Ya Tambwe, Makamba na janga la CCM


Abel Ndekirwa's picture

Na Abel Ndekirwa - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

MWALIMU Julius Nyerere alijaliwa na Muumba wake kuwa na njozi lakini pia kuona mbali. Baada tu ya kupata uhuru alitambua kwamba taifa lilikuwa linakabiliwa na maadui wakuu watatu, ujinga, maradhi na umasikini. Haijalishi sana kipi kinaanza na kinafuata kipi. Itoshe tu kusema aliona mbali.

Miongo kadhaa baada ya kukaa ikulu—alishiriki  kuunganisha TANU na ASP kikazaliwa Chama Cha Maponduzi (CCM), kisha akawa mwenyekiti wake wa kwanza—Mwalimu alistaafu urais lakini pia uenyekiti wa CCM. Hadi anastaafu, aligundua adui namba nne wa taifa; huyu alikuwa CCM.

Mwalimu alipambana sana kuhakikisha CCM inapasuka makundi mawili kwa kuwa alijua fika chama hicho kwa taifa hili, hakikuwa tofauti na ilivyo umaskini, maradhi na ujinga. CCM ni moja ya maadui wa taifa hili na itaendelea kuwa hivyo kwa kitambo itakachobakia kuwa kama ilivyo, CCM moja!

Tangu kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa tume ya kuratibu ukusanyaji wa maoni ya kuandikwa kwa katiba mpya, kumekuwa na harakati nyingi katika makongamano ya kutoa maoni juu ya muswada wa sheria unaokusudiwa kuunda tume hiyo.

Kikubwa ni baadhi ya watu kudhihirisha jazba zao, wengine kuchana nakala ya muswada, wengine kuchoma moto, ilhali wengine wakitokwa machozi wakati wanatoa maoni yao. Haya yote tunaweza kusema ni vibweka; vyaweza kuwa changamoto, lakini pia vyaweza kupuuzwa.

Kinachonisukuma kuandika leo ni tabia ya viongozi watendaji wa CCM chini ya Katibu Mkuu aliyejiuzulu mwishoni mwa wiki, Yusuf Makamba.

Mara mbili, wawakilishi wake ambao nina kila sababu ya kusadiki walitumwa na Makamba kukiwakilisha chama, kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa mjadala wa wasomi juu ya muswada huo, na pili kwenye ukumbi wa Karimjee wakati Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala, ilipokuwa inapokea maoni ya wananchi kuhusu muswada huo ambao tayari umekwisha kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza, walionyesha udhaifu mkubwa wa CCM na kushindwa kutambua kuwa hizi si zama za kucheza shere.

Mwakilishi wa Makamba pale Chuo Kikuu, Prince Bagenda, ambaye hadi leo bado watu wanajiuliza alirejea CCM kupitia mlango gani kwa kuwa hakukuwa na mbwembwe wala chereko kama ilivyozoeleka kila kokoro la CCM linapokokota kila kitambaacho juu ya nchi chenye asili ya binadamu na kusema ni wanachama wake, aliishia kuzomewa.

Siungi mkono tabia hiyo, lakini itoshe tu kusema kuwa alizomewa kwa kuwa alichokuwa akisema ama hakikufanana na hadhi ya mjadala ule, au kwa kuwa alitia walakini kwa kuwa hakuwa mtu ambaye alionekana kuwa CCM halisi.

Hakuwa mwerevu wa kujenga hoja, na hakuwa yule Bagenda mchambuzi wa mambo aliyeaminika hasa alipokuwa amesimama upande unaokinzana na CCM. Bagenda wa upande wa CCM ni kama mtu anayejaribu kusilimishwa na kutaka kuwa imamu aliyebobea papo hapo au Mkristo aliyebatizwa na kutaka kuhubiri kama askofu papo hapo; alipwaya kweli kweli!

Wengi wakiamini kwamba labda Makamba ambaye kwa hakika muda ambao amekalia kiti cha Katibu Mkuu wa CCM ulikuwa ni majuto makubwa kwa hadhi na maendeleo ya CCM, wakati makongamano ya wananchi kuwasilisha mawazo yao kwa kamati ya Bunge juu ya muswada huo, angejirekebisha na kutafuta mwenye busara zaidi kumwakilisha katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, wapi. Aliendelea kulikoroga.

