Zahor Tamali: Wavuvi wangeokoa abiria


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version

MVUVI mzoefu anayeishi kijiji cha Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja anaamini shughuli za uokoaji baharini zinaweza kufanywa kwa ufanisi mkubwa pakiwepo maandalizi mazuri.

Zahor Tamali, ambaye amekuwa katika maisha ya baharini kwa miaka 20, anashauri serikali ianzishe mfuko maalum wa dharura wa fedha za kutumika wakati wa ajali.

Katika mahojiano maalum na MwanaHALISI juzi, Tamali amesema anaona inafaa shughuli za uokoaji zikawekwa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi. Ana sababu.

“Unajua idara hii inawajua wavuvi wote. Inashughulikia kamati za wavuvi Unguja na Pemba na inatoa elimu ya uvuvi endelevu.

“Serikali itumie hazina ya mkurugenzi wa uvuvi, anajua wavuvi na viongozi wao, na anawasaidia sana. Kila wakati yuko nasi.

“Huyu amekuwa bega kwa bega kuelekeza na kukagua shughuli zetu. Hasubiri ripoti ofisini huyu. Anakwenda mwenyewe mpaka chini ya bahari pima kumi akipiga mbizi bila hofu.

“Anajua hasa oganaizesheni ya baharini. Anazijua hifadhi zote Zanzibar. Ni rahisi kuwaongoza wavuvi kwa shughuli za kuokoa watu panapotokea chombo kuzama,” anasema Tamali.

Mkurugenzi wa Uvuvi Zanzibar ni Mussa Aboud Jumbe Mwinyi, mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania kwa miaka 12 – Aprili 1972 hadi 1984.

Tamali ambaye huuza samaki wake Soko Kuu la samaki Feri, Dar es Salaam, anazitaja hifadhi hizo kuwa ni MENAI inayohudumia Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Hifadhi nyingine ni MINCA inayohudumia Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kwa upande wa kisiwa cha Pemba, kuna hifadhi ya PECO. Hifadhi hizi zinasaidia kulinda mazingira nyeti ya baharini kwa maeneo yote Zanzibar.

“Kwa kuwa hawa tunawaamini sana na wao wanatujua kwa tabia zetu, kilichobaki ni serikali kutambua kuwa mchango wetu wavuvi katika uokoaji hauna mfano,” anasema.

Anahoji, “Kwani ni nani waliowahi kuokoa watu ilipozama Spice Islander kule Nungwi? Ni wavuvi pamoja na wawekezaji binafsi wa sekta ya utalii wanaomiliki boti za kasi.”

Tamali anasema uokoaji wa haraka na wenye ufanisi hufanywa na vyombo vidogo vikiwemo ngwanda, ngalawa na boti za fibre zinazofungwa mashine nje. Anasema kuna vyombo hivi vipatavyo 36,000 Zanzibar.

Anasema boti ya kisasa ya Police Marine, iliyotolewa msaada na Marekani, iliagizwa kwenda eneo la tukio, lakini “ilishindwa njiani (kabla ya kufika Chumbe) ikarudi.”

Hata ingefika anasema, ingeishia kuhangaika tu. Kwanini? Anasema, “Wafanyakazi wao hawana ujuzi wala uzoefu wa kuzamia kama tunavyofanya sisi. Hawajiamini.”

Anatoa mfano wa kilichotokea bandarini siku ilipozama mv Skagit. Boti kubwa ya kampuni ya Azam & Coastal Ferries ilitumwa eneo la tukio, lakini wazamiaji waliokuwa mbele na tayari kwa kazi ilikuwa ni wavuvi binafsi.

“Usidhani maskhara. Tunajuana na tunakutana kwenye kazi,” anasema Tamali ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Hifadhi ya MENAI na mwenyekiti wa diko (kituo cha uvuvi) la Kigaeni, Makunduchi.

Tamali anasema tatizo kubwa jingine la serikali na taasisi zake ni kuchelewa kuratibu kazi ya uokoaji chombo kinapozama. “Udhaifu huu unaongeza maafa,” anasema.

Anasema ilipozama mv Skagit, wavuvi wadogo ndio waliowahi eneo la tukio na kuanza kuokoa watu wengi kwa kutumia vyombo vyao hivyo vidogo vya mbao.

“Sasa mkurugenzi wa uvuvi angeamuru tu ‘nyie wavuvi, tokeni mkaokoe watu kule, mambo mengine baadaye.’ Ungeona wewe. Kila mtu angetoa chombo chake na kuchukua mafuta yake ya akiba akakimbilia kuokoa watu.

“Tungeelekezana sote tukakimbia kuwahi kuokoa. Tunajua idara ya uvuvi itarudisha mafuta yetu na hata kutoa kifuta jasho kwa waliotoa vyombo vyao na kushiriki kuokoa,” anasema Tamali.

Anasema kwa upande mwingine, serikali ingekuwa na mafuta ya kutosha ambayo ikitokea ajali baharini, inagawa mafuta kwa vyombo kwenye vituo vya Forodhani (kwa mjini) na Fumba (Magharibi, karibu zaidi na ukanda wa bahari kutoka Dar es Salaam) ambako wavuvi wangechangamkia kuokoa watu.

Anapoulizwa kama kushauri jukumu hilo lipelekwe Idara ya Uvuvi ana maana Idara ya Maafa ipunguziwe majukumu kwa kuwa hilo ni jukumu lake, Tamali anasema hata ikiwa hivyo “ni sawa.”

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)