Yanga yaelemewa na wachezaji


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version

YANGA ya Dar es Salaam imeanza kulemewa na wingi wa wachezaji inaosafiri nao sasa inapanga kupunguza saba katika kila safari ili kupunguza gharama ugenini.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kwamba kwa wastani, Yanga huwa na msafara wa watu 33, ambao hutumia si chini ya Sh milioni 1.4 kwa malazi na chakula pamoja na matibabu madogo.

Uchunguzi unaonyesha malazi kwa wachezaji pamoja na viongozi wa Yanga hugharimu karibu Sh 700,000. Vyumba vya malazi kwa wachezaji kugharimu kati ya Sh 20,000 na Sh 30,000 na chakula hugharimu karibu Sh.700,000.

“Tumeamua kupunguza wachezaji kwa sababu ni wengi na wengine husafiri tu hawachezi,” kilisema chanzo cha habari hizi.

“Tukipunguza wachezaji saba katika msafara tutakuwa tumepunguza karibu Sh 285,500. Ni kiasi kidogo, lakini kinasaidia,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Katika safari moja, Yanga huwa na wachezaji 27 na viongozi wasiopungua sita wakiwemo kocha mkuu, msaidizi, daktari wa timu na meneja. Pia husafiri na mtu wa kufua jezi, katibu na kijana wa kutumwa.

Lakini katika mazingira yaliyozoeleka kwa klabu kubwa za Simba na Yanga, pia huwepo kundi la wanachama waitwao ‘kamati ya ufundi’ na mashabiki maarufu. Wote hao hulipwa na klabu.

Yanga inafikiria kupunguza wachezaji katika safari zao katika kipindi ambacho inakabiliwa tatizo la kutakiwa kuwalipa nyota wake watatu waliotemwa wakiwa ndani ya mkataba.

Kwa mujibu wa kanuni za usajili, timu hutakiwa kutoa taarifa ya wachezaji itakaowatema kabla ya kusajili wengine. Yanga haikufanya hivyo.

Yanga imejikuta kwenye matatizo baada ya kukiuka taratibu za usajili. Kwanza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hutangaza kipindi cha usajili kulingana na muda.

Pili hutoa nafasi kwa klabu kutangaza wachezaji ambao haitawasajili kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kumalizika kwa mkataba, mgonjwa, anakatishwa mkataba ana anahama.

Tatu hutoa nafasi klabu kusajili wachezaji wapya kujaza nafasi zilizowazi kwa kuzingatia kanuni inayotaka kila klabu isiwe na wachezaji wa kigeni wanaozidi watano na isipangua wachezaji zaidi ya 10 wazalendo.

Kwa kuwa Yanga haikuwatema wachezaji hao nab ado ikasajili wachezaji wengine ikalazimika kuwatema Wisdom Ndlovu na winga John Njoroge. Wachezaji hao wanadai fidia ya kuvunjiwa mikataba yao.

Kadhalika Yanga inatakiwa kuwalipa Ali Msigwa na kipa Stephen Malashi waliotemwa ilhali wana mikataba halali. Wachezaji hao wote waliandika barua wakidai Sh milioni 168.

Yanga haikuwa na ubavu wa kulipa pesa hizo, lakini walipopata mawakili chini ya usimamizi wa Chama cha Wachezaji (Sputanza), kiwango kimepanda hadi Sh 252 milioni.

Deni lao limefikia kiasi hicho kutokana na kujumuisha masuala kadhaa ambayo hayakuwapo awali katika deni hilo.

Hoja ya Yanga kugoma kutoa fedha zilizopendekezwa na Sputanza ni kwa kuwa hailingani na mchango waliotoa katika klabu.

Fedha hizo ni za kuvunjwa kwa mikataba yao, pia malimbikizo ya mishahara na marupurupu kwa kipindi chote ambacho hawatokuwa na timu.

Kiburi ndicho kimeiponza Yanga kwani badala ya kutii kanuni ilishirikiana na timu nyingine za Simba, Azam FC na African Lyon kutaka kuigomea TFF juu ya kanuni hiyo.

Timu nyingine hazikuwa na mzigo mkubwa. Azam FC ililazimika kumtema kipa Ben Kalama wa Uganda ambaye alirudi kwao.

Simba ilizidisha mchezaji mmoja, ikamtoa Mike Barasa ikamhamishia African Lyon. Alikataa kuichezea klabu hiyo akaenda zake kwao Kenya japokuwa kisheria bado ni mchezaji wa Simba

Klabu nyingine zilizokumbwa na matatizo ya kanuni ya usajili ni African Lyon iliyopangua wachezaji zaidi ya 10 na ikabaki na kikosi cha wachezaji 18. Ilirekebisha kasoro hiyo ikakwepa adhabu ya kuondolewa kwenye mashindano.

Pamoja na tatizo hilo, leo Yanga inatarajiwa kwenda Morogoro kuumana na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu katika uwanja wa Jamhuri.

Ikiwa ikishinda itafikisha pointi tisa baada ya kushinda mbili za awali 1-0 dhidi ya Polisi Dodoma na 2-0 dhidi ya AFC ya Arusha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: