Yanga ni Manji, Madega na wenzake wana nini?


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version

NIMEKUWA nikijiuliza mara kwa mara majukumu ya viongozi wa Yanga tangu kuingia kwa mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji.

Nina sababu za kujiuliza, kwamba siku zote Manji ndiye anayeonekana kuifanyia klabu mambo makubwa, huku viongozi wakibaki mithili ya ‘sanamu’ ndani ya klabu hiyo kongwe kuliko zote nchini.

Kwa mfano, katika msimu uliopita wa Ligi Kuu, tulishuhudia bilionea huyo akimwaga zaidi ya Sh nusu bilioni kwa usajili pekee, achilia mbali gharama nyingine za timu.

Mwisho wa msimu, Yanga iliambulia ubingwa wa Tanzania Bara pekee na kuvuna kiasi kisichozidi nusu ya sh milioni 100. Zawadi ya bingwa wa Tanzania Bara ni Sh 40 milioni kutoka Vodacom.

Pamoja na gharama hizo, Yanga haikuweza kufua dafu kwenye michuano ya kimataifa.

Kimahesabu, tayari Yanga ilishakula hasara isiyomithilika, labda kitu pekee walichoweza kufanikiwa ni kuwatambia watani wao wa jadi Simba waliotoka ‘mswaki’ bila ubingwa tangu mwaka 2007.

Na msimu huu, Manji amefanya kufuru ya aina ile ile kwa kumwaga mamilioni ya fedha kusajili kikosi imara, mpaka kwenye Orijino Komedi, ametokea akijitetea mbele ya mchekeshaji fukara wa maigizo, anayeigiza kama bepari wa Kihaya.

Safari hii amejaza nyota kumi wa kulipwa kutoka nchi mbalimbali za ndani na nje ya Afrika. Haiyumkini ni Yanga pekee inayoonyesha jeuri ya fedha katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Bado Manji anabeba jukumu la kuwalipa mishahara hali kadhalika akibeba mzigo wa `kuwalea’ makocha wa kigeni, Profesa Dusan Kondic na Spaso Sokolovisk.

Lakini cha kustaabisha ni kwamba, pamoja na ujasiri wa Manji wa kumwaga pesa kila kukicha, hakuna cha ajabu kinachoonekana katika soka ya timu hiyo uwanjani.

Inafikia mahali unajiuliza, hivi kulikuwa na umuhimu gani wa Yanga kumwaga kiasi kikubwa cha fedha kama hivi wakati soka inayoonekana kila kukicha ni ile ile?

Mbona hata inapotokea kushinda, mbona wanaocheza ‘Jihad’ si wa kulipwa, bali ni nyota wazalendo wa taifa hili?

Maswali ni mengi, lakini ‘madudu’ ya msimu huu yanaacha maswali mengi juu ya umuhimu wa viongozi wa Yanga, tena wasomi.

Mpaka sasa hawajaonyesha umuhimu wao ndani ya klabu, kwani binafsi ninaamini ama wamelala au wamjisahau.

Ndiyo, tangu kampeni za usajili, Manji amekuwa akitajwa kufanya kila jambo. Na hata wakati timu ilipoanza kambi na kutokea kamgomo baridi, ilielezwa kwa sababu Manji hakuwepo kumalizia posho na viporo vya maslahi ya wachezaji.

Ni kwa sababu hizo zinazotajwa, timu ilianza ligi vibaya, ikitoka sare na baadaye ikaishinda kwa taabu Manyema kabla ya kufungwa na Majimaji ya Songea kabla ya kuponea chupuchupu kwa JKT Ruvu na hatimaye kuzindukia kwa Mtibwa Sugar mwishoni mwa wiki iliyopita.

Nithubutu kusema kwamba, pengine bila Manji kutia mkono wake kuhamasisha wachezaji kuanzia wakati wa maandalizi ya mchezo na ha hata siku ya mchezo, bila shaka Yanga isingeshinda.

Hapa ndipo swali linapokuja, kuna nini Yanga? Ina maana bila Manji Yanga haiwezi kufanya chochote? Kwa mara nyingine, uko wapi umuhimu wa viongozi wa klabu?

Ikumbukwe kwamba, Manji si kiongozi na wala hatambuliki kikatiba ndani ya Yanga.

Pamoja na ukweli huo, viongozi wanaonekana kuwa wamebweteka, kiasi cha kuacha jukumu kubwa la kuitunza timu kwa shabiki wake huyo.

Kwa hakika, viongozi wa Yanga hawapaswi kuendelea na staili hii ya kuendesha klabu.

Kama Manji amesajili timu, amefanya ukarabati wa jengo la makao makuu ambako wachezaji watakuwa na makazi ya kudumu tofauti na kipindi cha miaka kumi iliyopita, bado viongozi wakiongozwa na Mwenyekiti Imani Madega wanapaswa kumwachia mfadhili huyu hata jukumu la kuhamasisha ushindi wa timu?

Liko wapi jukumu la viongozi kama wanashindwa hata kukaa na wachezaji na kupanga mikakati ya pamoja ya ushindi?

Nadhani kuna tatizo, na hili linapaswa kufanyiwa kazi haraka na uongozi wa Madega ambao umejaa wasomi pengine tofauti na watani wao Simba ambao naamini kama wangekuwa na nusu Manji tu, timu yao ingekuwa tishio ndani na hata nje ya nchi, kwani ninawasifu kwa `fitna’ za soka.

Simba hawana jeuri ya fedha kama Yanga, lakini ni mabingwa wa mikakati yenye kutetemesha, ndiyo maana najaribu kujiuliza ingekuwa vipi kama Manji angekuwa anaifadhili Simba?

Inakuwaje hata posho za wachezaji asubiriwe mfadhili anayeifanyia klabu hiyo kila kitu?

Wakati umefika viongozi wa Yanga waonyeshe uwezo wao halisi wa uongozi, badala ya kuwaaminisha wadau kwamba, bila Manji klabu yao haiwezi kwenda kokote. Hizo ndizo salamu zangu za Idd Mbarak.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: