Yanayosemwa kuhusu serikali hii


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

NILIPOFIKA nyumbani kutoka kwenye mihangaiko yangu, juzi, nilimkuta binti yangu mdogo amejiinamia huku akiwa ameshika gazeti  lililokuwa na picha ya Dk. Steven Ulimboka.

Haraka alinipokea kwa swali, “Baba, wameishamuua?” Nikamuuliza kina nani wamemuua? Alichonijibu, najua mwenyewe.

Niwe mkweli, mimi sikumfahamu Dk. Ulimboka zaidi ya kumsikia na kumwona katika vyombo vya habari wakati wa mgomo wa madaktari.

Sasa nikajiuliza, kama mimi sikumfahamu Ulimboka, mwanangu tena mdogo alimfahamu vipi? Kitu gani kilimfanya amfahamu?

Jibu likawa wazi; ni habari za mateso ya kinyama aliyofanyiwa ndiyo yalimfanya mwanangu amfahamu. Naamini wako watu wengi sana ambao  hawakuwa wanamfahamu Dk. Ulimboka lakini sasa wanamfahamu kupitia mateso ya kinyama aliyofanyiwa. Hili ni dosari kubwa kwa nchi yetu.

Waliomfanyia mateso hayo ya kinyama hatuwafahamu lakini Mungu anawafahamu. Kama walitumwa, aliyewatuma ana dhambi kubwa zaidi. Hukumu yao imeandikwa juu ya vichwa vyao nao wataipata hapahapa duniani.

Hadi nilipokuwa naandika makala haya, serikali ilikuwa haijatangaza kama kuna hata mtu mmoja aliyekamatwa kuhusiana na tukio hili la kusikitisha. Hali hii ndiyo inayozidisha hofu, mashaka na wasiwasi katika nchi.

Wananchi wanategemea hifadhi kutoka serikalini, lakini inapokaa kimya na kuonekana kama haifanyi chochote kuwasaka wahalifu hawa, inatoa fursa kwa wananchi kufikiri na kuhisi vile wanavyoona wao kuwa ndivyo.

Wapo watakaodhani kwamba polisi haina uwezo wa kutosha kuwakamata wahalifu hawa. Lakini wapo watakaodhani kuwa polisi haiwezi kuwakamata wahalifu hao kwa sababu ni wenzao, wakiwa na maana kuwa serikali ndiyo iliyotenda unyama huu!

Wananchi wakiachwa waamini hivyo, imani kwa serikali yao itapotea na hivyo kupelekea kupotea kwa amani. Athari zake ni kubwa kwa wananchi wenyewe, kwa nchi na ni hatari kubwa zaidi kwa serikali yenyewe.

Ili kuondoa manung’uniko na hisia mbaya, serikali lazima iunde tume huru kuchunguza tukio hili ili ukweli upatikane.

Tangu lini mtuhumiwa namba moja akapewa jukumu la kujichunguza? Katika mazingira haya, serikali haiwezi kujichunguza kwani kutaamsha hisia kuwa kuna kitu inachotaka kuficha.

Mengi yameandikwa na walioandika wameitwa majina mbalimbali. Mara wachonganishi au wafitini, hata kufika wakati wanaitwa wachochezi.

Ni busara basi kutoa fursa hapa kwa wasomaji wa safu hii, wasome wenyewe maoni ya wasomaji wengine kama walivyoniandikia katika meseji zao.

“Mwalimu mkuu, yaliyotokea yamethibitisha maandiko ya mwanafalsafa Shabani Robert kuwa serikali za wanyama ndege na wadudu ni bora kuliko ya wanadamu. Watanzania hawana imani na yeyote sasa. Na asiye na tumaini wakati wowote atafanya lolote la kutisha. Usinitaje”.

“Makala yako ya 4 Julai kuhusu dokta wetu Ulimboka yaani imenifanya niingie kwenye maombi maalumu kumwombea kwa sababu mateso yake yanafanana na ya Yesu Kristo. Jamani, hao waliomfanyia unyama huo, upanga u juu yao na Mungu aliyemwokoa huko Pande atamponya na wala hatakufa bali ataishi na hata asipoishi hapa duniani ataishi kwa amani ya milele katika Paradiso. By Catherine”

“Kaka umeandika vizuri sana, hakuna mtu ambaye hakulia kwa unyama uliofanyika. Kweli liwalo na liwe ila miaka yao inakaribia kwisha. Magreth Arusha”

“Mwalimu mkuu nimemwona Dk. Ulimboka kwenye tv nimetetemeka. Lakini kinachonifariji hapa ni historia ya kitabu chako cha Mwalimu Mkuu wa Watu, uk wa 14…. Vijana wale wa madini walipigwa risasi na kuuawa na akina ….katika msitu wa Pande, leo Dk Ulimboka tena. Kunapambazuka. Mungu ibariki Tanzania. Yona wa Temeke”.

“Mwalimu Mayega, habari. Naitwa Fumbuka. Mikononi mwangu nina masalia ya gazeti la tarehe 30, Machi 2011. Maneno uliyoyaandika siku hiyo yanathibitisha utimilifu wa nyakati! Uliandika, ‘……Rais dhaifu huifanya nchi yake kukosa mwelekeo. Nchi hujaa malalamiko, manung’uniko na watu waliokata tamaa…’ Hapa ndipo tulipofika. Mwalimu, wanyama wale waliotuficha ukweli ndio walioifikisha nchi hapa ilipofika”.

“Ukifuatilia vipindi vya Bunge hakuna shaka utagundua kuwa kuna machizi. Mtu anachangia mpaka unashindwa kujua anawawakilisha akina nani. Aliyesema wahanga wa Richmond wanyongwe, sasa ni wakati wanafiki nao wanyongwe. Kwa upande wa Ndugai Naibu Spika amepoteza sifa, weledi na ujasiri. Sasa anafanana na mshereheshaji”.

“Mzee Mayega, usishangae sana ya Ulimboka mzee wangu, maana nchi tayari ipo mikononi mwa shetani. Ukishangaa ya Ulimboka utashangaa mangapi maovu yajayo ya kikatili katika taifa hili? Rais hana bilioni 2.1 za kuwalipa madaktari wa ndani, lakini anazo bilioni 200 za kuwalipa madaktari kutoka nje.”

“Biblia inasema haki huinua Taifa, sasa unategemea dhuluma itainua Tanzania yetu? Tuombe uzima, utayaona yakutisha kuliko haya unayoyaona leo. Ni mimi Alfred.”

“Godbless Lema alisema, ‘Ni bora vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu’. R Chuga.”

Yako mengi yanayozungumzwa na wananchi. Jambo zito kama hili haliwezi kupita hivihivi tu! Busara kubwa inahitajika kwa maana ubabe wa liwalo na liwe una athari kubwa kwa pande zote na hasa kwa amani ya nchi.

Msitu wa Pande umekuwa kielelezo cha jinsi ambavyo watu wabaya wanavyotumia baraka tulizopewa na Mwenyezi Mungu kwa mambo yao ya kishetani.

Hayati mama yangu aliniambia, “Ngowe mwanane a Mungu panowaumbanga, waunvile wantu ni vintu” yaani ‘Ngowe mwanangu Mwenyezi Mungu wakati anaumba, aliumba watu na vitu’.

Walioutenda unyama huu ni vitu si watu. Kama liwalo na liwe, ndiyo unyama huu,  basi kilichotendeka kwa Dk. Ulimboka ni unyama! Unyama siku zote hutendwa na wanyama.

Wote waliohusika katika kuutenda hawataikwepa hasira ya Mungu na laana yake itakuwa juu yao kila watakapokuwa wakiukanyaga uso wa dunia yake!

Maandiko katika vitabu vitakatifu yanasema wazi kuwa siku ya hukumu ya mwisho kuzimu kutawatoa wafu  wote. Bahari nayo itawatoa wafu wote waliofia ndani yake. Naamini siku hiyo na msitu wa Pande nao utatoa wafu wake wote waliouawa ndani yake! Nayo majina ya wauaji wao yatawekwa wazi tayari kupokea hukumu yao. Nao watatupwa katika lile ziwa la moto!

0713 334239
0
No votes yet