mabadiliko Zanzibar; kazi itabaki kwa serikali kukamilisha utaratibu wa kikatiba kuwezesha serikali ya umoja wa kitaifa kuundwa baada ya uchaguzi mkuu.

Nasaha: Kupiga kura ya NDIYO, maana yake ni kusema hapana kwa magomvi, chuki na visasi. Ni kusema ndio kwa umoja, maelewano na maendeleo ya kweli kwenye nchi yetu.
Tuchague maridhiano!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: