Ze Comedy watang'ara bila uhuru?


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version
Ze Comedy

SWALI kubwa ambalo watazamaji wa televisheni wanajuliza ni: "Waigizaji wa Ze Comedy" wamehama Cannel 5 ya East Africa Television (EATV) na kwenda TBC, je watabakia na uhuru waliokuwa nao?"

Waigizaji walikuwa wanaigiza rais, waziri mkuu, wabunge, wananchi wa rika na nyadhifa mbalimbali. Kikubwa zaidi walikuwa wanamwigiza hata mwenye chombo walimokuwa wanaonekana.

Ni uhuru uliotamalaki. Ni fursa nyingine ya kufikiri bila kikwazo na kutoa ujumbe unaomaini kuwa hakika ni maoni unayosimamia, hata kama yameongezwa chumvi kidogo ili yatimize shabaha yake: Kufurahisha na kustarehesha.

Ze Comedy walikuwa wanaonekana katika chombo kilichoko chini ya makampuni ya IPP. Miezi minane baadaye, na hiyo ni baada ya kupata jina na kukubalika kuwa wanaweza kuwa huru na kupambanua masuala mbalimbali kwa njia ya maigizo, sasa wamehama.

Wamehamia TBC – Shirika la Utangazaji Tanzania. Tayari wameanza kuonekana. Jumamosi iliyopita walikuwa kwenye kioo wakiburudisha watazamaji wakati wakisubiri pambano kati ya taifa Stars na Cameroon kuanza na wakati mwingine katikati na mwishoni mwa maonyesho.

Hiyo ndiyo nafasi mpya ya Ze Comedy au "Zee Comedi" kama ambavyo jina lao lilionekana Jumamosi kwenye kioo. Kwa mtazamo wa haraka mtu aweza kuona kuwa kazi yao sasa inaweza kuwa tofauti na ilivyokuwa Channel 5.

TBC ni chombo cha umma. Kwa Tanzania ambako kutaja umma ni kutaja serikali, TBC bado inaonekana na inaweza kutumiwa na serikali. Na hivyo ndivyo ilivyo.

Kwa kuangalia kilichotokea Jumamosi na jinsi Zee Comedi walivyotumika, yawezekana ukawa ndio mtindo wa kila siku; na kama hivyo ndivyo, basi huo utakuwa msiba mkubwa kwa wasanii hawa.

Kwani huu ni mtindo wa "njoo unifanyie hili," au "igiza huyu afanane yule," au "tusaidie kuchekesha watu pale?unajua ninyi mna uwezo bwana." Wakienda kwa mtindo huo, uwezekano wa kutosonga mbele utakuwa mkubwa.

Ni hapo ambapo watazamaji wa Ze Comedy kwa miezi minane katika Channel 5 ya EATV wanauliza, iwapo huko walikokwenda watakuwa na uhuru wa kufanya mambo yao bila kutumikishwa kisiasa.

Hata kabla ya kutangaza uamuzi wao wa kujiengua kuonyesha vichekesho vyao kupitia Channel 5, fununu zilitawala kwamba wasanii wanaounda kundi hilo maarufu la vichekesho nchini wana mpango wa kujiunga na TBC.

Kundi hili linaloundwa na vijana sita ambao kwa majina yao ya kisanii ni Masanja, Vengu, Wakuvanga, Joti, Mpoki na Mac Reagan, pamoja na mtayarishaji wao Seki kwanza walikana, mbele ya waandishi wa habari, taarifa za wao kutaka kujiunga na TBC.

Awali walisema wanataka kupumzika kwa kuwa walifanya kazi kwa muda wa miezi minane mfululizo. Eti "walichoka!"

Hatimaye wiki mbili zilizopita walitoboa siri. Wakafuta fununu na kuanika ukweli. Wakayathibitisha yale yaliyokuwa yanasemwa na mashabiki wao. Wakaweka hadharani, kwamba sasa wamejiunga rasmi na TBC kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Hii ni taarifa njema kwa wapenzi wa kundi hili, walioanza kusikitika baada ya kuwasikia wasanii wenyewe wakidai kupumzika kwa muda usiojulikana. Wapenzi wa vichekesho wanataraji kuona yale waliyoyakosa kwa muda wa wiki kadhaa sasa.

Kundi hili, kwa mujibu wa taarifa za awali mara baada ya kujiengua Channel 5, lilikuwa lisafiri kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mafunzo ya kisanii kwa muda wa mwezi mmoja.

Safari hiyo ambayo imefahamika kuwa ingedhaminiwa na mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini, Yusuf Manji bado haijafanyika. Chuo na mji ambako mafunzo yatafanyika havijatajwa.

Bali ni vema wasanii hawa wakachukua tahadhari katika kauli na matendo yao baada ya kujiengua Channel 5. Ila mimi nataka kuwatahadharisha mambo mawili makubwa wasanii hawa kufuatia maneno machafu waliyoyatoa baada ya kujiengua.

Wanadai walikuwa wananyonywa na mmiliki wa kituo walimokuwa wakionekana na kwamba sasa wamempata mtenda haki. Hili naliona kama kumtukana mkunga wakati uzazi ungalipo.

Ina maana wasanii hawakuyaona hayo wakati hawajampata huyo bosi mpya wanayemwita "mtenda haki?" Ni juzi tu wamerudia kauli kwamba hapo TBC wamepata "mteremko?siyo njaanjaa."

Sikatai kuhama au kubadilisha sehemu ya kazi kutokana na kuahidiwa maslahi mazuri zaidi ya unayopata. Kila mtu anataka kuwa na maslahi mazuri zaidi.

Bali kwa muungwana, si busara kumtupia kashfa aliyekuhifadhi wakati unatafuta sura; wakati unaumbika na unatafuta upenyo. Ukipata pazuri zaidi, aga tena kwa matumaini na kauli za "tutakutana tena."

Katika mazingira mazuri ya kuhama kwa ustaarabu, huenda kule ulikokwenda mambo yakawa magumu nawe ukaamua kurejea "nyumbani." Ukirejea unakaribishwa kwa kuwa, kama wasemavyo vijana mijini, unakuwa "hukunyea kambi."

Wasanii hawa wanatarajiwa kuwa kioo cha jamii; hivyo wanapaswa kuonyesha mfano bora kwa wengine. Kwa mfano kukumbuka walikotoka na kujua kuwa ":maisha ni mzunguko," kwani wanaweza kurejea hapo.

Ukitoka mahali ukiwa umelikoroga na ukijua kuwa hata ukitaka kurudi hakuna atakayekukubalia, basi huko uendako, hata wakikunyanyasa, utabaki hukohuko, katikati ya manyanyaso na utumwa. Katika mazingira hayo utashindwa hata kufikiri vizuri na kujenga vipaji vyako vya usanii.

Kwa hiyo, hata kama maslahi yao awali yalikuwa madogo, wasanii wa Ze Comedy wanapaswa kuishukuru Channel tena kwa kuwatangaza, kuwalea na kuwakomaza hadi walipofikia. Tayari historia imenukuu hilo na halifutiki.

Kuna wasanii wengi hapa nchini wenye uwezo wa kuigiza kama au kuliko wale wa Ze Comedy, lakini TBC hawakuwataka.

Hawakuwataka kwa sababu hawajaziona kazi zao. Wamewachukua Ze Comedy kwa sababu wameona uwezo wao kupitia EATV. Kwa nini wasikishukuru kituo hicho kwa kuwafungulia milango?

Tunasubiri kuona wasanii hawa wakiwaigiza viongozi waliomo serikalini au bungeni ambao walitajwa kwenye orodha ya "mafisadi." Wataweza?

Lazima waweze. Wasipoweza watateleza. Wakiteleza wataanguka. Wakianguka watapotea. Wakipotea watasahaulika. Wakisahaulika, basi! Historia itaandika – walikuwepo.

Kama nilivyoeleza hapo awali, sifa na heshima ya kundi hili ilitokana na uhuru uliotolewa na mwenye kituo walimokuwa wakiigizia kazi zao. Wanahitaji uhuru uleule, vinginevyo wataangamia katika kiza – huko walikotokea.

Sitaki kuamini maneno ya shabiki mmoja wa kundi hili. Yeye aliniambia kwamba wasanii hawa wamenunuliwa makusudi ili kuwaziba midomo kutokana na uigizaji wao wa "kuwapiga madongo viongozi mafisadi."

Tunaloweza kusema hapa ni, "Hebu tusubiri na tuone."

0
No votes yet