Ya Tunisia yasitokee Tanzania


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi
Maandamano Tunisia

WAHENGA walisema “ukiona mwenzio ananyolewa wewe kichwa chako tia maji”. Nadhani walikuwa na maana kuwa usipotia maji utanyolewa kavukavu.

Habari zilizotufikia wiki iliyopita zilieleza kuwa Rais wa zamani wa Tunisia, Zine – al –Abidine Ben Ali, pamoja na mkewe Leila wamehukumiwa kifungo cha miaka 35 jela baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya mali ya umma.

Katika hali ya ubinadamu mtu ukisikia mtoto amezama mtoni jambo la kwanza kama una watoto utawakumbuka watoto wako. Na kama watoto wako walikuwa na mazoea ya kwenda mtoni peke yao, basi hutulii mpaka utakapowaona.

Ukisikia mikasa inayohusu mama, baba au vijana wa kwanza kuwakumbuka ni wale waliokaribu yako na hasa unaowajali. Ndiyo maana niliposikia Rais wa Tunisia na mkewe wamefungwa jela mara moja nikafikiria hapa nyumbani.

Dunia imeshuhudia miisho tofauti na mingine ya aibu kwa marais wake. Kuna walioishia kufungwa gerezani; wapo waliofia mahabusu kama Slobodan Milosovic. Wengine walinyongwa kama Saddam Hussein, na kuna waliouawa kama Nicolae Ceausescu na wako waliofia ugenini kama Idd Amin Dada.

Kwa Tanzania Mwenyezi Mungu bado anawatunza marais waliotangulia, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Tunamshukuru Mungu kwa hilo. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ametangulia mbele ya haki.
Dunia inataka, kupitia kwake, iandike historia ya mwanasiasa, Rais wa nchi kutangazwa kuwa mtakatifu.

Kumbe kuwa mwanasiasa siyo lazima uwe mhuni au muuaji. Kila mtu atahukumiwa kufuatana na matendo yake. Adhabu zetu zitalingana na nafasi aliyokuwa nayo mtu katika jamii.

Hii ndiyo sababu iliyonisukuma kuandika makala wiki iliyopita kuwa viongozi wetu wa dini zote wajitazame upya. Kwa maoni yangu viongozi wa dini wana wajibu mkubwa kwa jamii kuliko viongozi wengine hususan wanasiasa. Watu hawa wamepewa heshima kubwa na jamii ambayo nao sasa wanaanza kuwagawia wanasiasa.

Katika nchi nyingi, heshima ya viongozi wa kisiasa imebaki kwa vitu vinavyowazunguka, kama misafara mirefu ya magari ya kifahari na ulinzi wa bunduki. Wamepoteza kabisa heshima mbele ya wanachi kwa sababu ya uroho wa madaraka, ufisadi wanaozifanyia nchi zao na dhuluma na mauaji wanayowafanyia watu wao.

Wengine waliokosa fikra, wamebaki kuendekeza utoto, ufuska na anasa za kitalii. Wanafanya upuuzi wa kitoto, kwa kila jambo hata pale maisha ya watu yanapoguswa. Marais wa aina hii duniani wapo.

Kwa mtazamo wangu, huu ni wakati mwafaka sasa kulinganisha urais wetu na urais wa Ben Ali kwa lengo la kutaka kutofautisha. Urais wetu ukiendelea kufanana na urais wake basi mwisho wetu utafanana na mwisho wake. Serikali ya awamu ya nne imetokea kuchezea vyombo nyeti ambavyo serikali zilizotangulia ziliviheshimu.

Mahakama ya rufaa iliposhindwa kuhukumu kama mgombea binafsi awepo au asiwepo ilijivunjia heshima mbele ya jamii. Hii ilitafsiriwa kuwa iliingiliwa na mhimili Serikali.

Sakata la kashfa ya Richmond lilivyozimwa kihuni na Bunge lililopita, lililivua nguo Bunge na kuliacha utupu mbele ya jamii. Viongozi wake walipozawadiwa vyeo vya uwaziri ilivuta hisia kuwa lilisukumwa na mhimili Serikali.

Maana ya mihimili mitatu ya dola hapa inapotea. Inakuja taswira ya utawala wa kiimla. Hali kama hii tutakwepa vipi hukumu? Kuna yale tutakayohukumiwa na wanadamu na kuna yale ambayo Mwenyezi Mungu atatoa hukumu yake.

Sehemu iliyokuwa imebaki bila kutawaliwa na serikali ilikuwa sehemu ya dini. Viongozi wa dini zetu zote wanakoelekea siko. Wako viongozi wa dini ambao wamesimama imara katika imani lakini nao wanajikuta wanaingizwa katika kapu bovu kwa kutowakemea viongozi wenzao wanaoidhalilisha taasisi hii ya Mungu mbele ya wanasiasa.

Viongozi wa dini ya Kikristo walimwalika mwanasiasa Yusufu Makamba kuwa mgeni rasmi ndani ya kanisa la Magomeni. Alipofika akaanza kuwafundisha jinsi ya kuhubiri Injili kwa namna anayotaka yeye.

Asiyemkiri Kristu kuwa ni mwana wa Mungu hastahili kuingia katika nyumba ya Bwana. Mbio za urais zimeanza, sitashangaa kuona viongozi wa dini ya Kiislamu wakimwalika Msikitini mwanasiasa mkristu asiyemkiri Mtume Mohammad (SAW) kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hata nyoka wa mdimu wataihubiri Koran Tukufu.

Wote tunakiri kuwa Mungu ni mmoja. Imani zetu tofautitofauti ziheshimiwe ili tuishi kwa amani kama watoto wa baba mmoja.

Siku zote viongozi wa dini ndiyo waliosimama upande wa wananchi pale Serikali ilipoleta mateso juu yao. Taswira ya kiimla inapojitokeza ni viongozi wa dini ambao wangetegemewa kukemea hali hiyo. Leo chama cha siasa kinawatuma watu wake kuizunguka nchi nzima kuhubiri mafarakano, chuki, fitina, majungu na kisasi katika jamii ileile ambayo dini zote zinahubiri upendo, umoja na amani, viongozi wa dini wako kimya!

Kuna baadhi ya viongozi wetu wamekuwa malofa. Wamefilisika kisiasa, sasa wanatafuta vitu vya kijinga wakidhani vitawasaidia kwa kusema kuna udini nchini mwetu.

Lengo lao ni kujenga chuki kati yetu ambao tumeishi kwa amani tukishirikiana kwa upendo katika sherehe na misiba bila kujali tofauti zetu za kiimani. Viongozi wetu wa dini hawawakemei wanasiasa hawa malofa! Hatari ya jambo hili ni kubwa!

Madhali madhila yaliyowasibu wananchi wa Tunisia ndiyo yanayowasibu Watanzania, kama hazitachukuliwa hatua madhubuti kuleta amani, mwisho mchungu kama shubiri wa Ben Ali na mkewe sisi tutaukwepa vipi?

Katika kutahadharisha mambo Waswahili wana utajiri wa methali kama ‘Hala hala mti na macho’ au ‘mwenye macho haambiwi tazama’ au ‘Ukiona mwenzio ananyolewa wewe chako tia maji’.

Tel: 0713334239, Email: ngowe2006@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)