Yaliyomkuta Lema, yawe fundisho


Josephat Isango's picture

Na Josephat Isango - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Godbless Lema, Mbunge wa Arusha mjini

TUSIDANGANYE. Rais Jakaya Kikwete, bado ana deni. Hajalilipa wala kulitangaza kwa wananchi wake.

Akizungumza wakati wa kufungua Bunge la 10, tarehe 18 Novemba 2010, rais alisema moja ya vidonda vikuu vya uchaguzi vinavyotafuna taifa, “Ni dhambi ya udini.”

Kwamba baadhi ya viongozi wa kidini walitumika kupigia kampeni baadhi ya wagombea. Alitaka wote kwa pamoja kuungana kulipinga jambo hilo.

Hata hivyo, rais katika hotuba yake hiyo, amekacha dhambi moja kubwa inayofanywa na viongozi wakuu wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na wale wa serikali. Dhambi hii si nyingine, ni dhambi ya kuchakachua matokeo.

Ni wazi kwamba rais ameacha kuzungumzia dhambi hiyo kwa kuwa uchakachua ni jadi ya CCM na bila kusimamia hilo, kitambo chama hicho kingekuwa kimeondoka madarakani.

Hii ndio dhambi kubwa au jeraha ambalo bado linatafuna taifa na rais amegoma kulisema.

Kuzungumzia suala la udini kwa sasa ni sawa na kutafuta mwizi katika chumba cha giza na kumwacha yule wa sebuleni ambaye anaonekana.

Hatua ya viongozi wa CCM na serikali kushikiza Mary Chatanda kupigakura katika uchaguzi wa kumtafuta meya wa manispaa ya Arusha, 18 Desemba 2010, wakati si mjumbe halali kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na CCM wenyewe, inathibitisha kuwa baadhi ya viongozi tulionao hawana nia njema na taifa.

Chatanda ni katibu wa CCM mkoa wa Arusha, lakini nafasi yake ya ubunge ameipata kupitia mkoa Tanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, Estomy Chang’a ndiyo chimbuko la maafa yaliyotokea katika uchaguzi huo. Amekubali kutumika kama “dodoki.” Naye amekubali kufanya kazi hiyo chafu.

Uchaguzi wa meya wa manispaa ya Arusha ulifanyika 18 Desemba 2010 bila kushirikisha madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Manispaa ya Arusha, ni ngome kuu ya Chadema. Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, ni Godbless Lema kutoka Chadedema.

Madiwani wa 11 wakiwamo nane wa kuchaguliwa na watatu wa viti maalumu wanatosha kuongoza jiji hilo kwa kuwa itakuwa na madiwani 14.

CCM kina kina madiwani 10 wa kuchaguliwa, watatu wa wa viti maalum na wabunge wawili wa viti maalum; huku chama cha Tanzania Lebour Party (TLP) kikiwa na madiwani 2. Kwa hesabu

Hivyo basi, kwa hesabu hiyo, wajumbe halali wa uchaguzi walipaswa kuwa 31. Ndiyo sababu ya CCM kushikiza Chatanda kupigakura Arusha badala ya Tanga.

Katika utetezi wake, mkurugenzi alidai kuwa Chatanda ni mwalika. Lakini upo ushahidi unaothibitika, kwamba mjumbe huyo wa “kukodishwa” alipigakura.

Kuna hili: Ili mkutano wa madiwani katika Jiji la Arusha uwe halali, unahitaji theluthi mbili ya wajumbe wote. Hii ina maana kuwa wanahitajika kuwapo kwa madiwani 21 kutimiza matakwa ya sheria.

Lakini waliohudhuria ni madiwani 17 kutoka CCM na TLP tu! 

Ili mtu asiyemjumbe katika Bunge au baraza la madiwani aruhusiwe kuingia katika kikao, ni lazima kanuni zitenguliwe na wajumbe wenyewe.

OCD ameingia ndani ya ukumbi wa madiwani. Nani aliyetengua kanuni? Mkuu wa polisi ameingia ndani ya ukumbi na vijana wake na ameelekeza askari wake wa vyeo vya chini, kumshambulia mbunge.

Nani ametoa ruhusa mkuu wa polisi kuingia ndani ya ukumbi wa madiwani? Nani ameruhusu kushambulia wajumbe?

Je, ni kweli kwamba kulikuwa na dalili za uvunjifu wa amani? Je, hakukuwepo na njia nyingine ya kumwita mbunge hadi mkuu wa polisi aruhusu askari kuingia ndani na kumpiga mbunge?

Mbona picha za televesheni zimetuonyesha mbunge akitii maagizo ya polisi?

Ukiacha hilo, kuna jingine pia. Baadhi yetu tunajua vema taratibu za kuendesha vikao vya aina hiyo. Kwamba wajumbe wanapokuwa na malalamiko, msimamizi wa uchaguzi, ama mwenyekiti wa kikao anapaswa kumpa mjumbe mwenye lalamiko, fursa ya kuwasilisha hoja yake.

Je, mkurugenzi wa Arusha aliruhusu hilo? Kuna madai mengine hapa. Mkuu wa polisi ametamba hadharani kuwa yeye ni CCM damu. Ametaka madiwani wa Chadema kwenda watakako, lakini yeye hatateteleka.

Iwapo kila mwenye nafasi atatumia nafasi yake kwa maslahi ya chama chake badala ya taifa, nchi itafika wapi? Kama kila askari atatumia uaskari wake kukandamiza wafuasi wa chama kingine, OCD ataweza kufanya kazi?

Tujaribu kufikiri, hivi mbunge wa Jiji la Arusha mwenye wafuasi lukuki angesema wafuasi wake waandamane kumsaidia kutetea haki, hatima yake ingekuwa ni nini? Kwanini tunataka kupeleka taifa huko?

Yaliyotokea Arusha, yatapongezwa tu na wale wasioitakia mema taifa.

Hata kisingizio cha Chatanda kwamba ni mkaazi wa Arusha, ijapokuwa anakiri kuwa ni mbunge wa viti maalumu kupitia mkoa wa Tanga, amethibitisha bila chembe ya  mashaka kuwa jinsi alivyojipatia madaraka hayo kwa njia hila. Ilikuwaje awe mkaazi wa Arusha, halafu awe mbunge kupitia Tanga?

Mary Chatanda anajua kuwa CCM ilitaja orodha yake ya wagombea ubunge hata kabla uchaguzi haujafanyika. Taarifa hizo zilinukuliwa katika gazeti la serikali la Habari Leo la 27Julai 2010 ambapo Chitanda ilimtaja kuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia mkoa wa Tanga.

Kama tunahitaji utendaji bora unaozingatia sheria; kama tunataka taifa hili liendelee kufaidi matunda ya umoja na amani, ni wajibu wa kila mmoja kukemea vitendo hivi. Lakini iwapo tunachokitendaa, sicho tunachokiamini, basi tunyamazie.

0
No votes yet