Makamba akamtuma Tambwe Hizza, Kaimu Katibu Kitengo cha Propaganda na Uenezi cha CCM makao makuu, akabofua vibaya! Watu wakamshushua na mwishowe wakatumia nguvu kumtoa kwenye jukwaa la kujengea hoja.

Kikubwa si hoja zake, bali jeuri na kiburi chake; anasimama na kuwakebehi waliokuwa wamechoshwa na kauli zake. Lakini kibaya zaidi alitaka kugeuza ukumbi wa Karimjee kuwa uwanja wa malumbano na si sehemu ya kujenga hoja kwa kuzingatia muswada. Akavuka mipaka na kutaka kujibu hoja za wengine. Tambwe akajipachika madaraka yasiyo yake.

Lakini Tamwe, anayejulikana historia yake tangu akiwa Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kuona joto kubwa pale Karemjee alijiapiza na miungu yake kutoka Usambaani, kwamba hata yeye alikuwa na uwezo wa kukusanya watu na kuwapeleka Karimjee kuujaza ukumbi pomoni!

Hii ni kutokana na kauli yake kwamba waliokuwa wanamzodoa pale ukumbini walikuwa vijana wa CHADEMA ambao walitoka vyuo vya elimu ya juu.

Kama utani vile, kesho yake Tambwe akadamka  mapema, saa 10 alfajiri akazoa vijana mitaani, vijana wachovu, wasiojua hili wala lile, akawapakia kwenye magari hadi Karimjee wakajaza ukumbi kungali bado alfajiri.

Majira ya saa mbili hivi asubuhi wakati watu wenye upeo, wanaojua nini maana ya muswada, na wakiwa wamejiandaa kwenda kutoa mawazo yao, wakapigwa butwaa kukuta ukumbi umejaa vijana wadogo wadogo wanaosinzia ovyo,  hawajui hata pale walikwenda kufanya nini. Mhh! Kazi ya Tambwe, hapana kazi ya CCM ya Makamba.

Wenye fikra pevu wakajua kumbe CCM hata katika hili wanataka kuchakachua, yaani Bunge linatumia fedha kuwatawanya wajumbe wa kamati ya Sheria, Katiba na Utawala, kupata mawazo ya wananchi juu ya muswada huo, lakini wao wanataka kupotosha hasa kile wananchi wanachotaka.

Swali linaibuka akilini mwa watu, sasa hawa CCM wanataka kuchakachua nini?Mbona wale vijana walibebwa kwenye magari wana njaa kali tu?Mbona hata huyo Tambwe mwenyewe anahemea chakula tu? Mbona hata huyo Makamba naye hana hakika sana na kesho?

Swali linazidi kuwa gumu.Hivi katika lile kundi la wale vijana wenye umri mdogo, wenzao kutoka familia za wakubwa serikalini au ndani ya chama, mbona hawakuswagwa kwenda Karimjee?

Hawakuwapo kwa sababu moja muhimu, kwa muda huo ama walikuwa darasani wakisoma kwa bidii kwa kuwa wapo kwenye shule nzuri au vyuoni kwa wengine na wanajiandaa kwa ajili ya kukabili changamoto za maisha baada ya umri wa ujana mwembamba ambao hupewa kila kitu na wazazi.

Lakini hawa wa Tambwe, si tu aliwatumikisha bali alitumia umaskini wao, kupuuzwa kwao na mfumo wa elimu ya taifa, kulaaniwa kwao kwa kuwa ni watoto wa maskini, na kukosa kwao mtetezi isipokuwa Tambwe ambaye naye hana akijuacho zaidi ya kutembeza mdomo, akimwaga sumu mbaya ya kuchochea hasira na chuki miongoni mwa jamii, ndiyo maana akaishia kushushwa jukwaani Karimjee.

Ndiyo maana tunapoitazama CCM hii ambayo ilishikiliwa na Makamba na Tambwe huwezi kusema kuwa Mwalimu Nyerere alikosea kuiweka kwenye kundi moja na maadui wa taifa, yaani umaskini, ujinga na maradhi, kwa kuwa CCM imetufikisha pabaya mno kama taifa. Tusubiri baada ya Makamba na jeuri ya Tambwe ya kukusanya vijana kutoka vijiweni kwenda kuzomea kwenye vikao makini kama itaendelea. Kila la Kheri Tambwe Hizza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: