Yanga waambulia kuizomea Simba


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

KWA ushabiki, mtu anaweza kuiponda klabu ya Simba kwamba haina lolote; na kwa ushabiki mtu anaweza kuipenda Yanga kwa moyo wake wote.

Ukweli Simba ina kila kitu cha kumfanya mpenzi wa soka aishabikie; iko hatua nzuri kutawazwa mfalme wa soka nchini na iko mguu mmoja ndani ya hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Imeziondoa Kiyovu ya Rwanda, ES Setif ya Algeria na imewatia adabu Al Ahly Shandy ya Sudan kwa kuifunga mabao 3-0 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mkondo wa kwanza. Inahitaji kushinda ugenini au kutoka sare au ifungwe mabao chini ya 2-0 isonge mbele.

Mzigo uko kwa Shandy, lakini Msimbazi ni chereko na hoi hoi. Wapenzi wamefurahi na wanapongeza uongozi wao kwa kusajili kikosi madhubuti na kuajiri kocha bora.

Simba wanatia raha lakini kwa watani wao wa jadi, Mtaa wa Jangwani hakuna furaha, wapenzi wamenuna, bundi aliyetua tangu mwanzo wa Ligi Kuu hajaondoka. Wazee wamehamaki, wanachama wamekasirika na viongozi wanasutana na kujiuzulu.

Lakini tuwaulize, Yanga wameandikiwa na nani kuwa mabingwa wa kudumu nchini? Je, walikuwa na uwezo wa kuepuka aibu hii? Je, viongozi na wazee walikuwa na mikakati yoyote ya maana?

Yanga haikuanza Ligi Kuu ya Bara kwa mafanikio na katika hali ya kushangaza ikamtimua kocha Sam Timbe aliyeipa taji msimu uliopita na kumrejesha Kostadin Papic aliyeikacha klabu hiyo.

Filamu ikakamilika. Mzunguko wa pili ulipoanza, habari kutoka Jangwani zilikuwa za masikitiko – kocha analia njaa na wachezaji wanalia. Ilipoingia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilinusa tu – ilitolewa asubuhi kweupe ikaambulia kuvaa jezi za wapinzani wa Simba na kuzomea katika mechi za kimataifa.

Hiyo ndiyo mikakati iliyoonekana kwa Yanga. Katika hatua muhimu ya kutetea ubingwa, wachezaji wakaacha mafundisho ya soka waliyopewa na Papic, wakageuza Uwanja wa Taifa, kuwa ulingo wa makonde.

Katika mechi dhidi ya Azam FC, timu inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Yanga wakadai kipigo cha mabao 3-1 walichopata kilichangiwa na mwamuzi Israel Nkongo. Wakaacha kucheza soka wakamsindilia makonde sawasawa.

Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikaliona hilo kuwa kosa la kuutia aibu mchezo wa soka, ikawafungia vipindi tofauti na kuwapiga faini.

Hatua hiyo ikawaibua wazee wa Yanga ambao badala ya kufuatilia kujua tatizo ili lirekebishwe, wao wakajiingiza kulumbana na TFF.

“Eeeh, tunajua, wamepanga timu moja iwe bingwa. Tutaonana. Wao wamemwaga ugali, sisi tutamwaga mboga,” alitamka mmoja wa watu wenye hadhi ya uzee wa klabu.

Katika matamshi yao, walipinga uwezo wa Kamati ya Ligi kutoa adhabu; wakadai TFF imepanga klabu moja iwe bingwa; na wakaapa kupambana na TFF.

Wazee hao ambao walipaswa kuwa dira ya klabu hiyo kongwe nchini, walibaki na hasira zao dhidi ya TFF huku wakiwaacha kocha mkuu, kocha msaidizi pamoja na meneja wa timu wakifanya kosa jingine kubwa na lenye madhara la kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Canavarro’ katika mechi nyingine dhidi ya Coastal Union huku wakijua alipaswa kutumikia adhabu ya kutocheza mechi tatu kwa kosa la kumpiga mwamuzi.

Hapo wazee waliibuka tena kuikoromea Kamati ya Ligi kwamba inawawangia kuipa Coastal ushindi wa pointi tatu na mabao matatu hivyo kubatilisha ushindi wa bao 1-0 iliyokuwa imepata Yanga.

Mwishoni mwa wiki, wazee wa klabu hiyo walionekana kurejewa na akili zao, wakagundua kwamba katika kadhia yote hii, viongozi wao wanahusika kwa uzembe.

Wakagundua kwamba kumbe TFF iliwapa taarifa kuwa klabu isimtumie Canavarro kwa sababu anatumikia kadi nyekundu aliyoonyeshwa aliposhiriki kumtwanga mwamuzi.

Lakini mara wakaondokewa na busara; wakatangaza kuitwaa timu kwa nguvu kutoka kwenye mikono ya uongozi wa Mwenyekiti Lloyd Nchunga.

Wakasema wanatwaa timu ili kulinda wachezaji waliopo wasiondoke; kuiandaa vema kwa ajili ya mchezo wa kufunga msimu wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, ambayo imeitafuna Shandy 3-0 na mwisho kufanya mikakati ya kurejesha nidhamu.

Huhitaji kuwa mzee kujua kwamba wazee wa Jangwani ni sehemu ya tatizo. Wazee wanaopaswa kuwa washauri wanaingia jikoni kufanya nini? Kama wangetulia tangu mwanzo, si wangesaidia kudhibiti nidhamu ya wachezaji na viongozi?

Wazee wanapotaka kutwaa timu, wanajua hizi si enzi za mwaka 47 walipokuwa na uwezo wa kupindua meza na kuuondoa uongozi wapendavyo? Wanajua kuwa tangu wawe wanachama wa TFF hawana uwezo wa kupindua meza?

Wazee waonyeshe busara wadhibiti kwanza viongozi wanaojiuzulu ovyo, warejeshe mshikamano, nidhamu, wasome kanuni, wajue mipaka yao ili kuepusha vurugu. Aidha, waiandae vizuri timu yao ili mwakani itoe ushindani isiishie kuvaa jezi za kuizomea Simba.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: