Zanzibar kupata serikali ya umoja siyo mseto


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

HARAKATI kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe watakaounda timu ya watu sita itakayoratibu utekelezaji wa azimio la Baraza la Wawakilishi, ziko mbioni kukamilishwa.

Kwa kuwa sikuwa na uhakika iwapo uteuzi wao umewekewa muda maalum kufanyika, niliona ni vema nikautafuta kwa wanaohusika.

Niliwasiliana na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee. Nilipopiga simu yake ya mkononi Na. 0754 882967 sikupata jibu kwani iliita kwa muda mrefu bila kuitikiwa. Mzee aligoma hata kujibu ujumbe niliomtumia.

Ujumbe wenyewe ulikuwa: Ninataka kujua kama kuna timeframe (muda maalum) ya kupatikana kwa wajumbe 6 wa timu itakayoratibu utekelezaji wa azimio la BLW kuhusu maridhiano. Majina yanawasilishwa kwako Katibu au Spika?

Spika Pandu Ameir Kificho, anayetumia simu Na. 0773 190198 naye sikumpata kwani simu yake haikupatikana kwa muda mrefu.

Mwandishi mmoja wa habari aliyeko Zanzibar alinieleza kwamba kwa mujibu wa azimio lilivyopitishwa, hakuna muda uliowekwa katika uteuzi wa wajumbe hao. Bali alisema anadhani kwa dhamira iliyoonyeshwa na pande zote barazani, anatumaini uteuzi utafanywa “haraka.”

Taarifa za ndani ya serikali na vyama vya CCM (Chama Cha Mapinduzi) na CUF (Chama cha Wananchi) zinaonyesha kila moja inachukua hatua kuhakikisha haitakuja kulaumiwa kuwa imechangia kukwamisha matarajio ya wananchi.

Kwa namna mjadala wenyewe wa hoja binafsi iliyowasilishwa na Kiongozi wa Upinzani barazani na Abubakar Khamis Bakary ulivyokuwa wa maelewano, hakuna aliye tayari kutajwa kuwa amezorotesha utekelezaji wa azimio lililopitishwa.

Si uongo hata kidogo. Wananchi wanaangalia kwa karibu kila upande katika maridhiano. Wanataka kujua nani mbaya wao katika dakika hizi ambapo mwelekeo wa siasa nzuri umejitokeza na matumaini ya Zanzibar kupiga hatua katika mustakbali mwema yanazidi kujengeka.

Wanataka kila mhusika atimize wajibu wake ili asije kubebeshwa lawama. Wazanzibari wamechoka kulaghaiwa kila uchaguzi unapokwisha kupitia miafaka isiyotekelezwa. Wanataka mabadiliko ya kweli nchini kwao.

Watu wa Unguja na Pemba wanataka kupiga mstari mwekundu katika kumbukumbu mbaya wanazozijua – iwe kwa kushuhudia maovu wakitendewa wao binafsi au walivyosimuliwa na waathirika – ili watazame yaliyo mbele yao.

Viongozi wakuu wa siasa wa CCM, Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad walishasema wamekubali kusameheana na sasa kwa pamoja wanaelekeza nia zao nzuri kuhimiza ujenzi wa Zanzibar mpya. Tuliobaki tunafuata nyayo zao.

Wiki iliyopita nilieleza haja ya Rais Karume kuharakisha utekelezaji wa dhamira yake njema ya kujenga siasa safi kabla ya kutua mzigo wa uongozi, kwa kuanza kuteua watu wa kuwapa dhamana katika serikali bila ya kusita.

Akifanya hivyo mapema atakuwa anazidi kudhihirisha alivyo na utashi wa kweli wa kuleta mabadiliko yaliyokosekana kwa miaka mingi Zanzibar.

Lakini, kwa kubadilisha serikali kipindi hiki kupitia mamlaka aliyonayo kikatiba, Karume pia atakuwa anatengeneza utaratibu mzuri wa kuja kuachia hatamu za uongozi pasina mazonge. Na hiyo ndiyo historia muhimu tunayomhimiza aiandike.

Tuna muda mdogo kufikia uchaguzi mkuu Oktoba na iwapo patakuwa pameshafanywa marekebisho ya sheria ya uchaguzi kwa lengo la kuwezesha uchaguzi kuahirishwa, maana yake ndiyo nafasi ya serikali ya umoja wa kitaifa kufanya kazi.

Uzoefu utakuwa umepatikana kama rais Karume alishaanza kujenga uongozi mpya unaozingatia spiriti ya ushirikiano, baada ya kupangua serikali ya sasa ili kupisha serikali inayojumuisha viongozi wa CCM na CUF.

Nimesema hakuna kifungu chochote katika Katiba ya Zanzibar ya 1984 wala ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kinachomzuia kufanya hivyo.

Katiba zote hizi mbili hazina hata mahali pamoja zinapombana rais kwamba baada ya uchaguzi mkuu wakati wa kuunda serikali basi ateue mawaziri na naibu mawaziri wa chama kilichompitisha tu kugombea urais. Hakuna!

Ninakumbuka sana maneno ya Ali Mzee Ali, mwakilishi wa kuteuliwa na rais lakini akiwa pia ni Mwenyekiti wa baraza la wawakilishi (anayekalia kiti cha enzi wakati naibu spika anapodharurika):

“Hapana mahala pazuri kama serikali ya shirikisho, umoja wa kitaifa ni mhimili mkuu katika nchi.” Wananchi wanataka hekima ionyeshwe kwa vitendo siyo hisia peke yake.

Serikali ya Umoja

Wapo watu hawajaelewa tofauti ya serikali ya umoja wa kitaifa na serikali ya mseto. Hivi ni vitu tofauti kinadharia na kihalisia.

Kwa mujibu wa azimio la Baraza la Wawakilishi, serikali inayohitajika kuwepo Zanzibar ni serikali ya umoja wa kitaifa, siyo ya mseto.

Nilifafanua jambo hili katika kipindi cha Tuongee asubuhi kinachorushwa kila siku na kituo cha televisheni cha StarTV Dar es Salaam, Jumapili.

Serikali ya mseto ni ile inayoundwa na vyama zaidi ya kimoja kikiwemo chama kiongozi katika matokeo ya uchaguzi mkuu lakini hakikupata kura za kutosha kikatiba kukiwezesha peke yake kuunda serikali.

Kwa mfano, tuseme Katiba inasema chama kitakachounda serikali ni kile kilichopata asilimia 50 ya kura zote za bunge. Chama A kimepata asilimia 40 na ndiyo cha juu ya vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi.

Kipo Chama B kimepata asilimia 20 ya kura. Hiki ndio chama cha pili baada ya chama A na kitabaki kuwa chama kikuu cha upinzani bungeni. Chama A kitahitaji asilimia 10 ili kiunde serikali.

Hapa kitalazimika kuomba kushirikiana na chama kimoja au viwili vilivyopata kura chache ya kile chama B ili kufikisha asilimia 50 ya kura zinazotakiwa na katiba kukiwezesha kuunda serikali.

Hii ndio serikali ya mseto. Kwa sasa serikali kama hii ipo nchi nyingi zikiwemo India, Ujerumani na Israel.

Serikali ya umoja wa kitaifa ni ile inayoundwa na vyama zaidi ya kimoja – vyaweza kuwa viwili tu – vilivyoingia katika majadiliano kwa nia ya kutatua mgogoro wa kiuongozi unaokabili nchi. Mfano mzuri ni Kenya na Zimbabwe.

Aghalabu serikali ya aina hii hutokana na muafaka baada ya kutokea mgogoro unaoweza kuwa umesababishwa na mabishano ya matokeo ya uchaguzi au mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa.

Zanzibar iliwahi kuwa na serikali ya mfumo huu baada ya uchaguzi wa mwaka 1963. Ilishirikisha vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).

Mohamed Shamte ndiye aliyekuwa waziri mkuu wa serikali hiyo na alifanikisha kuipeleka Zanzibar kwenye Umoja wa Mataifa ambako ilipata kiti chake kama mmoja wa wanachama wa umoja huo.

Serikali hiyo iliyoundwa kufuatia uhuru wa 10 Desemba 1963, iliangushwa baada ya siku 33 tu – kwa mapinduzi ya 12 Januari 1964 – kwa kile kilichoelezwa na waasisi wa Afro Shirazi Party (ASP) kwamba haikuwa serikali halali ya wazalendo bali vibaraka wa utawala wa Kisultani uliokuwa unahifadhiwa na Uingereza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: