Yanga na siku 38 za kuiua Al Ahly


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 February 2009

Printer-friendly version

USHINDI wa Yanga wa mabao 8-1 dhidi ya Etoile d'Or Mirontsy ya Comoro ni ishara tosha kwamba, wakali hao wa makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, pale Kariakoo, Dar es Salaam wameshamaliza ngwe ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoongoza kwa utajiri mkubwa wa fedha, utitiri wa vipaji na mvuto.

Ni miujiza tu ndiyo inayoweza kuwashukia Etoile na kuweza kuwageuzia kibao Yanga katika mchezo wa marudiano na hatimaye kuwatupa nje ya michuano ya mwaka huu.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kupigwa kati ya Februari 13 na 15 na kuchezeshwa na  Dlamini Gilbert wa Swaziland atakayesaidiwa na Mbingo Petros na Mkhabela Bhekisizwe pia wa Swaziland.

Mwamuzi wa akiba atakuwa Amaldine Soulaimana wa Comoro na kamisaa atakuwa Roch Henriettes wa Shelisheli.

Kwa tafsiri iliyo rahisi, Yanga sasa italazimika kuelekeza nguvu katika raundi ya pili kuvaana na wababe wa soka ya Afrika, Al Ahly ya Misri wanaoshikilia ubingwa wa bara kwa sasa.

Kwa ujumla, Al Ahly wametwaa ubingwa wa Afrika mara sita.

Wachambuzi wa masuala ya soka wanaamini kwamba, safari ya Yanga itaishia kwa Al Ahly maarufu kama 'Red Devils', yaani `Mashetani Wekundu' kutokana na sababu kadha wa kadha.

Miongoni mwa sababu ni rekodi ya Waarabu hao wa Misri dhidi ya Yanga.

Kwa mfano, mwaka 1982, Yanga baada ya kuitoa Textile Pungue ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 4-1, iliangukia kwa Al Ahly walioshinda 5-0 jijini Cairo na katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam, ngoma iliisha kwa sare ya 1-1.

Miaka sita baadaye, yaani mwaka 1988, baada ya kuitoa Wagad ya Somalia, kwa mara nyingine iliangukia kwa Al Ahly.

Ilijitutumia kwa suluhu nyumbani na ilipokwenda Cairo, Yanga ikalambwa 4-0!

Na baada ya kupita miaka 20, timu hizo zinakutanishwa tena, mchezo wa kwanza ukitarajiwa kufanyika kati ya Machi 13 na 15 huko Cairo, Misri, ingawa kuna uwezekano mkubwa wa ngoma kuangukia Ijumaa kutokana na utamaduni wa nchi hiyo.

Hii ina maana kwamba, tunahesabu siku 38 kuanzia leo kwa timu hizo kukutana katika shughuli inayoaminika kuwa ngumu kwa Wanayanga.

Ndiyo, kwa hesabu za haraka, Al Ahly ni mlima mrefu kwa Yanga, lakini kama mikakati ya kweli ikiwekwa, Yanga iliyoimarika katika kila idara ya 2008 ina kila sababu za kuwaduwaza wababe hao wa soka wa Afrika.

Kamwe Yanga wajisidanganye kwa ushindi ulioacha gumzo Afrika mwishoni mwa wiki wa mabao 8-1 (hatujui mavuno mengine itakayoyapata katika mchezo wa marudiano) na kudhani kila kitu kitakuwa chepesi kwao.

Tayari nyota wa Yanga wameshaanza kukaririwa wakitamba kuwa bado Ahly! Ahly ipi kwa kulambwa kirahisi hivyo?

Kama Etoile walikuwa wagumu na kuitia kiwewe yanga katika dakika 45 za kwanza, kwa nini Al Ahly ambao ni wazoefu katika soka ya Afrika kwa zaidi ya miaka 100 walinganishwe na Wacomoro wanaoitia mguu kwa mara ya kwanza katika soka ya kimataifa?

Hapa ndipo ninapoona kuna dalili za kuvimba kichwa na kudhani kila kitu kitakuwa mteremko mbele ya mabingwa hao watetezi.

Lazima Wanayanga waelewe kwamba, nguvu, akili na maarifa yote yanapaswa kuelekezwa katika kusaka mbinu za kufuta uteja dhidi ya timu kutoka mataifa ya Kiarabu na pia kufuta dhana ya kuwa kibogoyo linapokuja suala la michuano ya kimataifa.

Kwa aina ya usajili wa Yanga hii msimu wa 2008/9, inatoa matumaini kuwa, kama nguvu na mikakati thabiti ikiwepo, hata Ahly wanaweza kutemeshwa ubingwa kama ilivyokuwa kwa Zamalek mwaka 2003 walioduwazwa na Simba, timu pekee ya Tanzania inayotajwa kuwa na mbinu za kimataifa.

Tujiulize, kama Simba waliweza kuwavua ubingwa Zamalek mwaka 2003, tena ikiwa na mastaa wengi wa Kitanzania, kwa nini miaka sita baadaye Yanga iliyoimarika zaidi ishindwe kufanya kweli?

Na bahati kwa Yanga yaweza kuwa ratiba inawabeba, kutokana na kuanzia ugenini ambako kama wakigangamala, wanaweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano mbele ya umati wa mashabiki wake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Historia inaonyesha kwamba, mara zote mbili ilizotolewa na Ahly, Yanga haikuwahi kufungwa nyumbani, bali ilikandamizwa kwa idadi kubwa ya mabao ugenini Cairo na hivyo kuwapisha Waarabu hao waendelee na safari katika michuano.

Je, miaka 17 ya uzoefu wa Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa (zamani Klabu Bingwa Afrika) bado Wanayanga wataendelea kuwa wanyonge kiasi cha kuwa washiriki tu wa michuano ya Afrika badala ya kuwa washindani?

Haiingii akilini na haitakuwa na maana ya kujiimarisha kwa usajili unaotafuna mamilioni ya shilingi kama ubavu utaendelea kuishia kwenye Ligi Kuu pekee.

Yanga kama inavyoonekana kuwa ni timu ya ushindi, ifungue ukurasa mpya katika michuano ya kimataifa kwa kujiandaa na kushiriki kikamilifu bila ya woga wa majina au sifa za klabu wanayokutana nayo.

Haya yakizingatiwa, tunaamini siku 38 za maandalizi ya kuiua Al Ahly zikitumiwa vizuri, zinaweza kuzaa matunda na kuifanya Yanga na Watanzania kwa ujumla kutembea kifua mbele kutokana na kufanya mambo makubwa yanayoashiria mapinduzi ya kweli ya soka ya nchi hii si  kwa timu ya taifa pekee `Taifa Stars' bali hata klabu zetu.

Kwa maandalizi ya dhati, mastaa kama Mohammed Aboutrika, Flavio Amado, Mohammed Barakat, Ahmed Hassan, Osama Hosny na hata Wael Gomaa hayatakuwa na jeuri ya kuwafunika akina Mrisho Ngassa, Athuman Idd, Shadrack Nsajigwa, Juma Kaseja, Mike Baraza, Boniface Ambani, Ben Mwalala, Nadir Haroub `Cannavaro', Jerry Tegete, Abdi Kassim `Babbi' na wengine.

Na pia hawataweza kufuta ndoto za bilionea mwenye matarajio makubwa na kikosi hicho, Yussuf Mehboob Manji au hata jopo la makocha waliobobea katika soka ya kimataifa wakiongozwa na Profesa Dusan Kondic.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: