Ya Tunisia, polisi na majeshi ya ulinzi


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version

HAPO zamani za mwezi uliopita, kulikuwa na kijana – mwanaume aliyeenda shule. Akahitimu. Akapata digrii. Akakosa kazi. Akalazimika kuwa machinga. Ni huko, nchini Tunisia, kaskazini mwa Afrika.

Machinga mwenye digrii akabaingiza. Akadunduiza. Akajenga kibanda. Akawa anafanyia pale uchuuzi wa mboga – mtaani wanakopita watu wengi.

Wakaja mgambo – wakishirikiana na polisi. Wakamkuta machinga. Wakafoka. Vuta nywele. Sukuma huku na kule. Piga mateke. Angusha. Kanyaga. 

Hawakukomea hapo. Wakavunja kibanda cha machinga: tegemeo pekee; kimbilio pekee; kishika uhai cha asiye na mbele wala nyuma. Mwisho wa mategemeo. Mwisho wa kufikiri.

Machinga alipoacha kufikiri akafurikwa na mvurugano wa vitimbi vya maisha. Akafura kwa hasira kuu isiyotawalika; akaongozwa na hisia chache zilizosalia hadi kwenye kibeba mafuta ya taa/petroli. Akajimwagia. Akawasha kiberiti. Akajichoma moto.

Nyuma akawa ameacha machinga wa ainaaina – wenye digrii kama yeye na wasiokuwa na digrii, lakini waliokomaa katika mbinu za mapori ya kisiasa na kiuchumi. Mara hii siyo mesenja. Ni “machinga kaleta balaa nyumbani kwa rais.”

Jijini Tunis na miji mingine – machinga wakajua kuwa mwisho wao umewadia. Wafe kama mwenzao au wasubiri kuuawa? Wafe kwa njaa baada ya kuporwa uwezo wa mwisho wa kudundisha mioyo yao? Wafe vipi?

Ghafla neno “machinga” likapata maana mpya. Siyo tena ile ya mtu hohehahe, mbaingazaji, mdunduizaji, mchuuzi wa bidhaa mikononi; bali mwananchi aliyekosa, aliyenyimwa, aliyenyang’anywa haki ya kuishi; hata ile ya kujikimu – yeye na familia yake.

Hivyo machinga wakakusanyana katika ufukara wao uliowaloanisha mvuani na kuwaanika juani. Hawakukumbuka tena milio ya risasi itishayo kutoka mbali.

Hawakutishika tena kwa ndimi za moto zitokazo kwenye mitutu ya bunduki. Hawakulegea misuli tena kutokana na kukemewa na walioko kileleni.

Walisema, lije na lijalo. Wakaingia mitaani. Wakaimba nyimbo zilizotungwa papohapo; zilizoeleza watakacho na walichotayari kufia. Wakaandamana na kumwambia “mkuu:” Tumechoka.

Wakakataa kuwa wafu wanaotembea. Wakatumia haki yao ya kusema “hapana” kwa vitendo. Hao ndio walimfukuza Rais Ben Ali wa Tunisia. Hicho ndicho kinaitwa “Moto uliowashwa Tunisia.”

Katika mikondo ya waandamanaji – waliokosa, walionyimwa, walionyang’anywa haki ya kuishi; hata ile ya kujikimu – wao na familia zao, mlikuwa na wasomi, wafanyabiashara, wanasiasa ambao miaka yote waliona wamezibiwa fursa za kusogea walikotamani.

Humo mlikuwa na waliokosa ajira kutokana na rushwa. Waliolipwa kiduchu kutokana na wizi serikalini. Waliokosa elimu, tiba na huduma nyingine za kijamii ambazo wote waligharimia kwa njia ya kodi.

Tunisia! Oh Tunisia! Ndani ya waandamanaji walikuwa askari polisi walioishi kwa ahadi hewa mwaka hadi mwaka. Walikaribia kuwa kama askari wa Mobutu Sese Seko wa Kongo-Zaire (DRC) – walioishi kwa “roba” – kukaba watu njiapanda.

Askari wadogo walishazoea kuishi kwa wizi mdogo: kwa madereva, kwa wasichana na wavulana wasaka ngono gizani na kwa kubambikizia vijana kesi.

Ndani ya waandamanaji kumbe mlikuwa na askari wa jeshi la nchi. Nao pia waliishafikia hatua ya kuishi kwa “roba,” isipokuwa wale wachache ngomeni na waliog’ara na rais kila alipokanyaga.

Ni kweli, milio ya bunduki ilisikika mitaani; baadhi ya raia waliuawa, lakini haikuchukua muda vyote vikazimika. Ikasikika lugha moja: rais aondoke na wenzake.

Rais alikuwa tayari alama kuu ya ukandamizaji. Ishara kuu ya ukamuaji wa kodi za wananchi. Kielelezo kikuu cha ulafi wa utawala ambao ulishirikiana na wezi na mafisadi wa ndani na nje.

Rais alikuwa tayari ishara ya kushindwa kwa utawala; kushindwa kulikokuwa chanzo cha kushuka na kudhoofika kwa maisha ya wengi kwa maana ya kupungukiwa au kukosa kabisa chakula, makazi, elimu na ajira.

Yote haya yaliwagusa pia polisi na wapiganaji wa vyeo vya chini ambao ni wengi. Hivyo risasi za moto hazikuendelea kutoka, siyo tu kutokana na polisi kuemewa na umma, bali pia polisi kuwa na maslahi katika kung’oka kwa dikiteta Ben Ali.

Hali ilikuwa hivyo pia kwa askari wa jeshi la nchi hiyo. Waliotoa onyo hawakufuatilia utekelezaji wake. Waliotoa vitisho vya kuua, kujeruhi au hata kufunga wananchi hawakuvifuatilia; kama ambavyo hayo hayakutiliwa maanani na waandamanaji.

Yaliyotokea Tunisia yamedhihirisha kwanza, kuwa moyo umeshinda silaha. Pili, askari polisi na jeshi wana asili ndani ya umma na hufika wakati wakasutwa na dhamira zao zilizoshonwa kwenye ajira.

Tatu, uvumilivu una mwisho. Vijana wa umri wa miaka 25 hadi 30 waliozaliwa na kukulia katika mazingira katili na yasiyoleta matumaini, hatimaye wamejiuliza, “tuna nini zaidi cha kupoteza” wakati watawala wakila na kusaza katika ndoa yao na mumiani wa kiuchumi.

Mbele ya wananchi walioamua kuondokana na utawala wa kidhalimu; askari polisi na jeshi wa ngazi za chini walioamua kusimama na umma na baadhi ya viongozi wa kijeshi walioogopa hasira ya waandamanaji, hakika silaha hazikufua dafu.

Funzo kuu linalopatikana katika mapinduzi ya Tunisia, ni kwamba udhalimu una mwisho na mwisho wake ni fedheha na hata maangamizi. Hata watawala wapya wakiwa dhalimu waweza kuondolewa vivyo hivyo.

Hata kama viongozi wachache wa majeshi walikuwa bega kwa bega na wadhalimu, wezi wakuu na wafisidi fedha na raslimali nyingine za umma; nyoyo za sehemu kubwa ya walinzi na wapiganaji ziliendelea kuwa mingoni mwa umma.

Kwa mara ya kwanza ndani ya Tunisia, askari polisi na jeshi wamedhihirisha kuwa wengi wao si roboti za kufyatua bunduki kila zinapoguswa, bali wenye hisia za umma na wanaoweza  kusimama nao wakati wa haja.

Askari polisi na jeshi wa Tunisia hawakuvunja kiapo. Wamelinda serikali ya nchi hadi ilipotota na kukataliwa na umma ulioiweka. Yahitaji moyo! Walipoona hivyo, wakajiunga na umma kutafuta ufumbuzi.

Polisi na wapiganaji wamerejea makambini na sharti wafanye hivyo kupisha utawala mpya wa kiraia. Watafuta hata kesi walizokuwa wamewaandaliwa waliokamatwa katika siku za kwanza. Hazina maana. Acha historia inukuu intelijensia iliyowaongoza kusimama na umma.

Afrika na dunia inasubiri kuona mabadiliko. Rais Ben Ali aliishi kwa jeuri ya Marekani na Ufaransa kwa misaada ya fedha na zana za kivita.

Alikaribia viwango vya Shah Reza Pahlavi kabla Marekani kumchoka na kushindwa kumtetea mbele ya umma ulioongozwa na Ayatollah Khomeini kuleta mapinduzi ya Iran miaka 32 iliyopita.

Katika hali hii, walioshindwa pamoja na Rais Ali ni Marekani, Ufaransa na mataifa mengine makubwa yaliyoendesha mitambo ya ukandamizaji kwa silaha, fedha na ahadi nono kwa wadhalimu.

Misaada ya kulea na kuneemesha udhalimu kisiasa na kiuchumi, huishia kwenye anguko kuu na fedheha. Ndivyo ilivyokuwa Tunisia. Baada ya hapa, wapi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: