Yanga na mwelekeo wa kufufuka!


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version

KUNA wakati ilikuwa ni jambo la kawaida kuona viongozi wa klabu kubwa za Simba na Yanga wakichomekea katika usajili majina ya watoto au hata ndugu zao wa karibu.

Na haikuwa ajabu pia kusikia baadhi ya wachezaji `wakinunua’ nafasi za kusajiliwa na moja ya klabu kubwa nchini.

Haya yalifanyika bila kificho. Na kweli, kuna baadhi ya wachezaji walipita katika klabu hizi, lakini wakiwa na viwango duni kabisa.

Kwa ujumla, yalikuwa matunda ya kuua mfumo wa soka la vijana, hivyo kuzilazimu klabu kusaka wachezaji kila unapoingia wakati wa usajili.

Taratibu mambo yameanza kubadilika, yakionekana kwenda kisasa zaidi, ingawa klabu hizi bado hazitoi nafasi kwa timu za vijana, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kwa mfano, Yanga imeanzisha utaratibu wenye kuibua vipaji vya kweli vya soka, badala ya kukimbia majina au kulimbuka kwa kumuona mchezaji siku moja tu.

Kwamba, baada ya kuvutiwa na nyota kadhaa, kocha Profesa Dusan Kondic hakuhadaika na uwezo wa siku moja tu au majina ya wachezaji.

Alichokifanya, ambacho pia kinapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa klabu nyingine ni kuwakusanya wachezaji wote wapya, kuwapa mazoezi maalumu lengo likiwa kuwafuatilia kwa karibu na hatimaye kuwachuja wale wanaoonekana kutobahatisha uwanjani.

Hakuna shaka mfumo huu ni wa kisasa, na wenye kuondoa ujingaujinga katika usajili.

Ni staili hii ndiyo inayotumiwa na klabu zote zilizopiga hatua katika soka duniani. Kwa wenzetu, hakuna mchezaji anayepewa ulaji kwa sababu tu ya kuwa na jina kubwa.

La hasha. Mchezaji huweza kufuatiliwa na klabu hata kwa msimu mzima, na kama akishaonekana anafaa, hupewa nafasi ya kwenda kwa majaribio, angalau ya wiki mbili.

Jiulize, kwa staili hii ni timu gani itakuwa na wachezaji wa ajabu ajabu? Bila shaka hakuna.

Badala yake, timu ya aina hii itakuwa imekamilika katika kila idara, hivyo kuwa na matunda mazuri uwanjani, ingawa kuna wakati inaweza kutelekeza.

Ifahamike kwamba, timu inayofanya vizuri uwanjani ndiyo inayokuwa na nafasi kubwa ya kupata wadhamini wazito, wenye uwezo wa kuifanyia klabu mambo mengi.

Na klabu isiyo na dhiki na njaa, kamwe haiwezi kuyumbishwa na vidhoruba vidogovidogo, bali inakuwa mfano wa kweli wa timu, ndani na nje ya uwanja.

Huko ndiko klabu zetu zinakopaswa kufika, badala ya kuingia katika usajili unaoteketeza mamilioni ya wanachama na mashabiki wake, lakini mwisho wa siku timu ikiwa haina hili wala lile, zaidi ya kutegemea mapato ya milangoni.

Mbaya zaidi, usajili wa mamilioni tunaoushuhudia hauna maana yoyote, kwani mwisho wa msimu bingwa huondoka na fedha kiduchu mno, pengine inayotumika kumsajili mchezaji mmoja tu.

Na hata zinapoingia katika michuano ya kimataifa ambako kuna utajiri mkubwa wa fedha, mathalani Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo bingwa wake huzo sh bilioni 1.3, klabu zetu ni kama `misukule’.

Ndiyo maana nasema kwamba, utaratibu ulioanzishwa na Yanga unafaa kuwa wa kuigwa na klabu zetu.

Hata hivyo, staili hii ya kujaza wachezaji wa kigeni kamwe isigeuzwe kuwa ya kudumu, bali ya kupita.

Kama klabu zetu zikiamua, na kwa staili ya uchangishaji au upatikana wa fedha za usajili, zinaweza kuwa na fungu la kutosha kuendesha timu msimu mzima. Zinaweza pia kuwa na timu imara za vijana na baadaye kuwa tegemea kwa klabu zao, kwani licha ya `kunyeshwa’ maji ya bendera ya timu husika, chipukizi hao wanaopitia katika mfumo huu husajiliwa kwa bei chee, isiyoweza kuwapasua vichwa viongozi.

Na faida kubwa kuliko zote ni uhakika wa kuendelea kuwakomaza wachezaji wanaoweza kuuzwa nje kwa bei kubwa. Ndiyo, soka ni biashara inayolipa kushinda biashara nyingi, tena kwa muda mfupi tu.

Sasa tujiulize, kama kweli dhamira ya klabu zetu ni kusonga mbele baada ya kudumaa kwa miaka 70, kwa nini zisizame katika kuendesha mambo kisasa, lengo likiwa kwenda sambamba na wenzetu waliopiga hatua kimaendeleo, sasa wakivuna faida ya uvumilivu na ubunifu wa mambo?

Yanga imeanza, klabu nyingine zifuate, lakini hatua inayofuata iwe kuimarisha timu za vijana ambao wakipandishwa watakuwa na ubora mkubwa, tena wakipatikana kwa bei ndogo.

Na kwa staili hii, klabu zinaweza kupunguza matumizi makubwa yasiyo ya ulazima, na badala yake kuelekeza nguvu katika kuimarisha vitegauchumi vya klabu, hivyo kuviweka katika hali ya kujitegemea zaidi, badala ya utegemezi wa sasa wa kusubiri hata posho kutoka kwa wafadhili na wadhamini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: