Ya PanAfrican Energy tone tu


editor's picture

Na editor - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

KAMPUNI ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) imebainika kufanya udanganyifu katika mapato iliyopaswa kulipa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na hivyo kushindwa kusalimisha zaidi ya Sh. 100 bilioni.

Kulingana na mkataba wa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia na mafuta ghafi uliosainiwa mwaka 2004 kati ya PAT na TPDC, wawekezaji hao waliruhusiwa kuchukua asilimia 75 ya mapato wanayopata kila mwezi kutokana na kuuza gesi.

Hiyo ni kwa ajili ya kufidia gharama za utafiti pamoja na za uzalishaji, na kwa asilimia 25 ya mapato yaliyobaki, wao wachukuwe asilimia 70 na asilimia 30 yaliyobaki kuyakabidhi TPDC.

Kumbe wawekezaji kwa muda wote huo wa mkataba, wamekuwa wakiongeza gharama za uendeshaji ili mapato mengi zaidi yabaki kwao.

Miongoni mwa matokeo ya mbinu zao hizo chafu, ni kuinyima serikali zaidi ya Sh. 35 bilioni kwa njia ya gawio kutokana na mkataba.

Maofisa wa PAT walipoulizwa kuhusu udanganyifu huo wanadai walikosea kibahati mbaya.

Lakini, kinachoumiza zaidi ni uchunguzi za Kamati Teule ya Bunge kwamba mapato ambayo PAT inakusanya kutokana na mkataba, wanayatumia kwa shughuli za utafutaji wa mafuta nchini Uganda, Gabon na Nigeria.

Wawekezaji wenye uzoefu kama PAT hawawezi kukosea namna ya kufanya hesabu kwa muda wote huo halafu waseme ni bahati mbaya.

Bali kamati nyingine ya bunge inagundua ufisadi kupitia malipo haramu yaliyofanywa na katibu mkuu wa wizara katika harakati za “kufanikisha upitishwaji wa makadirio ya bajeti ya wizara.”

Uchunguzi unabaini kuwa chini ya katibu mkuu wake, wizara inalipa mamilioni ya shilingi kukirimu wanasiasa na fedha nyingine kulipa maofisa wake waliokuwa Dodoma wakati wa bajeti.

Imebainika kuwa maofisa wa wizara hiyo walighushi nyaraka zilizowezesha kufanywa malipo makubwa isivyostahili.

Hivi ni wizara ngapi hutumia mtindo huo kila kikao cha bajeti kinapofika hasa viongozi wanapohisi ugumu wa bajeti zao kupitishwa bungeni? Bila ya shaka ni nyingi hasa kwa kuwa maeneo mengi hayajaleta tija sana kiutendaji.

Sasa wabunge wamebaini. Viongozi watendaji wa ngazi ya juu hadi Ikulu wamethibitishwa kiuchunguzi kukingia kifua wahalifu. Haya yanarudisha mawazo ya Watanzania kwenye kashfa za mikataba ya Richmond/Dowans na ununuzi wa rada ya kijeshi.

Ni malipo gani yanafanywa kwa Watanzania walioumizwa kutokana na vitendo hivyo vya kifisadi vilivyotendwa na watumishi wa umma?

0
No votes yet