Yanga sasa ikuwe!


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version

NIANZE kwa kuipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu huu.

Imefanikiwa kuivua Simba ubingwa baada ya kujikusanyia pointi 49 katika michezo 26 katika ligi hiyo iliyoshirikisha timu 14, ingawa Coastal Union ya Tanga, Ashanti United, Manyema na Pan African za Dar es Salaam zimeishia kuangukia pua! Pole zao, bila shaka watajipanga upya.

Naipongeza pia Prisons kwa kugangamala na hatimaye kushika nafasi ya pili inayoipeleka katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Wakati Prisons ikijikita katika Shirikisho, Yanga itakuwa katika michuano yenye hadhi, ushindani na utajiri mkubwa wa fedha katika ngazi za klabu Afrika, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa Simba, mambo yamekuwa magumu, kwani baada ya michuano ya Kombe na Kagame na Tusker baadaye mwaka huu, watalazimika kusubiri pengine hadi mwaka 2010 kucheza michuano ya kimataifa, kama upepo mzuri utavuma upande wao.

Lakini hoja ya msingi iliyonisukuma kuandika makala hii ni kuhusiana na maana halisi ya ubingwa wa Yanga.

Kwamba, sasa viongozi wakuu, wachezaji, wapenzi na wanachama wanapaswa kufahamu kwamba, kuitambia Simba tu kwa kuipiku katika kampeni za ubingwa wa ligi yetu inayotajwa kujaa madudu, ni mambo yaliyopitwa na wakati.

Isonge mbele, na kuona kwamba, ina jukumu la kujiimarisha zaidi katika michuano ya kimataifa, hasa baada ya miaka nenda miaka rudi kuonekana wamekuwa wakishiriki badala ya kushindana, pengine kwa kiasi kikubwa ikichangiwa na kukosa malengo.

Leo hii, Yanga ikiwa na mfadhili `kimwaga', haina budi kukaa chini na kutafakari jinsi watakavyouenzi ubingwa wao.

Hapa nazungumzia tiketi waliyonayo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa mwakani, ikiwa na maana miezi tisa kuanzia sasa.

Miaka ya nyuma suala la muda wa kuziandaa timu zetu ulionekana kuwa mfupi, kwani ligi iliishia mwishoni mwa mwaka na kuunganisha na usajili, lakini hata kabla ya wachezaji kuzoeana, timu inaingia mashindano na kunyukwa, kisha zinarejea kwenye soka yetu ya fitna, basi.

Lakini sitarajii kuiona Yanga ikileta tena aibu kwa Watanzania kuanzia msimu ujao.

Ndiyo, itakuwa kichekesho cha aina yake kwa timu iliyopewa miezi tisa ya kujiandaa, kisha ikaingia mashindanoni kunusa na kuondoka, eti kwa sababu ya ubovu wa timu.

Kwa Yanga, na hata Prisons, kama ni muda wa kufanyia marekebisho vikosi vyao wanao wa kutosha, wana muda wa kuziandaa timu kwa ajili ya ushindani wa kweli, na kubwa zaidi, hata makocha wetu ambao mara kadhaa tumekuwa tukiwasikia wanalilia angalau miezi sita ya kuivisha timu, sasa nao watakuwa na uwanja wa kujidai.

Tusijidanganye, miezi tisa inaweza kuonekana mingi kwa kuitaja, lakini kwa viongozi wasio makini, wanaweza wakajikuta wakishindwa kufanya lolote la maana ndani ya muda huo.

Hatutaki yatokee hayo, ndiyo maana hata awali nilieleza kwamba, itachekesha kama Yanga itavurunda.

Ufikie wakati sasa klabu zetu zijenge heshima nje ya nchi, kwani mbali ya kujitangaza na kuvutia wadhamini wa uhakika, watajiweka pia katika nafasi ya kufanya biashara kubwa ya wachezaji, kwani matunda yao yatakuwa yanaonekana.

Hili likiwezekana kama ilivyo kwa ASEC yenye uhakika wa kuingiza mamilioni ya dola kila mwaka kwa kuuza wachezaji Ulaya na kwingineko duniani, Simba na Yanga na hata klabu nyingine nchini zitakuwa zimejikomboa na kuachana na staili ya kutegemeo mifuko ya wafadhili `uchwara', na hata wakati mwingine kujikuta viongozi wakikunjana na wachezaji kwa sababu ya `vijimishahara' ambavyo kwa ujumla havifikii hata sh milioni 5 kwa mwezi.

Hivi kwa klabu kubwa na kongwe, yenye wanazi wengi kila pembe ya nchi inakuwa na ujasiri gani wa kutambia jina ilhali pamoja na vitega uchumi inageuka ombaomba kila kukicha?

Tukubaliane kwamba, mambo haya sasa yamepitwa na wakati, Yanga inapaswa kukua, ili watani wao Simba nao wajitutumue kushindana nao, hapo ndipo maendeleo ya kweli ya soka na hata mapinduzi ya kiuchumi katika ngazi za klabu zetu nchini yataonekana kiasi cha kuweza kuzungumza lugha moja na klabu tajiri barani Afrika zikiwamo zile za Afrika Kusini, Misri na nchi za Magharibi mwa Afrika.

Huko ndiko tunakopaswa kwenda, si kuleteana ubabe, uchawi na fitna katika soka ya bongo kwa lengo la kuhamisha taji kutoka mtaa mmoja kwenda mwingine, basi. Na tutafakari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: