ZEC: Tume ya uchaguzi inayofurahia uchafuzi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 July 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KATIBA ya Zanzibar, ya mwaka 1984, ina mambo mengi mazuri yanayoelekeza haki za wananchi. Kwa maana ya mjadala wa leo, nagusa baadhi tu ya vifungu hivyo vinavyoelekeza ulinzi na ustaarabu wa kujali haki za wananchi wa Zanzibar.

Kifungu cha 5 cha Katiba, kinasema: Zanzibar itafuata mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa wenye kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu, usawa, amani haki na uadilifu.

Sura ya Pili ya Katiba kuna maneno yasemayo, "Malengo na Maamuru Muhimu ya Sera ya SMZ." Katiba inaeleza mantiki ya serikali katika kifungu cha 8:

Itakuwa ni wajibu wa vyombo vyote vya Serikali pamoja na vyombo vingine vyenye uwezo pamoja na watu wenye kutunga sheria kiutawala au uwezo wa kimahkama kufuata misingi ya uhuru, haki na amani.

Kifungu cha 9, kijifungu (1) kinaendeleza fungu: Zanzibar itakuwa ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii. Kijifungu cha (2) kinaendeleza: Kwa hivyo hapa inaelezwa rasmi kwamba:

(a) Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe;

(b) Usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la Serikali;

(c) Katiba hii itahakikisha kwamba wananchi wanashiriki katika Serikali yao.

(3) Muundo wa SMZ pamoja na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.

Ni maneno adhimu yaliyomo kwenye Katiba ya Zanzibar ambayo ndio muongozo pekee wa kisheria unaopaswa kutumika na kufuatwa na viongozi wenye dhamana ya kuendesha serikali.

Mwananchi anayeishi ndani ya mipaka ya Zanzibar, kama inavyotambuliwa na Katiba ya Zanzibar, anatambulika na anazo haki nyingi zilizowekewa miongozo kuhusu vipi ziheshimiwe.

Kifungu cha 6 cha Katiba kinasema: (1) Kutakuwa na Mzanzibari ambaye upatikanaji wake, upoteaji wake na urudishwaji wake atakuwa kama alivyoainishwa katika sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi (BLW).

Bado tunaonyeshwa manufaa ya kikatiba anayopewa Mnzazibari. Kijifungu (2) kinasema: Kila Mzanzibari, kwa misingi ya Katiba hii, ataweza kufaidi haki na fursa zote anazostahiki Mzanzibari, na atapaswa kutekeleza wajibu, majukumu na dhamana za Mzanzibari kama ilivyo kwenye Katiba hii au kwenye sheria iliyotungwa na BLW.

Kifungu cha 7, kijifungu cha (1) cha Katiba kinasema: Kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Zanzibar na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya kijifungu cha (2), cha kifungu hiki pamoja na masharti mengine ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika Zanzibar kuhusu mambo ya uchaguzi.

Mjadala unapamba moto. Katiba inatoa kila kitu, hata vile ambavyo havitajwi kikawaida. Inatoa fursa nyingi, hata zile ambazo mtu wa kawaida hawezi kuzifikiria. Tunayo katiba murua kwelikweli.

Sasa tushaambiwa kila Mzanzibari ana haki ya kushiriki katika serikali. Anashiriki kwa njia ipi? Katiba inasema akitimiza umri wa miaka 18, anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi.

Uchaguzi ambao Mzanzibari anayo haki ya kushiriki ili apate ile haki nyingine ya kushiriki katika serikali ya nchini kwake, unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), chombo mahsusi kilichoundwa kwa sheria ya Baraza la Wawakilishi na kupewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa Zanzibar.

Tuendelee kujadili. Kijifungu (2) cha Kifungu cha 7 cha Katiba – kile kitoacho haki ya kupiga kura kwa kila Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 18 – kinaelekeza mamlaka ya kuwepo sheria (itakayotungwa na Baraza la Wawakilishi), inayoweka masharti yanayoweza kuzuia Mzanzibari kutumia haki hiyo ya kupiga kura.

Katiba inataja sababu kupitia kifungu hiki. (a) kuwa na uraia wa nchi nyingine; (b) kuwa na ugonjwa wa akili uliothibitishwa na Mahakama Kuu; (c) kutiwa hatiani na kuendelea kutumikia adhabu kwa kosa la jinai katika Chuo cha Mafunzo (Magereza), isipokuwa kwamba mtu aliyewekwa rumande atakuwa na haki ya kuandikishwa kupiga kura.

Kijifungu cha mwisho, (d), kinasema: kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura (maana yake atakapokuwa na shahada ya uchaguzi aliyotumia uchaguzi kabla).

Vifungu hivi vinatufunza nini? Katiba imeziba mianya yote inayoweza kutumiwa kunyima mtu haki ya kupiga kura. Kumbe hata mahabusu ana haki hiyo. Anaipata?

Wakati huu ZEC wakiandikisha wapiga kura wapya ili waingizwe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK), inakabiliwa na lawama na shutuma nyingi za kutosaidia wananchi ili waandikishwe na kuingizwa kwenye daftari hilo.

Ni wakati wa vijana waliotimiza miaka 18 kuendelea na wale wasiopiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita, kufika mbele ya watendaji wa tume ili waandikishwe.

Hata hivyo, hiki kinachoitwa kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi kimekuwa kama punju. Baada ya ZEC kukikataa kisihusishwe na uchaguzi mwaka 2005, wameshindwa kuweka utaratibu utakaorahisisha wasionacho wakipate ili nao waandikishwe.

Kibaya zaidi, watendaji wa ZEC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salum Kassim Ali, wanatetea kutohusika kwao na kitambulisho. Wanadhani watu wanataka watoe wao kitambulisho. Sivyo.

Suala hapa ni Tume kutambua dhamana waliyonayo kikatiba ya kuhakikisha kila mwenye haki ya kupiga kura anaandikishwa na kuingizwa kwenye daftari. Watendaji wa tume wana wajibu wa kuchukia waonapo makundi ya watu wanaofika vituoni wanafukuzwa kwa kukosa kitambulisho.

Panatakiwa uwajibikaji. Viongozi wa ZEC wakerwe kuona watu hawaandikishwi. Si haki imetolewa na Katiba? Si mianya imezibwa ili mtu asikose kuandikishwa? Vipi kiwekwe kitambulisho wakati katiba inatambua shahada, cheti cha kuzaliwa na kadi ya uraia ambayo haipo?

Halafu Tume waseme si jukumu lao kuondoa kikwazo hiki cha mtu kuandikishwa ili aingie kwenye daftari?

Kama taasisi ya kidola, Tume itathibitisha uadilifu wake kwa kufuata Katiba ambayo inahimiza utendaji wa haki. Inapaswa kuondoa urasimu kwani kwa wananchi, huduma ndiyo muhimu kuliko yote.

ZEC haitafika hapo iwapo inafurahia – au hata kule kutosaidia wanaokwama kuandikishwa – kuona makundi ya watu wanaopaswa kuandikishwa wanafukuzwa kutoka vituoni kwa misuli ya Idara ya Usalama wa Taifa, Polisi na vikosi vya SMZ.

Hivi Tume inatoa mchango gani katika vifungu vya katiba hivi vinavyolinda haki za wananchi, ikiwemo ya kushiriki katika serikali iwapo haisaidii mtu asiyeandikishwa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: