Yusuf Makamba: Mara joto, mara baridi...


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi

TABIA ya Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni ileile ya mara baridi, mara joto, mara vuguvugu na mara baridi, tena katika muda mfupi.

Kwa mbunge, mteule wa rais, kiongozi mkuu wa utendaji katika chama kinachopanga ikulu, kuwa na tabia ya kubadilika kila kukicha au pale kipenga kinapopulizwa; siyo ishara ya kuwa makini.

Joto linapokuja – kwa msukumo wa chama au makundi au mtu binafsi – Makamba anafura kwa hasira na kutangaza ubabe. Hivyo ndivyo alivyofanya baada ya vikao vya CCM vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu jijini Dodoma hivi karibuni.

Ilikuwa baada ya baadhi ya wajumbe wa chama chake kumkaripia Sitta, kumtishia, kumpa onyo na kutaka kumnyang’anya kadi ya uanachama, Makamba alipigilia msumari wa moto akisema, "Kama siyo CCM, Samwel Sitta ahojiwe na nani?"

"NEC ina ubavu wa kumdhibiti Sitta," alinukuliwa Makamba akisema na kuongeza kuwa wajumbe wa NEC walikasirika sana hadi kutaka kumnyang’anya kadi ya chama.

Ni Makamba huyuhuyu aliyesema, "CCM kinauwezo, mamlaka na madaraka ya kuhoji wabunge wake akiwamo spika wa Bunge la Jamhuri, kwa kuwa spika huyo ametokana na CCM."

"CCM ndiyo baba na ndiyo mama na Sitta na wabunge wenzake ni kama watoto," Makamba alinukuliwa akisema kwa shabaha ya kutetea kilichofanyika ndani ya halmashauri kuu ya chama hicho.

Ndani ya vikao vya CCM, Samwel Sitta alitwishwa tuhuma: kugonganisha bunge na serikali; kudhoofisha serikali; kuongea kwa muda mrefu kuliko wabunge; kupendelea baadhi ya wabunge wanaoisakama serikali na hata wapinzani, kwa kuwapa nafasi ya kuhutubia bunge.

Ikaja asubuhi, ikaja jioni, siku zikapita. Wiki mbili. Makamba yuleyule, akaenda jimbo la Urambo, mkoani Tabora. Huko ndiko nyumbani kwa spika Samwel Sitta. Akachukua sura ileile ya kuumbika na kuumbuka.

Aliwaambia viongozi wa chama chake vikaoni na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, kwamba CCM inatambua kuwa "Sitta anafanya kazi nzuri ya kuijenga CCM."

Ni wachache sana waliomshangilia Makamba. Wengi walipigwa na butwaa na walishindwa kuamini kilichokuwa kinatoka kinywani mwake. Alirudia kauli hizo mara mbili na wakati wote kauli zake ziligonga nyuso zilizokunjamana.

Alifanya zaidi ya hayo. Makamba alitembelea mama mzazi wa Samwel Sitta. Alimweleza mama huyo wa umri wa miaka 83, kwamba hana chuki na mwanae.

Ni Makamba huyo; anaumbika na kuumbuka au kuumbuliwa. Anafura kwa hasira, lakini dakika chache zifuatazo, anatoa kicheko – cha kweli au cha unafiki.

Joto la ndani ya vikao vya CCM ndilo lilifanya Makamba awe mkali, jeuri na aongee kwa kujiamini. Wajumbe walioongea kwa kukandia Sitta, tena mbele ya mwenyekiti wa chama na rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete, huku wakipendekeza afukuzwe uanachama, ndio walikuwa msukumo wa Makamba.

Msukumo mwingine ulikuwa "Kamati ya Mwinyi" iliyoundwa rasmi kuchunguza "msuguano" kati na baina ya spika, bunge na serikali kujaribu kuleta muafaka. Kamati iliundwa katika kikao cha Halmashauri Kuu.

Kwa maandalizi ya vikao hivyo vya Dodoma; kwa taarifa kwamba wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa wameandaliwa rasmi kumkabili Sitta na hivyo ndivyo ilivyojitokeza; na kwa wingi wa wajumbe walioongea kutaka "Sitta amalizwe," hakika Makamba asingekuwa na mtu wa kutembelea Urambo anayeitwa Samwel Sitta – spika.

Tabia ya Makamba ya kubadilika haraka – kutoka joto sana hadi baridi na kesho kuwa vuguvugu – huenda ndiyo inamfaa yeyote anayetaka kuwa katibu mkuu wa CCM ya sasa.

Akiombwa na kundi moja linalopingana na lingine kuwa aandae mazingira ya uhasama na mashambulizi, basi afanye hivyo. Akiambiwa sasa apoe, anakuwa kimya kama aliyekwenda safari.

Lakini akijisikia au akitekenywa kwamba amwakie fulani, kwa sababu zozote zile, atafanya hivyo. Vilevile akiamua au akiambiwa kurejesha amani, atawaangukia aliokorofishana nao na kukumbuka walivyopeana pipi wakiwa darasa la pili.

Makamba anakuwa mkuu wa maabara isiyofuzu – CCM. Hawaamini kuwa waliishamaliza utafiti juu ya utengenezaji hewa ya oksijeni. Kwao utafiti ni utafiti tu usioisha hata kama waliishapata matokeo; ili mradi waonekana wako kazini, wanalipwa na wanatumiwa na waajiri wao.

Safari ya Makamba nyumbani kwa Sitta imekuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa kubanwa na wananchi na balozi za nchi za kigeni zilizoko Dar es Salaam, kuhusu vitisho alivyofanyiwa spika na nia mbaya ya kumdhoofisha.

Kama kwamba Rais Kikwete alijua kuwa hali hiyo ingedhoofisha uhusiano kati ya serikali yake na wananchi, asasi za kijamii zinazopigania haki za binadamu na hata nchi wahisani, akatafuta jinsi ya kulegeza msimamo kwa kutoa "maelezo ya nyongeza" kwa yale yaliyotolewa na Makamba.

Rais Kikwete alisema wiki iliyopita, katika kujibu "maswali ya wananchi ya papo kwa papo" katika televisheni kwamba, halmashauri kuu iliyokemea wabunge "wenye msimamo mkali," ililenga tu kuleta nidhamu na siyo kuwatishia.

Alisema wabunge walikuwa wanatakiwa kujadili mambo ya chama chao ndani ya vikao vya chama na siyo hadharani; na kwamba kwa hatua hiyo, chama kamwe hakikulenga kuwanyamazisha.

Kama kauli ya Kikwete ilikuwa ndiyo kauli ya halmashauri kuu ya CCM, basi Makamba na ofisa wake mdogo John Chilligati, hawajui kuripoti na kuwasilisha taarifa za chama chao kwa wananchama, wananchi na dunia.

Lakini kama taarifa zao, na hasa Makamba, ziliwakilisha yaliyojiri ndani ya vikao vya chama chake; na kauli za Kikwete ni tofauti na zilizolenga kupoza wanachama na kurejesha "amani" ndani ya CCM, basi kuna mgogoro ndani ya chama hiki.

Bali kinacholeta nuru juu ya yaliyotendeka ndani ya vikao na iwapo yalilengwa; ni kwamba hakuna hatua yoyote aliyochukuliwa Makamba kwa kutoa taarifa tofauti na zile za chama na tofauti na kauli ya mkuu wa kaya.

Dunia ya nje isiyotafiti wala kuchokonoa, yaweza kuamini kuwa aliyosema Kikwete ni sahihi na yale ya Makamba ni kauli binafsi au taarifa za chama zilizotiwa hamila. Kumbe sivyo.

Makamba aweza kutumika kwenye sherehe na kwenye misiba. Ni mchekeshaji ambaye pia ni mlizaji. Leo kapewa ngwe ya kumpaka mafuta Sitta kwa mgongo wa chupa.

Bali ekyaizile mabele – hakuna mwenye uwezo wa kuzuia matiti kuota kifuati pale yakiishaanza kuchomoza.

Mambo mawili yako wazi. Kwanza, juhudi za makusudi za kugeuza vita dhidi ya ufisadi kuwa "mchezo wa kuigiza." Pili, kuziba midomo ya wabunge na spika kwa shabaha ya kudhoofisha mamlaka ya Bunge.

Inawezekana spika Sitta hayajui haya. Lakini kwa umri wake katika maisha ya kawaida na katika minyukano ya siasa, ana uwezo wa kung’amua nani anatumwa na nani kufanya nini.

Hadithi yatufundisha: Lini sungura anakuwa rafiki wa simba? Ni pale tu simba anapokuwa ameshiba au sungura anapokuwa na swala upandeni. Bali ni urafiki wa muda. Ni urafiki wa mashaka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: