Yanga, Simba zakosa ‘minoti’ FIFA


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version

KLABU 400 zilizotoa wachezaji walioshiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika zinatarajiwa kupata mgawo wa mapato ya mechi hizo.

Klabu zitakazonufaika zinatoka katika vyama 55 vya soka wanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Mashindano hayo ya kwanza kufanyika Afrika yametajwa kuwa yalikuwa ya mafanikio makubwa.

Kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa, hakuna hata klabu moja ya Tanzania ambayo itanufaika na mgawo huo kwa vile hakuna hata mchezaji mmoja, awe wa ndani au nje, aliyekuwemo kwenye vikosi vilivyoshiriki fainali hizo. Hispania ilitwaa ubingwa baada ya kuilaza Uholanzi katika fainali.

Klabu za Tanzania husajili wachezaji kutoka nchi jirani kama Kenya, Uganda, Burundi, Zambia ambazo nazo hazikushiriki.

Hata wachezaji kama Ernest Boakye, Isaac Boakye na Yaw Berko kutoka Ghana iliyoshiriki michuano hiyo ya fainali, wanaonekana lulu Yanga lakini hawachezi katika timu za taifa.

Davis Mwape kutoka Zambia pia hayumo kwenye kikosi cha Chipolopolo. Ivan Knezevic wa Serbia ni mali Yanga lakini si mali Serbia.

Simba ina Emmanuel Okwi, Patrick Ochan na George Owino wanaochezea Uganda Cranes lakini haikufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Vilevile yupo Jerry Santo na Hilary Echessa wako kwenye kikosi cha Harambee Stars ambayo haikufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Kwa hiyo, kutokuwa na wachezaji wa daraja la juu kimataifa ni sababu mojawapo ya kuwa na ushindani wa kiwango cha chini kwamba yuko katika kikosi cha taifa kwa vile hakuna waliobora zaidi.

Taifa Stars, kwa mfano, ikiwa na wachezaji nyota kutoka klabu kubwa nchini, imekumbana na kisago cha mabao 5-1 kutoka kwa Misri katika mchezo wa mechi za Bonde la Mto Nile. Mechi ya pili ikatoka sare ya bao 1-1 na Burundi.

Kilimanjaro Stars ililambwa na Zambia katika mechi ya kwanza ya Kombe la Chalenji mwezi uliopita, lakini ikajikongoja na kufika fainali ambako iliichapa Ivory Coast isiyo na majina makubwa bao 1-0 na kutwaa kombe hilo.

Hivyo, pamoja na Simba na Yanga kuwa na ushindani wa hali ya juu na kutoa wachezaji wengi katika kikosi cha timu ya taifa, haziwezi kupata mgawo huo kwa vile hazikuwa na mwakilishi ama kupitia Taifa Stars au timu za taifa za nje.

Mgawo huo wa mapato yaliyotokana na mashindano hayo yatagawanywa kupitia vyama wanachama kwenda kwenye klabu ambazo zilitoa wachezaji 736 walioshiriki hatua ya mwisho ya mashindano hayo.

Klabu zilizotoa wachezaji wengi ndizo zitanufaika zaidi na mgawo huo wenye thamani ya dola 40milioni.

Uamuzi wa kugawa mapato ya fainali hizo ulifanyika Machi 14, 2008 Halmashaurio Kuu ya FIFA ilipoamua kuweka kifungu cha kanuni kuidhinisha kiasi cha dola za Kimarekani 40 milioni kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini na dola 70milioni kwa ajili ya Kombe la Dunia Brazil mwaka 2014.

Lengo ni kutambua mchango unaotolewa na klabu katika mafanikio ya fainali za Kombe la Dunia la FIFA.

"Tunafurahi kusema kwamba sasa tunaweza kugawana mafanikio ya Kombe la Dunia 2010 pamoja na klabu kwa kuzipatia kiasi cha faida ya mashindano haya, hasa kwa lengo la kutambua juhudi katika kuendeleza wachezaji vijana,” alisema Rais wa FIFA, Joseph S. Blatter.

Kwa mujibu wa Blatter, mgawo huo ulikokotolewa kwa kuangalia idadi ya wachezaji kutoka klabu walioshiriki, idadi ya mechi walizocheza.

Ukokotowaji wa muda ni kuanzia wiki mbili kabla ya mechi ya ufunguzi hadi siku timu ya mchezaji husika ilipotolewa.

Kisayansi zaidi ni kwamba “idadi ya jumla ya mchezaji” zilikokotolewa kwa kuzidisha na idadi ya siku mchezaji na kiasi kilichopatikana ni dola 1,600.  FIFA haikujali kama mchezaji alikuwa uwanjani anacheza au alikuwa benchi, bali imejali siku ambazo amekuwepo kwenye timu.

Klabu tano ndizo zimeondoka na kitita kikubwa kwani zilikuwa na wachezaji wengi katika fainali hizo.

FC Barcelona ya Hispania imepata dola 866,267;

FC Bayern München imeweka kibindoni dola 778,667);

Chelsea FC imejikusanyia dola 762,667;

Liverpool FC imebeba dola 695,600);

 Real Madrid CF imetengewa dola 678,133).

Japokuwa orodha hiyo imetawala na klabu zilizoko ligi maarufu, ukweli FIFA imepeleka mgawo hata kwa klabu ambazo hazishiriki ligi kubwa, muradi tu ziwe zilitoa wachezaji.

Hii ina maana hata klabu ambazo timu za soka za taifa hazikushiriki fainali hizo, zitaambulia mgawo kwa vile kigezo ni klabu kutoa wachezaji.

FIFA pia hugawa fedha zaidi ya dola 300,000 kwa vyama vya soka kutoka nchi zinazoendelea kwa lengo la kuendeleza soka ya vijana kupitia kile kinachoitwa Goal Project.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: