Ya Tunduma yana harufu ya mbinu za CCM


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

UVUMI uliotanda katika mpakani mwa Tanzania na Zambia, Tunduma, wiki iliyopita kwamba kuna makatasi ya kura yamekamatwa yakiwa tayari zimetikiwa kwa mmoja wa wagombea urais, ni jambo ambalo kwa Tanzania halikupaswa kushangaza wengi.

Si jambo la kushangaza kusikia kwamba kuna njama za kuchakachua kura kwa sababu historia ya chaguzi zote nchini tangu zama za chama kimoja, uchakachuaji wa kura umekuwa sehemu ya utamaduni wa uchaguzi.

Ukisikiliza simulizi mbalimbali za chaguzi zozote ambazo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahusika, malalamiko ya kuibwa kwa kura ni mambo ya kawaida kabisa.

Kuna ushahidi wa dhahiri na mwingine wa kuaminika juu ya rafu kwenye uchaguzi kila CCM inapohusika, iwe ni kwa chaguzi za ndani ya chama hicho au hata pale unapohusisha vyama vingine.

Ushahidi huu ndiyo unafanya watu kila wakati kuishi kwa kushuku kwamba hata katika uchaguzi wa rais na wabunge kama huu ambao Jumapili 31Oktoba 2010, wananchi watapiga kura kuchagua viongozi wao, kuna uwezekano pia wa hila kufanyika.

Kabla ya kuzungumzia hofu hii ya wizi wa kura, tukumbushane mambo machache yanaoelezea hila katika uchaguzi ndani ya CCM.

Mwaka huu wakati wa mchakato wa kura za maoni kupitia CCM kuna maeneo mengi sana malalamiko yaliibuliwa kuwa viongozi wa CCM walihusika kuchakachua kura za wale ambao hawakuwapenda ijapokuwa walikuwa wameongoza katika matawi wakati wa kupiga kura.

Kwa mfano, katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam kura za maoni zilichakachuliwa mno kiasi cha kuwafanya wanachama wa CCM kulalamika kwa viongozi wa juu.

Madai mengi yalionyesha jinsi kura hewa zilivyoingizwa kwa mmoja wa wagombea ili kuhalalisha ushindi wake.

Malalamiko haya hayakuwa Kawe tu, bali pia katika maeneo mengine mengi nchini. Katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi hila hizi zimeacha majeraha makubwa ambayo hayaonyeshi kutibika katika kipindi kifupi.

Utaratibu wa kuchakachua kura ndio mwaka 2002 wakati wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa CCM ulizaa kile kilichokuja kujulikana kama ‘kura za itifaki’ zikiwa zimepigwa kulingana na wadhifa wa kiongozi serikalini.

Ni katika kura hizi, kundi ambalo baadaye lilikuja kujulikana kama wanamtandano, chini ya Jakaya Kikwete na Edward Lowassa; lililalamika kuchezewa rafu.

Habari za ndani ya vikao vya CCM zilieleza wazi kwamba kundi la akina Kikwete liliwasilisha malalamiko rasmi kwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Waliohudhuria moja ya vikao vya juu vya CCM vilivyofanyika Zanzibar, walitoboa siri za ndani ya vikao na kusema kuwa hali ilikuwa mbaya sana kuhusu hujuma hizo za kura za itifaki, kiasi cha watu wa usalama kuitwa kujieleza kwenye kikao hicho.

Ingawa kwa mara ya kwanza Mkapa alionyesha kukerwa na mambo yaliyokuwa yanafanyika nyuma ya pazia tena bila idhini yake, bado hakufuta matokeo ambayo tayari yalikuwa ama yamewapa ushindi wasiostahili au kujeruhi waliokuwa kweli wanatakiwa na wanachama wa CCM.

Hata hivyo, msimamo aliouchukua Mkapa tangu siku hiyo ndiyo kwa kweli baadaye ulimtengenezea Kikwete njia nzuri ya kuingia madarakani mwaka 2005.

Ni kwa sababu, maadui zake wa kisiasa waliokuwa wametumia nguvu za vyombo vya usalama waligundua kwamba Mkapa, akiwa ndiye mwenye serikali, si kutumia usalama kama walivyofanya kwenye kura za itifaki.

Kura za itifaki kama zilivyo kura nyingine zinazochakachuliwa, nia inakuwa ni moja tu, kuhujumu upande mmoja kwa faida ya upade mwingine, tabia hii kama nilivyosema hapo juu imekuwa ni utamaduni wa chaguzi za taifa hili kwa miaka mingi.

Watanzania wangali wanakumbuka kwamba mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa vyama vingi baada ya kuruhusiwa tena mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, kuvurugika kwa uchaguzi katika majimbo yote ya mkoa wa Dar es Salaam haikuwa bahati mbaya.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika ripoti yake ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ilisema wazi kulikuwa na hujuma katika mkoa wa Dar es Salaam, lakini hawasemi nani alifanya hujuma na alitumwa na nani.

Ingawa si rahisi kutaja kwa uhakika mamlaka zozote hapa, itoshe tu kusema kwamba katika vuguvugu la kisiasa lililokuwako mwaka 1995, ilikuwa ni miujiza tu ingesaidia chama tawala wakati ule ipate japo jimbo moja tu la uchaguzi kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Uchaguzi wa majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam kwa maana hiyo yalichakachuliwa kama ambavyo visiwani Zanzibar CCM chini ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, walivyoshikiza uchakachuaji wa kura ambazo zilikuwa zimetoa ushindi kwa Chama cha Wananchi (CUF).

Hali hii kuchakachua kura ilijirudita katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 katika baadhi ya majimbo ya Unguja, haikuwa bahati mbaya, ni mwendelezo ule ule wa kuhujumu upande mmoja na kuubeba mwingine katika kutafuta ridhaa ya wananchi kuingia madarakani hasa unapokuwa haukabaliki.

Ukichukua kumbukumbu hizi ambazo bado zinagonga kwenye vichwa vya wananchi wengi jinsi tunavyoendesha chaguzi zetu, hisia za kuwapo kwa karatasi za kura, haziwezi kukosa nguvu.

Ukichua haya na kuyaweka ndani ya jamii ambayo imeshuhudia kwa miaka na miaka rafu za kimyakimya na za dhahiri zikichezwa kwenye chaguzi zetu, huwezi kuindoa CCM na serikali yake, katika tuhuma hizi.

Ukiangalia jinsi vyombo vya usalama vilivyojisahau na kujikuta ama vikicheza ngoma ya chama tawala, hakuna anayeweza kuamini kuwa CCM imebadili dini yake ya asili.

Ndiyo maana pamoja na taarifa za vyombo vya usalama, wakiwamo Mamlaka ya Mapato (TRA) kwamba kulikuwa hakuna karatasi za kura katika makontena yaliyodaiwa kuwa yalikuwa yamebeba vipodozi, inaacha maswali mengi kuliko majibu.

Maswali haya ni pamoja na hili, ilikuwaje kwa mfano mtu mwenye akili timamu aone makatasi ya kura lakini baadaye yageuke kuwa vipodozi?

Hakuna ubishi kwamba katika siku za hivi karibuni, hasa wiki mbili za mwisho za kampeni kumekuwa na mbinu chafu za wagombea urais kuchafuana.

Kwa bahati nzuri au mbaya muhusika wa uchafuzi huyo amefichuliwa na anaaminika anafanya hivyo kwa niaba ya chama talawa.

Sasa katika njama kama hizi, yaani chama tawala chenye nyenzo na kila aina ya rasilimali kuwafikia wananchi kuomba kura, chama ambacho kimepewa ridhaa tangu uhuru, leo hii kinaamini bila kuhujumu wapinzani hakiwezi kushinda, maana yake nini?

Nani basi anaweza kuwatolea dhamana kwamba pale Tunduma kilichodaiwa kuingizwa nchini hazikuwa karatasi za kura?

Uchakachuaji wa kura ni nembo ya CCM kihistoria. Je, inajinasua vipi kwa tuhuma za Tunduma? Nani atawaamini kwamba hawana njama hizo? Hii ni tafakari yangu wakati tunasogelea sanduku la kura ifikapo Jumapili 31 Oktoba mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: