Ya Nixon kuikumba Ikulu ya Dar?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

SERIKALI haikutoa tamko kulaani au kusikitishwa na tukio lile, kampuni za simu za mkononi nazo zilikaa kimya, na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) haikuwa na jibu.

Lakini wote walitumiwa ujumbe kupitia kwenye simu uliobeba kashfa dhidi ya mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Salaa.

Ujumbe huo uliotumwa kupitia Na. +3588976578 na Na. +3588108226 ulisema Dk. Slaa ni “mropokaji” anayelumbana na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi.

Kwa wakati ule TCRA ililazimika kukaa kimya ili isiwaumbue wakubwa. Ingefuatilia namba ile kama ilivyowaahidi Watanzania wakati wa kusajili namba za simu, wakubwa wa serikali wangeumbuka.

Sasa kwa kuwa uchaguzi umepita, TCRA itueleze kama imefuatilia uhalifu huo maana lengo la kusajili namba ni kudhibiti uahalifu. Uhalifu huo ni pamoja na kutukana, kupanga wizi au hujuma.

Je, TCRA bado haijaona kwamba ujumbe ule ilikuwa hujuma dhidi ya Dk. Slaa? Kwa hiyo, kama hata baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutolewa bado TCRA haitaki kueleza kilichotokea, moja kwa moja wananchi tutaihusisha na hujuma hiyo.

Sawa. Hata kama TCRA itaamua kufutika kaa hilo la moto, muda wa kuumbuka unawadia hasa baada ya ikulu nayo kuhusika katika kashfa nyingine ya kulipia tangazo kwenye gazeti la serikali linalomkashfu Dk. Slaa.

Kama ikulu inajua basi ‘aliyepangishwa’ katika jengo hilo miaka mitano iliyopita yaani rais anajua. Je, mtoto anaweza kufanya uchawi ndani ya nyumba baba asijue? Je, mtoto akitukana watu njiani, baba hatawajibika kwa madhara yote yatokanayo na matusi hayo?

Kwa kawaida, baba atawajibika kulipa gharama zote ikiwa mtoto atakuwa amesababisha hasara kwa majirani zake. Baada ya hapo baba atabaki akitafuta njia za kumkanya na kumrudi mwanaye.

Lakini kwa nini urais iwe kwa gharama ya kukashfu wapinzani? Kuna raha gani kuwa rais kwa gharama ya kashfa?

Tukio hili, halina tofauti sana na ilivyotokea Marekani mwanzoni mwa miaka ya 1970 enzi za utawala wa Richard Nixon wa Republican.

Juni 17, 1972 Nixon aliyekuwa anahaha kupata kurejea madarakani kipindi cha pili alijikuta kwenye kashfa baada ya kuhusika kufunika na kuwalinda waliovunja na kuiba siri kwa wapinzani wake.

Tukio hilo lililokuja kubatizwa baadaye kama kashfa ya Watergate lilijulikana baada ya watu watano kunaswa kwa tuhuma za kuingia kijasusi kupata siri kwenye makao makuu ya ofisi za Democratic zilizoko Hoteli ya Watergate, Washington, D.C.

Uchunguzi wa awali wa gazeti la The Washington Post lililopelekewa taarifa kwa siri na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ulionyesha watu hao wanahusishwa na ikulu ya White House.

Hii ilitokana na ukweli kwamba katika kashfa hiyo kamati ya uchaguzi ya Nixon ilihusika.

Kama kawaida ya viongozi wengi, Nixon alitupilia mbali habari hizo akidai kuwa ni propaganda za kisiasa tu na ikulu ilikanusha vikali ikidai ni habari za upande mmoja na za kupotosha.

Lakini baadaye FBI ilithibitisha pasina shaka kwamba wasaidizi wa Nixon walijaribu kuihujumu Democrats na baadhi yao wakaanza kujiuzulu. Mnikulu alishtakiwa katika kashfa hiyo hali iliyomweka pabaya Nixon.

Nixon aliwekwa katika wakati mgumu bada ya hati ya kiapo ya John Dean kuonyesha rais huyo alihusika na Alexander Butterfield alionyesha katika kiapo kuwa Nixon alikuwa na mfumo wa kurekodi mazungumzo ya simu ndani ya ofisi maarufu kama Oval Office.

Kesi ikanguruma, ushahidi ukatolewa na baadaye Aprili 1974, Nixon akasalimu amri akawasilisha mkanda huo wenye kurasa 1,200 aliorekodi mazungumzo hayo.

Nini kilitokea? Agosti 8, 1974 Nixon akatangaza wazi kupitia kwenye vyombo vya habari kwamba anajiuzulu na siku iliyofuata yaani Agosti 9, 1974 akaondoka na kumwachia madaraka makamu wake Gerald Ford.

Je, tunaweza kufananisha suala hili na tukio la ikulu ya Dar es Salaam kuhusika kulipia tangazo la kukashfu mpinzani wake? Jibu ni ndiyo; wanasheria waangalie taratibu zote zinazotakiwa na ikulu isifunike tupate ukweli wa tukio hilo pamoja na Na +3588976578 na +3588108226.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: