Yanga ikafute uteja wa kudumu Misri


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

JAPOKUWA timu bora inaweza kushinda nyumbani na ugenini, Yanga ya Dar es Salaam mara zote imekuwa na kawaida kuachia pointi zote au mbili inapokutana na klabu za Misri.

Yanga ni mteja wa kudumu. Kwa hiyo kazi inayoikabili sasa inapokwenda Misri ni kujitahidi kugeuza matokeo kutoka kichapo hadi kuwa sare au ya ushindi walau kwa mara ya kwanza.

Makala hii ina lengo la kuwaonyesha mashabiki wengi wa klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani walioisifu baada ya kufanikiwa kutoka sare ya bao 1-1 na Zamalek ya Misri wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwamba hawajui au wamesahau historia.

Yanga ina rekodi mbaya; kuambulia sare nyumbani na kula mkong’oto wa nguvu Cairo, Misri iwe katika mechi ya marudiano au ya kwanza na wakati mwingine inachapwa nyumbani na ugenini.

Kwa hiyo, inawezekana walioshangilia sare ya bao 1-1 ni mashabiki wapya au wasiofuatilia rekodi ya klabu yao au wanaodhani imebadilika sana. Hao ndio, kabla ya mechi waliifuta Yanga kwenye michuano, lakini baada ya mechi wakadai inaweza kufanya lolote lile ambalo klabu yao imeshindwa tangu mwaka 1982.

Hicho ndicho kinaitofautisha Yanga na watani wao wa jadi katika soka, Simba. Mwaka 1974 Simba iliitafuna Mehla Al Kubra ya Misri Dar es Salaam japo ilitolewa kwa penalti 3-0 hatua ya nusu fainali Misri.

Mwaka huo Simba ilizichapa Linare FC ya Lesotho jumla ya mabao 5-2; ikaiondoa Green Buffaloes ya Zambia 3-1; Hearts of Oak 2-1; Mehalla Al-Kubra 1-0 Dar es Salaam na ikafungwa 0-1 Misri na ikatolewa kwa penalti.

Mwaka 2001 Simba iliichapa Ismailiya bao 1-0 jijini Dar es Salaam halafu ilifungwa 2-0 Misri katika Kombe la Washindi.

Vilevile, mwaka 2003 baada ya kuichapa Santos ya Cape Town, Afrika Kusini kwa penalti 9-8 Simba ilikutana na Zamalek ya Misri. Simba iliongeza sifa mwaka huo, baada ya kuilaza 1-0 jijini Dar es Salaam na katika mechi ya marudiano mikono ya Juma Kaseja iliruhusu bao moja tu Cairo na hatua ya penalti Simba ikapiga 3-2 na kuivua ubingwa klabu hiyo mbele ya mashabiki wake Cairo.

Rekodi ya Yanga ni mbovu. Mwaka 1982 Yanga ilianza michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kuchuana na Textil Pungue ya Msumbiji kwa ushindi wa 2-1 ugenini na pia 2-0 katika mchezo wa marudiano Dar es Salaam.

Ushindi huo wa 4-1 uliipa tiketi Yanga kucheza raundi ya pili ambako ilikumbana na Al Ahly katika raundi ya pili. Mechi ya kwanza Yanga ilikung’utwa mabao 5-0 jijini Cairo na katika mechi ya marudiano iliambulia sare ya bao 1-1 Dar es Salaam.

Mwaka 1988, Yanga ilikutana na Al Ahly tena katika Ligi ya Mabingwa ambapo ilimudu kutoka sare ya 0-0 mjini Mwanza, lakini ilikung’utwa mabao 4-0 katika mechi ya marudiano Cairo.

Miaka minne baadaye yaani 1992, Yanga ilizamishwa raundi ya kwanza na Ismailia katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga ilipigwa mabao 2-0 Misri na mashabiki walidhani ingeweza kusonga mbele, lakini ikaambulia sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Sikio la kufa halisikii dawa. Mwaka 2000 Yanga ilijikuta kwenye mdomo wa Zamalek katika mechi ya Kombe la Washindi. Kama ilivyokuwa safari hii, Yanga iliambulia sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, lakini ilichapwa mabao 4-0 Cairo.

Kama ilivyo miaka mingine, mwaka 2009 Yanga ilianza raundi ya awali kwa kuwapa matumaini mashabiki wake ilipoitandika timu dhaifu ya Etoile d’or (Mirontsy) ya Comoro kwa mabao 8-0 Dar es Salaam na 6-0 mjini Moroni.

Pamoja na ushindi huo mkubwa wa mabao 14-0, safari ya Yanga iliishia kwenye miguu mahiri ya Al Ahly na ikala kichapo nyumbani.

Katika mchezo wa kwanza jijini Cairo Yanga ilifungwa mabao 3-0 na mashabiki wakapata matumaini kwamba Yanga ingeing’oa meno Al Ahly jijini Dar es Salaam lakini wapi ikalazwa mapema kwa bao 1-0 na kubaki ikisubiri mwaka mwingine.

Hii ndiyo rekodi ya Yanga kwa timu za Misri, hivyo mashabiki wanaoomba dua, “wanaoandaa kamati za ufundi” na wanaodai timu imebadilika sana wajue kuwa haijawahi kuwa na ubavu wa kuvuka zaidi ya hapo. Ikishinda Zamalek jijini Cairo tuishangilie, lakini….

0
No votes yet