Yaliyosemwa tayari yameanza kutokea


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 April 2008

Printer-friendly version
Kuteuliwa na Kujiuzulu kwa Chenge
Andrew Chenge

MwanaHALISI toleo la 20 – 26 Februari mwaka huu, lilichapisha makala ifuatayo juu ya wateule wa Rais Jakaya Kikwete katika baraza lake jipya la mawaziri chini ya kichwa "Wasioteulika ndio wameteuliwa." Mmoja wao alikuwa Andrew Chenge. Tunarudia hapa makala hiyo, kutokana na umuhimu wake kihistoria.

RAIS Jakaya Kikwete ameunda baraza jipya la mawaziri lenye mawaziri 26 na naibu mawaziri 21.

Baraza la mawaziri lililopita lilikuwa na mawaziri 30 na naibu mawaziri 31.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Kikwete kuvunja baraza lake la mawaziri na kuliunda upya tokea aingie madarakani Desemba 2005.

Kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri kulifuatia 'kujiuzulu' kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na waziri mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha.

Kujiuzulu kwa mawaziri hao kulifuatia tuhuma kwamba walinyamazia au walishiriki kupindisha maamuzi halali ya Baraza la Mawaziri, na kukiuka kanuni, taratibu na hata sheria katika kufikia maamuzi yaliyowezesha serikali kuwa na mkataba na kampuni ya Richmond.

Katika baraza lake la sasa, Kikwete amewaingiza baadhi ya wanasiasa wanaotuhumiwa, ama kushiriki moja kwa moja vitendo vya ufisadi, au kunyamazia na hivyo kubariki na, au kushabikia vitendo hivyo.

Miongoni mwao, ni Andrew Chenge, Adam Malima, Lawrance Masha na Profesa Juma Kapuya.

Chenge ambaye amerudishwa katika Wizara ya Miundombinu, ni mmoja wa watuhumiwa katika sakata la ufisadi nchini.

Anatajwa kuhusika moja kwa moja katika kuliingiza taifa katika mikataba ya maangamizi, wakati alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kati ya mwaka 1993 na 2005.

Mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni wa IPTL mwaka 1994 ulijadiliwa na kufikiwa Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa serikali.

Hii ina maana alitoa ushauri uliowezesha kufikiwa kwa makubaliano yaliyoazaa mkataba wa IPTL ambao ni katili na matokeo yake ni mzigo usiobebeka wa gharama ya umeme.

Kinachosikitisha ni kwamba ni Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), vilivyoona uchungu na kushauri serikali ivunje mkataba huo.

Msingi wa ushauri huo ni kwamba mkataba ulifungwa kutokana na shinikizo la rushwa zilizotolewa kwa baadhi ya watendaji serikalini.

Hati ya kiapo ya Patrick Rutabanzibwa, ambaye alikuwa Kamishina wa Nishati na Madini, inathibitisha alikataa kuhongwa dola za kimarekani 200,000.

Hati inaonyesha kuwa Maria Kejo, mmoja wa maofisa waandamizi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ndiye alimpelekea Rutabanzibwa fedha hizo.

Hii ina maana kuwa mkataba wa IPTL ulisainiwa bila kumshirikisha Kamishina wa Nishati na Madini ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maji.

Hata shirika la kupambana na ufisadi duniani, Transparency International (TI), katika ripoti yake, linamtaja Andrew Chenge kuwa mmoja wa wakubwa waliohakikisha mkataba huo unasainiwa.

Hapa Rais Kikwete anagawanyika pawili: kutamu na kuchungu. Huku anasema anapambana na ufisadi na huku anarejesha Chenge kwenye baraza la mawaziri.

Mbali na mkataba wa IPTL, Chenge anatuhumiwa kushiriki kuingia katika mikataba mingine, ukiwamo ule wa ubinafisishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambayo iliuzwa kwa "bei ya kutupa."

Ni Chenge huyohuyo ambaye chini ya uongozi wake kama mwanasheria mkuu, serikali iliingia makataba na kampuni ya kupakia na kupakua mizingo katika kitengo cha makontena bandarini Dar es Salaam (TICTS).

Mkataba huu, hata katika mazingira ya soko huria, unaipa kampuni hiyo hodhi ya shughuli za upakuaji na upakiaji na mkataba wake uliongezewa kinyemela, miaka10 hata kabla kipindi chake cha kwanza hakijamalizika.

Mikataba mingine ya kinyonyaji ambayo ilifikiwa Chenge akiwa mshauri mkuu wa serikali ni pamoja na ule wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC); Tanesco na Net Group Solution ya Afrika Kusini; gesi ya Songas; uuzaji wa Kampuni ya Simu (TTCL) na mikataba ya uuzaji viwanda na mashamba ya mkonge kote nchini.

Ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Akaunti ya Fedha za Nje (EPA) ulitokea wakati Chenge akiwa mshauri mkuu wa serikali. Ama alipuuza, alikataa, alizembea kufanya kazi yake ya ushauri, au alishiriki moja kwa moja katika ufisadi huo.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Chenge anatajwa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni tata ya Tangold iliyochotewa na serikali, kupitia BoT, mabilioni ya shilingi kwa njia ya udanganyifu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, rais halazimiki kuchukua ushauri wa mtu yeyote. Lakini Rais Kikwete, hata kama hataki kuamini kuwa Chenge alishauri vibaya au alishindwa kushauri vizuri, hana sababu ya kukataa kujenga mashaka kwa mtu wa aina hii.

Vyovyote itakavyokuwa, Chenge atakuwa amepoteza, moja kwa moja, sifa ya kuwa msaidizi wa rais, kwani ameshindwa kutimiza majukumu yake aliyokabidhiwa na taifa.

Laurance Masha: Huyu ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia.

Huyu alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, wakati mkataba wa kinyonyaji wa Richmond unajadiliwa na kusainiwa. Masha hawezi kukwepa lawama kwamba alishiriki katika kuangamiza taifa kutokana na hatua yake ya kunyamazia Richmond hadi wakafanikiwa kuvuna wasichopanda.

Ni jambo la wazi kuwa Masha alikuwa anafahamu kila kitu juu ya Richmond. Ndiyo maana hakujihangaisha kwenda mbele ya Kamati ya Bunge kusema kilichofanyika.

Bila shaka, Masha alifanya hivyo kwa lengo la kumlinda swahiba wake mkubwa, Waziri Mkuu 'aliyefukuzwa na Bunge,' Lowassa.

Masha alijua, kama sisi wengine tulivyojua, kwamba Richmond haikuwa kampuni ya Marekani, bali ilikuwa kampuni ya mfukoni ya hapahapa nchini.

Aidha, Masha anatajwa kuwa ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya mawakili ya IMMA Advocate ya jijini Dar es Salaam, ambayo inatuhumiwa kushiriki katika mikataba ya kifisadi.

Kampuni hii inatajwa kuwa ndiyo iliyoandaa na hatimaye kupitisha mkataba kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Deep Green Limited.

Taarifa za Wakala wa Usajili wa Kampuni (BLERA), zinawataja wakurugenzi wawili wa IMMA kuwa wakurugenzi waanzilishi wa Deep Green.

Ni Deep Green iliyochotewa na BoT na Wizara ya Fedha, mabilioni ya shilingi za umma kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Kwa maneno mengine, Masha hawezi kukwepa tuhuma kwamba ameshiriki kuangamiza uchumi wa taifa hili.

Ama ameshiriki, au alinyamazia makampuni hewa kusajiliwa na kuchota mamilioni ya fedha za wananchi.

Hata panga la Kikwete la kung'oa wafanyabiashara na watu wenye maslahi binafsi ndani ya serikali yake, lisingeweza kupita bila kumkata Masha.

Kampuni ya Masha ndiyo mshirika mkubwa wa kampuni za uchimbaji madini nchini, hasa Barick.

Adam Kigoma Malima: Ni naibu waziri wa Wizara ya Nishati na Madini.

Malima ni mmoja wa Watanzania na wabunge waliojifanya vipofu na viziwi katika kushughulikia suala la mikataba ya kinyonyaji; kwa mfano ule wa Buzwagi.

Si mara moja wala mbili, Malima kusikika akisema, "Hii ni mikataba mizuri na yenye tija kwa taifa."

Ni Malima aliyetembelea vituo kadhaa vya redio na televisheni kwa lengo la kuupaka mafuta mkataba wa kinyonyaji wa Buzwagi ili uonekane unafaa mbele ya wananchi. Hakufanikiwa.

Alipoulizwa na wananchi: "Je, unaufahamu mkataba huo? Umeuona?" Hakuwa na la kujibu mbali na kuendelea kung'ang'ana "Mkataba ni nzuri na una manufaa kwa taifa."

Kama dhamira ya Kikwete ya kupitia upya mikataba ni ya dhati, basi asitegemee kupata ushauri wa maana kutoka kwa Malima, ambaye si muumini wa dhamira hiyo ya Kikwete na haonekani kuwa na upeo mzuri katika eneo hili.

Profesa Juma Kapuya: Moja ya tuhuma zake kubwa ni kutumia rasilimali za umma kwa maslahi binafsi.

Kapuya anatuhumiwa kutumia vifaa vya jeshi, ikiwamo ndege na magari kinyume cha taratibu. Ni majuzi tu, chini ya uongozi wake, helikopta ya jeshi ilitolewa kwa matumizi ya raia wa kigeni.

Aidha, Kapuya ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa hapa nchini, akitajwa kumiliki mmoja wa migodi ya madini mkoani Arusha.

Kama helikopta ya jeshi ilivyoanguka watu wakapata fursa ya kujua matumizi yasiyo rasmi ya zana za jeshi; ilikuwa pale wezi walipomwibia Kapuya ndipo ikajulikana kuwa ni mfanyabiashara ya kuchimba madini.

Hata hivyo, wengi wa wateule wa rais hawana uwezo wa kuitetea serikali. Baadhi yao wana tuhuma nyingi na nzito, ambazo kwa hali ilivyo, hawawezi kujitokeza mbele ya wananchi na kutaka kujenga hoja ya kusafisha serikali.

Kutokana na hali hiyo, watu makini wanajiuliza, Kikwete anaelekea wapi? Bila shaka, ni Kikwete mwenyewe na wasaidizi wake ndiyo wanaojua aendako.

Lakini ukiondoa suala la watuhumiwa ufisadi kuingizwa katika baraza la mawaziri, hata uteuzi wa mawaziri wengine unahitaji uchambuzi.

Kwa mfano, Dk. Mauwa Daftari, bado ameendelea kubaki katika nafasi ya naibu waziri, wakati ambapo amekuwamo ndani ya serikali kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Haifahamiki kilichomsibu mwanamke huyo hadi Kikwete kuamua kumuacha papohapo. Labda anafahamika kuwa mchapakazi anapokuwa chini ya mwingine kimadaraka!

Daftari anafahamika kuwa na uwezo mkubwa ukilinganisha na baadhi ya naibu mawaziri waliopandishwa kuwa mawaziri kamili.

Daftari ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ndani ya CCM kwa takribani miaka kumi sasa. Ilitarajiwa kabla ya kupandisha naibu wengine, Kikwete kwanza angemuangalia Daftari.

Labda anahitaji miaka mingine 10 ili "afuzu" na kuwa waziri kamili. Rais wake ndiye ajuaye.

Je, Emmanuel Nchimbi? Huyu anaonekana kutoridhishwa na uteuzi wa sasa. Imefahamika alikuwa ameangalia mbali ya alipopewa.

Nchimbi ni mwenyekiti wa umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) na mjumbe wa Kamati Kuu.

Ukilinganisha na baadhi ya mawaziri, Nchimbi ana uzoefu mkubwa wa uongozi na hajakumbwa na kashifa za kifisadi kama wengine.

Je, mabadiliko haya yatampa usingizi Rais Kikwete? Je, anaweza kuacha kusema kwamba "urais wake hauna ubia?" Je, amefaulu kuwaacha nje wote waliokuwa wanataka ubia kwa urais wake?

Je, Kikwete anaweza kusema kwa uhakika kwamba yuko salama na hatalazimika kubadilisha baraza lake la mawaziri hadi mwishoni mwa miaka mitatu ijayo atakapoomba urais upya?

Haihitaji busara ya nyongeza kujua kwamba, kwa uteuzi wa sasa, bado Rais Kikwete atahitaji kufanya mabadiliko mengine, angalau madogo, ili kumvusha bahari hii ya ufisadi. Chenge ameshindwa kufika mwambao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: