Zama za giza zimepita


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Laurent Gbagbo

IWE kwa nguvu au la, ukweli ni kwamba sasa limebaki suala la muda tu kabla ya Laurent Gbagbo, kuachia ngazi kama kiongozi wa Ivory Coast.

Dalili ya kwanza kuwa Gbagbo hatadumu madarakani ni ukweli kuwa amekataliwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla wake.

Kuna kipindi jumuiya ya kimataifa humkataa kiongozi lakini akadumu pale mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi kama vile Marekani, Uingereza na Ufaransa yakimuunga mkono.

Tatizo ni kuwa Gbagbo haungwi mkono na taifa lolote kubwa. Ukijumlisha na wadau wengine katika jumuiya ya kimataifa kama vile Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Afrika (AU), ni wazi kuwa Gbagbo hawezi kushindana na presha hiyo.

Kwa hiyo ni suala la muda tu na itategemea pia ataahidiwa kitu gani akikubali kusalimu amri haraka na kuondoka Ikulu.

Kama ataamua kung’ang’ania, ni wazi subira ya jumuiya ya kimataifa itafutika. Hatari iliyopo ni kwamba ikilazimu kuondolewa kwa nguvu, kutaibuka upya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuiangamiza nchi na jirani zake ambako binafsi Gbagbo alisema, “zitalazimika kubeba wakimbizi.”

Hali hiyo ikitokea, mtu wa kulaumiwa zaidi atakuwa mmoja tu: Gbagbo mwenyewe.

Na si kwamba atabaki kulaumiwa pekee, ni lazima ajiandae kujibu mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu wa kivita kama alivyokumbwa Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia.

Dunia inazidi kuwa ndogo kwa wang’ang’aniaji madaraka na madikteta. Muda si mrefu, dunia itaanza kuwa sehemu isiyo salama kwa watawala wa aina hiyo.

Gbagbo huyu anayeleta shida leo, alikuwa kipenzi cha Ufaransa wakati wa harakati za kupambana na udikteta wa aliyekuwa rais Ivory Coast, Felix Houphouet Boigny.

Aliendelea kuwa kipenzi kwa Ufaransa na wapenda mageuzi wa nchi za magharibi wakati akipambana na utawala wa Henri Konan Bedie na baadaye Jenerali Robert Guei.

Lakini leo, baada ya kupingana na kila alichokuwa akikipigania awali, Gbagbo amekosa waungaji mkono hata wale ambao baadhi yake walikuwa ni rafiki zake.

Hii ndiyo dunia ya leo. Na ingawa ilijivuta hata kufikia kuwabana Robert Mugabe wa Zimbabwe na Mwai Kibaki wa Kenya walipong’ang’ania madaraka kwa wizi wa kura, ni wazi mambo yamebadilika. Uvumilivu kwa wachafuzi wa demokrasia unapotea kwa kasi duniani.

Hali hii haiku Afrika peke yake. Barani Asia, madikteta wa Burma, wamewekewa kibano kikali na jumuiya ya kimataifa hadi wakaamua kumuachia mwanaharakati na mwanasiasa maarufu, Aung San Suu Kyi.

Nchi hiyo ya barani Asia haina maliasili yoyote ya maana ya kuweza kuzivuta nchi za magharibi kuikimbilia kwa lengo la kuvuna raslimali hiyo kwa manufaa yao.

Hata hivyo, ukweli kwamba Umoja wa Mataifa (UN) uliamua kumtuma mjumbe wake, Ibrahim Gambari, kwenda kuzungumza na mkuu wa utawala wa kijeshi wa Burma, Jenerali Than Shwe, unaonyesha kuwa dunia inakerwa na kile kinachoendelea Burma.

Jambo zuri pekee linaloweza kuwa limeitokea dunia katika kipindi hiki ni ukweli kwamba mataifa mengi tajiri, hasahasa Marekani, yana hali ngumu kiuchumi kiasi kwamba hayana muda wa kuitibua jumuiya ya kimataifa.

Wala hali haiko hivyo tu Marekani. Mataifa mengine yenye uchumi mkubwa kama vile Ujerumani na Uingereza yako hivyohivyo. Hata Japan imeingia mkumboni.

Dunia siku hizi inapita katika kipindi ambacho wakazi wake wanategemeana kuliko katika kipindi kingine chochote cha historia ya mwanadamu.

Ukweli huu umeleta kuaminiana na kuheshimiana kwa kiasi fulani. Ndiyo maana, leo hata Gbagbo anaweza kuzungumza na Jacques Chirac na kumtukana bila ya hofu.

Miaka 40 hadi 20 iliyopita, hakukuwa na kiongozi barani Afrika, hasa kule ambako Ufaransa ilitawala, ambaye alithubutu kumtukana Charles de Gaulle, Georges Pompidou au Valery Giscard D’estaing.

Katika miaka ya 1970, aliyekuwa mtawala wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Jean Bedel Bokassa, aliwahi kuangua kilio kwenye mazishi ya Pompidou kwa kusema, “Baba, Baba, Baba….”

Hiyo ndiyo iliyokuwa Afrika ya zamani. Leo, Gbagbo anaweza kuhoji lolote kuhusu Rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy, kwa vile mkoloni huyo hana mchango tena kwa nchi hiyo ya Afrika kama ilivyokuwa zamani.

Rais Omar Hassan el Bashir wa Sudan ameruhusu unyama ufanyike dhidi ya wananchi wa Darfur na anaweza kukwepa mashitaka yake kwa sasa lakini wakati ukifika, hatma yake itajulikana.

Ni haki bin haki. Matukio yote haya yanapaswa kuchukuliwa kama fundisho kwa viongozi wa Tanzania wanaoota kufanya maasi zama hizi kwa kujidanganya kuwa wanaweza kulindwa na ‘wajomba zao’ nje ya nchi.

Zama za watawala kuua, kutesa na kunyanyasa raia kwa kisingizio chochote kile; iwe kulinda amani, mshikamano na umoja wa kitaifa au kudhibiti wapinzani, zimekwisha.

Kwa yule kiongozi anayetamani kutenda hayo, lazima ajue kuwa atakabwa na mkono wa sheria.

Waingereza wana kauli moja muhimu sana katika kueleza kile kitakachotokea: “You Can Run, But You Can’t Hide.” Maana yake ni kwamba “waweza kukimbia lakini huwezi kujificha.”

Ipo siku utapatikana. Na wala si katika maisha ya ahera; bali kama walivyoshughulikiwa Slobodan Milosevich wa Kosovo na Albert Fujimori wa Peru waliokufa wakisubiri hatima zao mahakama ya The Hague, mhalifu yeyote mwingine ajue atanaswa tu duniani.

0
No votes yet